Tuesday, May 3, 2016

Ugonjwa Mpya Usiojulikana Waibuka Nchini


UGONJWA usiojulikana jina wala chanzo chake, umeingia nchini kupitia Mkoa wa Kigoma, imeelezwa.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilisema jana kuwa hadi sasa watu 1,467 wamegundulika kuugua ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, ugonjwa huo uliripotiwa tangu Aprili 23 mwaka huu katika Vijiji vya Songambele, Buhigwe na Mulele wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Hata hivyo, hakuna taarifa zozote kuhusu kutokea vifo na uchunguzi unaendelea na hakuna kifo kilichoripotiwa.
Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema Dar es Salaam jana kuwa  watu waliopatwa na ugonjwa huo wamekuwa na dalili zinazofanana.

Alisema wagonjwa  hupatwa na homa kali, kichwa kuumwa na kulegea mwili.
Dalili nyingine   ni maumivu ya viungo, maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika na kizunguzungu.

Mwamwaja alisema matibabu kwa wagonjwa hao yanaendelea   na timu ya wataalamu tayari ipo mkoani Kigoma kwa ajili ya uchunguzi   wa ugonjwa huo.

“Wagonjwa 1,467 wana dalili za homa, kuumwa kichwa, kulegea mwili, maumivu ya viungo, maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika na kizunguzungu.

“Kijiji cha Songambele ndicho kimeripotiwa kuwa na wagonjwa wengi zaidi kikiwa na asilimia 68 ya wagonjwa wote.

“Matibabu yanaendelea kwa wagonjwa wote na timu ya wataalamu ipo mkoani humo kufuatilia kwa karibu chanzo zaidi cha ugonjwa huo,” alisema Mwamwaja.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger