Showing posts with label Jamii. Show all posts
Showing posts with label Jamii. Show all posts

Friday, May 20, 2016

Atiwa Mbaroni Kwa Kumbaka Mtoto wa Miaka 7

Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia mkazi wa eneo la Bombambili, Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kukutwa akimbaka mtoto wa miaka saba anayesoma darasa la pili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuber Mwombeji alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Mei 18 mwaka huu saa 11 jioni nyumbani kwao na mtoto huyo.

Alifafanua kuwa siku ya tukio mkazi huyo alikwenda sehemu hiyo kuangalia runinga sebuleni na baada ya muda mfupi binti huyo alirejea nyumbani akitokea shule.

“Msichana huyo alikuja sebuleni kuangalia runinga wakati huo wafanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo walikuwa nje na ndipo kijana alipopata mwanya wa kufanya ukatili huo,” alisema kamanda.

Alisema baada ya muda mfupi kupita, mfanyakazi wa kike aliingia sebuleni ghafla na kumkuta akimbaka mtoto huyo.

Alifunga mlango, kisha aliwaita majirani na viongozi wa Serikali wa mtaa huo.

Kamanda alisema wananchi walimkamata mtuhumiwa na kumpeleka polisi. Pia, mtoto huyo alichunguzwa na madaktari walithibitisha kuwa aliingiliwa kimwili na kuharibiwa sehemu zake za siri.
Share:

Wednesday, May 18, 2016

Waliombaka na Kumlawiti Binti wa Miaka 21 Morogoro Wapandishwa Kizimbani

WATU sita wanaodaiwa kumbaka na kumlawiti msichana kisha kumrekodi na kusambaza video hiyo, leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni pamoja na Iddi Adamu Mabena (32) Mkazi wa Njombe na Zuberi Thabiti (30) Mkazi wa Mbalali, Mbeya ambapo kesi hiyo inasimamiwa na waendesha mashtaka watatu wa serikali- Grolia Rwakibalila, Edgar Bantulaki na Kalistus Kapinga.
Akisoma maelezo ya kosa katika shtaka la kwanza la kubaka na kulawiti, Wakili Rwakibalila aliwataja wahusika kuwa ni pamoja na Iddi Adamu na Zuberi Thabiti.
Mwendesha mashataka huyo amedai kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja huku wakijua kufanya hivyo ni kosa, walimbaka na kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 21 na kumsababishia maumivu makali.
Wakili huyo alidai kuwa, washtakiwa hao walimbaka na kumuingilia kinyume na maumbile msichana huyo tarehe 27 Aprili, saa 1 usiku katika  nyumba  ya  kulala  wageni ya Titii iliyopo  katika Tarafa  ya  Dakawa  Wilaya  ya  Mvomero.
Hata hivyo, mawakili wote wa serikali walipinga dhamana ya washtakiwa hao kwa madai kuwa, kesi hiyo imegusa hisia za watu wengi hivyo kwa usalama wao pia kuhofia kuharibu ushahidi ni bora waendelee kushikiliwa.
Mbele ya Marry Moyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi washtakiwa hao walikana kuhusika na mashtaka hayo ambapo wamerudishwa rumande baada ya kukosa dhamana. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Juni Mosi mwaka huu na kwamba, upelelezi haujakamilika.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wakiwa na wenzao wanne walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kusambaza picha chafu za ngono katika mtandao wa kijamii wa whatsapp.
 
Edgar Bantulaki, mwendesha mashataka amedai kuwa, washtakiwa hao wamefanya kosa hilo chini ya kifungu cha sheria namba14 (1) (b) na 2 (b) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.

Bantulaki amewataja washtakiwa wengine kuwa ni pamoja na mshtakiwa namba 1 na 2 na Rajabu Salehe, (30), Ramadhani Ally (26), Muhsin Ng’ahy (36), John Peter (24) wote wakiwa ni wakazi wa Wami, Dakawa wilayani Mvomero.
 
Mwendesha mashtaka huyo amedai kuwa, washtakiwa wote kwa pamoja walianza kusambaza picha hizo kati tarehe 28 hadi 30 Aprili mwaka huu wilayani Mvomero na mkoa mzima wa Morogoro kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp.
 
Hata hivyo Ignas Kunge, wakili wa mshtakiwa wa nne (Ally) aliiomba mahakama kumpa dhamana mshtakiwa wake jambo lililopingwa na mawakili wa serikali kwasababu suala hilo limegusa jamii zaidi pia kwasababu za kutoingilia na kuharibu upelelezi wa kesi hiyo.
 
