JAMII imeshauriwa kutowafungia ndani watoto wenye vichwa vikubwa, badala yake wa wawapeleke hospitali ili kupatiwa matibabu.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wa Watoto Wenye Vichwa Vikubwa (ASBAHT), Abdulhakim Bayakub, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kujadili changamoto zinazowakabili watoto hao.
Alisema watoto wenye vichwa vikubwa kama watapatiwa matibabu mapema wanaweza kuondokana na ulemavu usiokuwa wa lazima.
“Wapo baadhi ya wazazi bado wanawafungia ndani watoto wao kwa madai ya kuwa ni walemavu kutokana na vichwa vikubwa walivyonavyo, lakini huu si ulemavu, tumewashuhudia watoto wengi waliofanyiwa upasuaji wa vichwa vikubwa wamepona na kurudi katika hali yao ya kawaida,” alisema Bayakub.
Alisema wapo baadhi ya watoto wanawahishwa hospitali lakini wazazi wanapotakiwa kuwarejesha tena kwa ajili ya uchunguzi huwa hawawarudishi, hali inayosababisha ongezeko kubwa la vifo vya watoto wenye vichwa vikubwa.
“Asilimia 60 ya watoto wanaofanyiwa upasuaji hawajarudishwa tena hospitali, inakadiriwa wamefariki dunia, kwani hakuna taarifa yoyote inayothibitisha kama wapo hai,” alisema Bayakub.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa ni kutokuwa na uwezo, kwani kati ya watoto 600 mtoto mmoja ndio hutibiwa kwa matibabu binafsi, waliobaki wote huendelea kusota kusubiri msamaha wa matibabu.
Kwa upande wake, Daktari wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Rebeca Majige, alisema ipo haja ya kutoa elimu kwa wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa ili kupunguza ongezeko la vifo vya watoto hao.
Alisema kati ya asilimia 45 hadi 48 ya watoto waliopo wodini hukutwa na matatizo yote mawili, wakiruhusiwa kutoka hushindwa kurudi hospitali kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya afya zao na kusababisha ongezeko la kubwa la watoto hao kupata maradhi ya maambukizi.
Aidha aliitaka Serikali kuongeza bajeti katika Wizara ya Afya ili kuweza kuwasaidia kimatibabu watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
0 comments:
Post a Comment