Serikali
inatarajia kumwaga ajira kwa askari katika mwaka ujao wa fedha.Taarifa
juu ya ajira hizo, zilitolewa jana bungeni na waziri mwenye dhamana.
Akiwasilisha
Makadirio ya Mapato ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2016/17 kuhusu
ajira za askari, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
alisema wataajiriwa askari wapya 3,700 katika mwaka wa fedha 2016/17.
Waziri Kitwanga alisema mbali ya kuajiri askari hao, pia watawapandisha vyeo askari 7,140, wakaguzi 1,325 na maofisa 991.
Alisema
katika mwaka 2015/16, jumla ya askari polisi wapya 3,882 waliajiriwa,
na askari wakaguzi na maofisa 4,065 wa vyeo mbalimbali walipandishwa
vyeo kwa kufuata utaratibu wa ajira.
“Aidha,
serikali imeendelea kuhuisha viwango vya mishahara na posho mbalimbali,
ikiwemo posho ya chakula ambayo iliongezwa kutoka Sh 180,000 hadi
kufikia Sh 300,000 kwa mwezi,” alieleza Waziri Kitwanga.
Alisema
katika mwaka ujao wa fedha, Jeshi la Polisi litaongeza umakini katika
kusimamia nidhamu kwa askari wake kwa kufanya uchambuzi wa kina
(vetting) kwa kuchukua vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT), wanaoomba kujiunga na Jeshi la Polisi ili kuwa na askari
wenye nidhamu na moyo wa dhati wa kulitumikia Taifa kwa ujumla.
Kwa
upande wa Jeshi la Magereza, alisema linatarajia kutoa mafunzo kwa
maofisa na askari 4,975 katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na yale
ya Taaluma ya Urekebishaji.
Alisema
ili kukabiliana na changamoto ya uchache wa miundombinu ya makazi kwa
askari Polisi, serikali kupitia mkopo kutoka Serikali ya China
inakusudia kujenga nyumba 4,136 chini ya usimamizi wa Shirika la
Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi.
Akizungumzia
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, alisema jeshi hilo linahitaji vituo 152
Tanzania Bara, lakini kwa sasa lina vituo 57 na kati ya hivyo, 38 vipo
katika miji na 19 katika viwanja vya ndege.
Alisema huo ni upungufu wa vituo 95 hali inayosababisha maeneo mengi kukosa huduma za zimamoto na uokoaji.
Inategemea
kujenga kituo kimoja cha zimamoto na uokoaji katika eneo la Kigamboni
katika Jiji la Dar es Salaam na kuendelea na ujenzi wa Jengo la Makao
Makuu Tazara - Mchicha, Dar es Salaam.
Aidha,
alisema Jeshi la Polisi litaendelea kupambana na makosa yanayovuka
mipaka hususani ugaidi, uharamia, biashara ya dawa za kulevya, biashara
haramu ya kusafirisha binadamu, wizi wa vyombo vya moto hususani magari,
wizi wa kutumia mitandao ya Tehama, bidhaa bandia, na biashara haramu
ya silaha na uchafuzi wa mazingira.
0 comments:
Post a Comment