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Ivan Msaki, washtakiwa hao walikana kuhusika na shtaka hilo ambapo wamerejeshwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Juni Mosi mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa kwa kujadiliwa suala la dhamana iliyopingwa kwa kiapo na mawakili wa serikali.

Urlich Matei, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amesema, washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani kati ya 11 waliokuwa wakituhumiwa kuhusika na tuhuma hizo kufuatia upelelezi kutokamilika dhidi yao.

Kamanda Matei amesema, katika hatua za awali upelelezi kipolisi ulikamilika kwa watuhumiwa sita wa mwanzo ambao ndio wamefikishwa mahakamani.

Aidha amesema kuwa, vitendo vilivyofanywa na watuhumiwa ni vibaya na ambavyo kamwe haviwezi kuvumiiwa na jamii katika nchi.
 
Hivyo ametoa rai kwa wananchi kuacha kufanya uhalifu kwa kutumia mitandao kwani sheria yake iliyopitishwa na bunge hivi karibuni haitamwacha mtu akiwa salama.
 
Hata hivyo kamanda huyo ameomba polisi wapewe kifaa kama cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru na kukamilisha mwenendo wa kesi mapema.

Amesema, kwa sasa uhalifu kwa njia ya mitandao unakuwa kwa kasi duniani kote na kwamba, mtu anaweza kutenda makosa mengi yanayosumbua jamii ikiwemo wizi mkubwa na mdogo wa fedha kwenye benki, makosa ya udhalilishaji, lugha za matusi na mengine mengi.

Amesema kuwa, kupatikana na kifaa hicho kutasaidia ushahidi kuwa madhubuti na sio rahisi kumwondoa mtu katika hatia.

Pia amewataka wananchi wote hususan vijana kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao badala ya kutumia muda mwingi katika mitandao
  ya kijamii.
 
Safari ya kuelekea kizimbani ikiwa imeiva
 
Zuberi Thabit mtuhumiwa wa ubakaji
 
Idd Adamu mtuhumiwa wa kurekodi video za ubakaji
Share:

Mtoto wa Chacha Wangwe Abadili Msimamo Mahakamani

Mtoto wa aliyekuwa mwanasiasa machachari na Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, amebadili msimamo mahakamani katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii, kuwa Zanzibar inakandamizwa na Tanzania Bara na kwamba ni koloni lake.

Mtoto huyo, Bob Chacha Wangwe (24), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alibadili msimamo jana aliposomewa shtaka hilo kwa mara ya pili, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wangwe alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 11, na alisomewa shtaka linalomkabili na alikiri kutenda kosa hilo.

Mshtakiwa anapokiri kosa, kwa kawaida Mahakama inaweza kumtia hatiani na kumpa adhabu kwa mujibu wa sheria, kulingana na kosa siku hiyo hiyo au siku nyingine yoyote.

Baada ya kusomewa shtaka na kukiri, Hakimu Mkazi Mkuu, Waria lwande Lema, aliamuru mshtakiwa huyo apelekwe rumande hadi jana, Mei 17, kwa kuwa hakimu aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo hakuwapo.

Hata hivyo, jana mshtakiwa huyo alipopandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo, ili kusomewa maelezo ya awali kabla ya Mahakama kumtia hatiani na kumhukumu, tofauti na siku ya kwanza, alikana kutenda kosa hilo.

Kutoka na mshtakiwa huyo kukana kosa, Wakili wa Serikali, Salim Msemo, aliieleza Mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika, hivyo aliiomba ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Wakili wa mshtakiwa huyo Peter Kibatala aliiomba Mahakama impe dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili linadhaminika, maombi ambayo yalikubaliwa na aliachiwa kwa dhamana na kesi iliahirishwa hadi Juni 15.

Wangwe ambaye baba yake kwa sasa ni marehemu, anadaiwa Machi 15, jijini Dar es Salaam, alisambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Share:

Tuesday, May 17, 2016

Bodaboda Wagongana Jijini Mwanza, mmoja afariki

Mwendesha pikipiki ambaye hajafahamika amefariki dunia baada kugongana uso kwa uso na mwenzake, eneo la Mabatini jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema bodaboda mwingine Stanley Maimu (24), alijeruhiwa katika tukio hilo lililotokea Mei 15.

Msangi alisema ajali hiyo ilisababishwa na mwendokasi wa wahusika, hivyo bodaboda wote walishindwa kumudu pikipiki zao na kugongana uso kwa uso.

