Daktari Msaidizi wa Zahanati ya Rwamchanga, Miriam Martine amefikishwa
Mahakama ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kujibu mashtaka ya
kusababisha kifo cha mtoto mchanga na kushindwa kumzalisha mama yake.
Akimsomea
mashtaka juzi mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Emmanuel Ngaile,
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Paschael Nkenyenge alidai kuwa Mei 15,
katika zahanati hiyo, mshtakiwa huyo alishindwa kumzalisha mama huyo,
Mugesi Juma kwa uzembe na kusababisha mtoto huyo ambaye ni pacha kufa.
Mshtakiwa
huyo alikana shtaka na kupatiwa dhamana ya Sh5 milioni za maneno baada
ya wadhamini wawili kukidhi masharti yaliyowekwa na mahakama hiyo,
ikiwamo mmoja kuwa mtumishi wa umma. Kesi hiyo namba 85/2016,
iliahirishwa hadi Mei 27, itakapotajwa tena.
Mkurugenzi Mtendaji
wa halmashauri ya wilaya hiyo, Naomi Nnko alimsimamisha kazi daktari
huyo siku moja baada ya kutokea kwa tukio hilo.
Wakati huohuo;
Mwalimu wa kujitolea wa Shule ya Sekondari Nagusi wilayani Serengeti, Fikiri
Bunduki Mochemba (22) mkazi wa Kijiji cha Singisi amefikishwa mahakamani
hapo kujibu shtaka la kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha pili (17)
shuleni hapo.
Mshtakiwa alikana shtaka na kurudishwa rumande hadi Juni mosi.