Katika tukio jingine, Polisi inawashikilia watu wawili; Chacha Mwita (34) na Rashid Mohamed (34) wakazi wa Kata ya Kitangiri wilayani Ilemela kwa kosa la kukutwa na misokoto sita ya bangi kinyume na sheria.

Kamanda msangi alisema Mei 14 saa 14.00 mchana, polisi waliokuwa doria walifanikiwa kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwapo kwa watu hao wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya kuuza dawa za kulevya.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wanapobaini vitendo vya uhalifu.
Share:

Mjane Aliyemwaga Machozi Mbele ya Rais Magufuli Akabidhiwa Nyumba Yake

Hatimaye mjane aliyemwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli akidai kudhulumiwa mali ya urithi, amepewa nyumba na shamba baada ya Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Crispin Meela kusuluhisha mgogoro wa umiliki wa mali hizo.

Hivi karibuni akiwa mjini Babati, Rais Magufuli alimuagiza Meela ahakikishe mjane huyo, Mwanaidi Mussa anapewa mali zake ikiwamo nyumba na shamba zilizokuwa zinadaiwa kuchukuliwa na mke mdogo kinyume cha sheria.

Meela alimkabidhi nyumba na shamba la ekari 2.5 mjane huyo juzi na kuagiza mke mdogo kama hakuridhika na uamuzi, akakate rufaa mahakamani.

Meela pia aliwataka wananchi kuacha kurubuniwa na watu wachache wenye maslahi binafsi na badala yake wafuate maelekezo yanayotolewa na vyombo vya sheria.

“Migogoro ya mirathi imeendelea kukithiri katika maeneo mengi nchini kutokana na watu kutofuata sheria za mirathi na wengine wakitaka kunufaika na mali zinazoachwa na marehemu,” alisema Meela.

Mwanaidi ambaye amezeeka, alidai kwa muda mrefu amewaomba viongozi wa Serikali ya mtaa anaoishi wamsaidie, kutatua tatizo lake lakini walimpuuza.

Mke mdogo, Asia Musa alidai kuwa nyumba hiyo aliyokabidhiwa Mwanaidi, aliijenga na mumewe kauli ambayo ilikinzana na ya mke mkubwa aliyedai kuwa wakati Asia anaoelewa alikuta nyumba ameshaijenga na mumewe.
Share:

Monday, May 16, 2016

Vijana Wanaovaa Suruali Chini ya Kiuno Kuchapwa Viboko 70

Wakazi wa Kata ya Karansi, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wametoa uamuzi kuwa wanawake watakaovaa sketi fupi na vijana watakaovalia suruali chini ya kiuno, wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko 60 hadi 70.

Uamuzi huo umefikiwa na wakazi zaidi ya 200 wakisema uvaaji huo ni kinyume na mila na desturi za Kiafrika.

Vazi lingine lisilotakiwa kwa wanawake ni kuvaa suruali pamoja na vijana kunyoa ndevu mitindo isiyofaa.

Mkutano huo ulioandaliwa na wazee wa kimila jamii ya Meru (Wachili) na Wamasai (Malaigwani), uliwavutia wananchi wengi ambao walihudhuria.

Sambamba na uamuzi huo utakaokuwa unafanyika hadharani, pia adhabu hiyo itawahusu wezi wa mali na wanaopenda kucheza pool table wakati wa kazi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbrod Mutafungwa alipinga uamuzi huo akisema kwa maazimio hayo ya kuwaadhibu watuhumiwa kwa kuwachapa viboko ni kujichukulia sheria mkononi na ni kinyume na sheria.
Share:

Wanaofanya Biashara ya Ngono Wataka ajira Irasimishwe

Baadhi ya wanawake wanaojiuza katika mitaa ya Majengo B na Fisi, mjini Mpanda mkoani Katavi wameitaka Serikali kuandaa utaratibu wa kuwatambua ili nao waweze kulipa kodi na kuliingizia taifa pato kutokana na shughuli wanayofanya ya kuuza miili yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi usiku, baadhi ya wanawake hao walisema wanafanya kazi kama zilivyo kazi nyingine kwani zinawaingizia kipato kizuri kinachowasaidia kutimiza mahitaji yao ya msingi hivyo kazi hiyo inapaswa kuheshimiwa na kutambuliwa na serikali.

Mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Joyce, alisema ni wazi Serikali ikiandaa utaratibu mzuri wa kuwatambua itawafanya waweze kulipa kodi ambayo italiongezea pato taifa tofauti na ilivyo sasa ambapo wamekuwa hawalipi kodi kwa kuwa hawatambuliwi.

" Sisi kazi yetu ina kipato kizuri kutokana na makubaliano yanayofanyika kati na wateja wetu lakini Serikali haitaki kututambua hivyo sio rahisi hata kututaka tulipe kodi, nchi nyingine watu kama sisi tumetambuliwa na tunalipa kodi serikalini" alisema Rosemary Kazeze.

Aliongeza kwamba kipindi hiki ambacho Serikali inatafakari au haioni umuhimu wa wao kutolipa kodi, anawashauri kina dada poa wenzake kuacha tabia ya kukwepa kwenda Nyumba za kulala wageni zinazotambuliwa na Serikali kwani kufanya  hivyo kunaikosesha serikali mapato

Alisema kuwa siku za nyuma walikuwa wanafanya biashara hiyo katika madanguro kitendo ambacho polisi walikuwa wakiwasumbua kwa kuwakamata kutokana na misako ya mara kwa mara, lakini hivi sasa hawasumbuliwi kwani wamepanga vyumba katika gesti halali na wanalipia vyumba hivyo na mmiliki analipa kodi kwa msingi huo nao wanachangia pato la taifa.

“ Kaka yangu mwandishi tunashukuru sana hata wewe kutufikia, wanatudharau na kutunyanyasa sisi lakini wateja wetu wakubwa ni hao hao viongozi wa serikali na taasisi nyingine lakini wajue kufanya biashara ya ukahaba sio sababu ya kuto muunga mkono Rais wetu katika suala la mapato ya serikali”…alisema Mayasa Hussein
Share:

Saturday, May 14, 2016

Ahukumiwa Kifungo cha Miaka 30 Jela Kwa Kumuoa Binti Yake wa Kumzaa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, jana ilimhukumu kifungo cha miaka 30, Godfrey Mjelwa (48), baada ya kupatikana na hatia ya kuishi kinyumba na binti yake wa kumzaa.

Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo, Mwajuma Lukindo alisema ushahidi wa pande zote ulithibitisha kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo la kuishi chumba kimoja na binti yake, kama mke na mume.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, Mjelwa aliamua binti yake mwenye umri wa miaka 15 (jina limehifadhiwa) kuwa mke na kuishi naye katika Mtaa wa Kizota Manispaa ya Dodoma. 
Hakimu Lukindo alisema kosa alilokutwa nalo mtuhumiwa ni ‘maharimu’ (kufanya mapenzi na ndugu za damu), licha ya kuwa mtoto huyo bado alikuwa mdogo, lakini ni mtoto wake wa kumzaa.

Mwendesha mashtaka Janeth Mgome, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa, ili liwe fundisho kwa wengine ambao wana tabia ya aina hiyo. 
Utetezi wa mtuhumiwa huyo uliwavunja mbavu watu waliokuwapo mahakamani hapo, kwani alitaka kupunguziwa adhabu kwa kuwa mtoto wake ana miaka 14 na miezi tisa na siku tisa, siyo miaka 15 kama ilivyodaiwa mahakamani hapo.
Share:

Friday, May 13, 2016

Mbuzi wa Tambiko Aua Watu Watano wa Familia Moja

VILIO, simanzi na hofu vimetanda kwa wakazi wa Kitongoji cha Lotii, Kijiji cha Mwitikira, Tarafa ya Olboloti, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara baada ya watu watano wa familia moja kufariki dunia kwa namna ya kutatanisha.
 
Watu hao wanadaiwa kufikwa na mauti baada ya kula nyama ya mbuzi iliyotolewa kutekeleza mila ya kutatua mgogoro uliojitokeza katika familia mbili zilizopo Kijiji cha Kaachini kilichopo wilayani humo.

Akisimulia tukio hilo la aina yake kijijini hapo, mmoja wa majirani wa familia hiyo, Juma Kijaji, aliliambia  MTANZANIA kwa simu jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya familia ya Kilangazi Mbao na majirani zao (majina tunayo).

Kijaji alisema kuwa awali familia hizo zilikubaliana kulipana mbuzi baada ya kutofautiana katika masuala kadhaa kulingana na mila na desturi za jamii yao.

Alisema baada ya siku sita, walikubaliana mbuzi huyo achinjwe na nyama hiyo igawanywe kwa majirani wengine katika kitongoji hicho.

“Hata hivyo siku chache baadaye kulizuka uvumi kijijini hapa kwamba nyama hiyo haikupaswa kuliwa na familia ya Mzee Mbao, jambo ambalo lilifuatiwa na vifo vya mfululizo kutoka familia hiyo,” alisema.

MWENYEKITI WA KITONGOJI

Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Ally Msambo, aliieleza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto kuwa kabla ya vifo hivyo, wanafamilia hao walivimba mwili mzima.

Msambo aliwataja wana familia waliotangulia kufariki dunia kuwa ni watoto wawili, Juha Mbao (3) na Mwajuma Mbao (5).
Alisema siku moja baadaye babu yao, Chirangas Mbao naye alipatwa na ugonjwa huo huo wa ajabu na kufariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.

Katika mfululizo huo wa vifo, mtoto mwingine, Agnes Mbao naye alipoteza maisha na kufuatiwa na baba yake Chilangas Chilangas aliyefia katika kitongoji hicho baada ya kutoroka hospitalini na kukamilisha idadi hiyo ya watu watano wa familia moja kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

Mwenyekiti huyo wa kijiji aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya wanakijiji kushtushwa na vifo hivyo, walikubaliana kutozika miili ya mtoto na baba yake hadi kwanza wapate ufumbuzi wa kiini cha vifo hivyo.

MKUU WA WILAYA

Akisimulia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, alisema hali hiyo imesababisha wananchi kuingiza imani za kishirikina kwa kudai kuwa kuna kitu kimefanywa ili kiweze kuwadhuru wanafamilia hao.

Alisema tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji hicho.
Nzoka ambaye alikiri kuwapo kikao hicho cha upatanishi, alisema mama mmoja ambaye mumewe na watoto wake walifariki katika tukio hilo, alienda kukopa mbuzi kwa jirani yake ambaye ni Mmasai.

Baada ya kupata mbuzi huyo, alitakiwa amchinje ili wananchi waliojitokeza kwenye kikao kilichokuwa kinafanyika kijijini hapo wale ile nyama.

“Baada ya kula nyama hiyo, mtoto wa mama huyo alifariki, siku iliyofuata alifariki mtoto mwingine na siku ya tatu alifariki baba mdogo wa watoto hao,” alisema Nzoka.

Alisema wananchi walichukua maiti hizo na kwenda kuzika, lakini baadaye alifariki mtoto mwingine wa familia hiyo.
“Siku iliyofuata (juzi) alifariki baba mzazi wa watoto hao, hali iliyosababisha kujitokeza kwa hofu kwa wananchi wa kijiji hicho na kudai kuwa mbuzi huyo amefanyiwa mambo ya kishirikina ili watu wa familia hiyo waweze kufariki.

“Nilikwenda jana (juzi) mimi na timu yangu ya madaktari kutoka wilayani kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo,” alisema Nzoka.

Alisema baada ya kuzifungua maiti, zilikuwa zimevimba sana hivyo madaktari walizifanyia upasuaji kwa kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Mmoja wa madaktari ambaye alihusika kufanyia uchunguzi maiti ya watoto wawili waliofia hospitalini, alisema mapafu yalikutwa yameharibika.

VIFO VINGINE FAMILIA MOJA

Kutoka mkoani Mara, watoto wanne wakiwamo watatu wa familia moja wamekufa maji katika matukio mawili tofauti yaliyotokea ndani ya wiki moja Manispaa ya Musoma na wilayani Butiama.

Watoto watatu wa familia moja walikufa maji katika Kijiji cha Mirwa wilayani Butiama baada ya kunasa kwenye tope wakiwa wanaogolea kwenye mto Mei 9, mwaka huu, saa 8 mchana.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Leonard Chacha, aliliambia MTANZANIA kuwa watoto hao waliokuwa wakiishi na mama yao, Mtabutwa Cherehani, waliondoka nyumbani kwa lengo la kwenda kuoga mtoni.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Wambura Kizengo (11) mwanafunzi wa darasa la tano, Dismas Kizengo (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza, wote katika Shule ya Msingi Mirwa na Mkirya Kizengo (4) mwanafunzi wa chekechea.

Chacha alisema baada ya kupata taarifa za watoto kupotelea mtoni, ilipigwa ngoma kwa ajili ya kuwakusanya wananchi kwa lengo la kwenda kuwakoa, lakini walipofika mtoni walikuta tayari wamefariki dunia.

Diwani wa Kata ya Mirwa, Pitalis Odero, alisema wamesikitishwa na vifo vya watoto hao.
Katika tukio jingine lililotokea Manispaa ya Musoma, mvua iliyoambata na upepo mkali iliyonyesha juzi jioni, imesababisha kifo cha mwanafunzi Benaderta Aley (12) aliyekuwa anasoma darasa la pili Shule ya Msingi Kamnyonge.

Kaka wa mwanafunzi huyo, Delta Aley, alisema mdogo wake akiwa na wenzake walikwenda kusaga mashineni, wakati wanarudi mdogo wake alianguka kwenye mtaro uliokuwa unapitisha maji kwa kasi na kusombwa.

Alisema mwili wa marehemu ulipatikana baada ya siku mbili ukiwa umbali wa kilomita mbili.
Share:

Thursday, May 12, 2016

Mtoto wa marehemu, Chacha Wangwe afikishwa kortini kwa makosa ya kimtandao


BOB Chacha Wangwe (24), mtoto wa mwanasiasa marehemu Chacha Wangwe, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii.

Akisoma kesi hiyo namba 167, Paul Kagoshi mbele ya Waliarandwe Rema, Hakimu Mkazi katika mahakama hiyo alisema kuwa, Bob Chacha Wangwe amefikishwa mahakamani hapo kwa kutenda kosa la kuchapisha taarifa za kupotosha katika ukurasa wake Facebook.

Mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo  tarehe 15 Machi na kwamba alichapicha maneno haya; “Tanzania ni ambayo….inajaza chuki wananchi … matokeo ya kubaka Demokrasia Zanzibar ni hatari zaidi ya muungano wenyewe…. Haiwezekani nchi ya Zanzibar kuwa koloni la Tanzania bara kwa sababu za kijinga.”
Share:

Monday, May 9, 2016

Atupwa Jela Miaka 33 kwa Wizi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Chato mkoani Geita, imemhukumu kifungo cha miaka 33 jela Matiku Wambura (34) baada ya kupatikana na hatia ya makosa manne ya wizi likiwamo la kuiba vyombo vya muziki mali ya Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Chato mission.

Wambura ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kitela kata ya Chato wilayani hapa aliiba kinanda na vinasa sauti vyote vikiwa na thamani ya Sh3.94 milioni.
Hakimu Jovith Kato amesema leo kuwa mahakama inamtia hatiani baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa.
Amesema atahukumia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kwanza, kosa la pili na tatu ni miaka mitano kila moja, huku la nne atalitumika kwa miaka mitatu.
Share:

Monday, May 2, 2016

Video: Godfrey Magila Aeleza Jinsi Ilivyo Rahisi Kukamatwa kwa Mtu Yeyote Anayefanya Makosa ya Kimtandao

Godfrey Magila ni mtaalamu wa Teknolojia kwenye upande wa mitandao na ndio aliyetengeneza App ya Tigo Back-Up, amekaa kwenye Interview na Millard Ayo na kueleza urahisi wa kukamatwa kwa yeyote anaefanya kosa la kimtandao ikiwa tayari sheria ya makosa ya kimtandao imeshaanza kufanya kazi Tanzania.

Tayari watu kadhaa wameshafikishwa Mahakamani Tanzania akiwemo aliyemtukana Rais Magufuli, aliyeandika habari za uongo za mkuu wa majeshi kulishwa sumu.…Wengi wanaamini sio rahisi kukamatwa hata ukitumia jina ambalo sio lako kwenye mtandao ila Magila anasema ni rahisi sana.
 Anasema 
Kila mtu aliyejiunga kwenye mtandao kuna kama unaacha alama ya unyayo kwahiyo hilo watu wanalichukulia kirahisi lakini lina umuhimu wake na ndio linafanya ijulikane muda, sehemu na taarifa nyingine kuhusu wewe pale unapotafutwa, unyayo unaonyesha mpaka aina ya simu

Kubadilisha jina na kumtukana mtu kwenye mtandao itasaidia usikamatwe? 

Kuna baadhi ya vitu hata ukibadilisha jina haisaidii mfano mitandao mingi ukijiunga au email unaambiwa uingize namba ya simu kwa ajili ya uthibitisho, utatumiwa msg kwenye simu ili uthibitishe…. tayari namba yako uliyoiweka ina taarifa zako nyingi na hiyo ni moja tu ya njia nyingi zinazoweza kufanya ukamatwe’
Share:

Wednesday, April 27, 2016

Hali ya Kituo cha Mabasi ya Kusini Mbagala si Shwari

 Hali ya kituo kikuu cha Mabasi yaendayo mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara si nzuri jambo ambalo limekuwa kero kwa abiria pamoja na watoa huduma hiyo ya usafiri.

Kituo hicho kilichopo Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam kimesheheni madibwi ya maji hivyo wadau mbalimbali wameiomba Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kutupia jicho kituo hicho na kukifanyia ukarabati wa kumwaga kifusi kuondoa kero hiyo.
Share:

Thursday, October 1, 2015

Magufuli Afunika Dodoma.....Aahidi Kumaliza Mapigano Ya Wakulima Na Wafugaji


Mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM Dkt. John Pombe Magufuli (pichani) akihutubia umati wa watu kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma jana.
Akitoa hotuba yake katika mji wa Kibaigwa Dk. John Pombe Magufuli alisema hakuna kitu kinachomuumiza kama mauaji ya wakulima na wafugaji yanayotokea kati ya wilaya za Kongwa Mkoani Dodoma na Kiteto mkoani Manyara.
Dkt Magufuli aliahidi kuwa mara baada ya kuchaguliwa na kuunda Serikali yake, jambo hilo atalipa uzito wa juu na kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa. 
“Yaani mimi Magufuli nimteuwe Waziri na watendaji wengine wa serikali halafu mauaji yatokee watu wafe, Mkuu wa mkoa yupo, Mkuu wa wilaya yupo na Kamanda wa Polisi yupo wabaki wanapunga upepo... wamiliki wa ng’ombe wabaki wanakula maisha... haiwezekani! Nitalala nao mbele na ng’ombe wataliwa msibani kwa uzembe waliousababisha” alisema Magufuli kwa msisitizo mkubwa.

Magufuli amewataka wafugaji na wakulima kuishi kwa amani bila kubaguana, lakini pia akasema atatumia sheria za ardhi na kuhakikisha maeneo ya wafugaji na wakulima yanatengwa, ili wafanye shughuli zao na kukuza kipato na uchumi wao bila kusumbuliwa.
Baadhi ya wananchi wa mji wa Dodoma na vitongoji vyake wakimsiiliza Dkt Magufuli alipokuwa akinadi sera zake za kuomba kura ili kushika nafasi ya Urais ya awamu ya tano.
Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, akimnadi Dkt.Magufuli kwa kuhubiri amani katika mikitano yake ya kampeni kuliko wagombea wa vyama vingine hawasisitizi kudumisha amani nchini jambo ambalo ni tunu ya taiafa
Dkt. Magufuli akimnadi mgombea Ubunge wa Dodoma Mjini,mara baada ya kumkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Ndugu Anthony Mavunde wakati wa mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Jamhuri mjni Dodoma leo.
Dk Magufuli akimnadi Mgombea ubunge Jimbo la Mpwapwa, George Lubeleje,mjini MPwapwa katika uwanja wa mgambo.
Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli akimnadi Mgombea ubunge Jimbo la Kongwa, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati wa mkutano wa kampeni jimboni humo.
Mawaziri wakuu wa zamani, John Samuel Malecela na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba wakifuatilia mkutano wa kampeni wa Dkt Magufuli alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Dodoma kwenye mkutano wa kampeni.
Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, akimsimamia Mgombea ubunge Jimbo la Mtera kupitia CCM, Livingstone Lusinde aliyekuwa akifanya mazoezi ya Push Up wakati wa mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa akimuombea kura Dk Magufuli wakati wa mkutano huo wa kampeni mjini Dodoma  jana jioni .
Walemavu nao wana haki ya kuwasikiliza wagombea nafasi mbalimbali ikiwemo ya Urais,Ubunge na Udiwani
Wananchi wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakimsikiliza Mgombea Urais wa CCM,Dkt. Magufuli alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa kampeni mjini Kongwa.
Mgombea Urais Dkt John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Waziri Mkuu wa zamani Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba,mjini Kibaigwa wilayani Kongwa kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni.
Wananchi wa Kibaigwa wilayani Kongwa wakifuatilia hotuba za Dkt Magufuli kwenye mkutano wa kampeni.
Dk Magufuli akijipigia kampeni kwa wakazi wa Kibaigwa , wilayani Kongwa jana. Dkt. Magufuli akiwapungia mikono wananchi alipowasili kwenye kampeni Uwanja wa Jamhuri Dodoma jana.
Share:

Wednesday, September 30, 2015

Polisi Wasambaratisha utafiti wa Nani Mkali kati ya LOWASSA na MAGUFULI Uliokuwa Ukifanywa Mitaani



Wakati tafiti za kienyeji zenye lengo la kupima kukubalika kwa wagombea urais, hasa Dk John Magufuli na Edward Lowassa zikizidi kuongezeka, polisi jijini Arusha mwishoni mwa wiki walitumia nguvu kutawanya vijana waliokuwa wakiendesha kura za maoni kwenye stendi ndogo ya mabasi na soko kuu.

Tangu kutangazwa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi za Twaweza na Ipsos, vijana kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko, hasa sokoni na kwenye baa wamekuwa wakiendesha tafiti zao za kienyeji wakiwa na lengo la kuonyesha hali halisi ilivyo mitaani tofauti na matokeo ya tafiti hizo mbili.

Katika tafiti hizo za Ipsos na Twaweza, Dk Magufuli, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa mbele ya Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chadema na vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini matokeo hayo yamepingwa vikali na wadau mbalimbali, huku yakiamsha tafiti za kienyeji mitaani.

Katika tukio lililotokea mjini Arusha, vijana walikuwa wakiendesha utafiti wao kwenye soko kuu la Arusha na eneo la kituo kidogo cha mabasi, lakini polisi walifika na kuwatimua wakidai wanavunja sheria. 
 
Wafanyabiashara hao wa soko hilo na stendi ndogo, waliandaa maboksi mawili ya kura, moja likiwa limeandikwa “Magufuli” na jingine “Lowassa”. Baadaye walialika watu kwenda kupiga kura.

Kila aliyepita katika eneo hilo alielezwa utaratibu wa kupiga kura na alitumbukiza karatasi yake katika boksi lililoandikwa jina la mgombea anayeona anafaa kuwa rais.

Utafiti wa stendi ndogo ulikamilika baada ya muda na ulionyesha matokeo ya wagombea hao (tunayo).

Wakati watu waliokuwa stendi ndogo wakiendelea kushangilia matokeo hayo, wafanyabiashara wenzao wa soko kuu walikuwa wakiendelea kupiga kura na ghafla polisi walifika maeneo hayo na kuwatimua vijana waliokuwa wakikusanya kura.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema waliokuwa wanafanya utafiti huo walikiuka sheria na kwamba kitendo chao kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kulikuwa na watu wasioafikiana.

Aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kufanya mambo ambayo hayana manufaa, badala yake wasubiri siku ya kupiga kura.

“Huo ni utafiti wa aina gani wa maboksi?” alihoji alipoulizwa kuhusu tukio hilo.

“Hizi ni vurugu za mitaani. Tunawaomba wananchi watulie, wasubiri siku ya uchaguzi wapige kura kwa amani.”

Hili ni tukio la pili la utafiti unaofanywa kienyeji mitaani baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam kuendesha utafiti wao kwa kuruhusu watu kumpigia kura mgombea wanayempenda kati ya Magufuli na Lowassa.

Mbali na utafiti huo wa wakazi wa Dar es Salaam, kwenye maeneo mengine nchini kumekuwapo na watu wanaoendesha tafiti kama hizo zenye lengo la kujua ni mgombea gani wa urais anakubalika zaidi.
Share:

Thursday, May 28, 2015

Update: Yule msichana aliyeua mtoto wa miaka 9 afikishwa mahakamani....Apigwa ngumi mbele ya polisi huko morogoro

Msichana Judith Chomile(15) amefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro akikabiliwa na tuhuma za kumnyonga hadi kufa mtoto mwenye umri wa miaka 9 mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Bernard Benderi ya mjini Morogoro.
Akisoma shitaka mbele ya hakimu mkazi Ivan Msaki, mwendesha mashataka wa polisi Aminata Mazengo amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo may 20 kinyume na kifungu namba 196 cha kanuni ya adhabu nahakutakiwa kujibu lolote kutokana na kosa lenyewe na kuwa mtuhumiwa yuko chini ya miaka 18 hivyo kuwakilishwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 10 mwaka huu itakapo tajwa tena mahakamani hapo .
Katika hali isiyo ya kawaida ndugu wa marehemu Edga Mafwere kwa hasira amempiga ngumi mtuhumiwa muda mfupi baada ya kutoka mahakamani mbele ya maafisa wa jeshi la polisi na ustawi wa jamii ambapo naye alijikuta katika mikono ya jeshi la polisi na kufungwa pingu ambapo anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Akizungumza juu ya uhakika wa usalama wa msichana Judith Chomile ,afisa ustawi wa jamii manispaa ya Morogoro Jasmin Masenge amesema msichana huyo atakuwa katika mikono salama chini ya uangalizi wa kitengo cha ustawi wa jamii pamoja na jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto hadi kesi inayomkabili itakapotolewa hukumu.
Share:

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger