ZAIDI ya watoto 80 wako katika hatari ya kutofanyiwa upasuaji wa moyo
kutokana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kukabiliwa na uhaba
mkubwa wa damu katika benki yake.
Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCT), Prof. Mohammed Janab, katika hafla ya
kutambulisha madaktari kutoka Marekani waliokuja kwa ajili ya upasuaji
huo.
Prof. Janab alisema mtoto mmoja hutumia chupa sita hadi nane za damu
wakati wa upasuaji, hivyo kwa idadi ya watoto 80 inahitajika zaidi ya
chupa 600 ili kuokoa maisha yao.
Kwa mujibu wa Prof. Janab, kwa sasa akiba ya damu iliyopo katika Benki ya Damu ni chupa 250 tu na upo upungufu wa chupa 350.
“Tunakabiliwa na uhaba mkubwa wa damu katika benki yetu ya damu, kwa
kipindi cha wiki moja tumeanza kuwafanyia watoto wenye matatizo ya moyo
upasuaji, lakini damu haitoshelezi ni vyema Watanzania wakajitokeza
kuchangia damu,” alisema Prof. Janab.
Alisema upasuaji wa moyo unahitaji kuwapo damu nyingi na kuwaomba
Watanzania kujitokeza kuchangia ili kuokoa maisha ya watoto hao.
Prof. Janab alisema kufanyika kwa upasuaji huo nchini kumeokoa fedha
nyingi kwani watoto hao wangesafirishwa nje ya nchi zingetumika zaidi ya
Sh milioni 10 hadi 60 kwa kila mtoto ili kukamilisha upasuaji wake.
“Watoto hawa watafanyiwa upasuaji kupitia msaada wa Taasisi ya
Muntada Aid kutoka Marekani, hivyo ni vyema kuwachangia damu ili kuwapa
moyo wahisani hao,” alisema.
Prof. Janab alisema kuanzia Januari mwaka huu hadi Machi, taasisi
hiyo kwa kushirikiana na jopo la wataalamu kutoka nchi mbalimbali,
wameweza kuwafanyia upasuaji wa moyo wagonjwa 90 na hali zao zinaendelea
vizuri.
Alisema kwa kipindi cha Aprili mosi hadi kufikia jana, tayari
wamewafanyia upasuaji wagonjwa 45 wakiwamo watoto wadogo na watu wazima.
Naye Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Matt Sutheland, alisema hii ni
mara ya pili kwa nchi yake kuisaidia Taasisi ya Jakaya Kikwete kwa lengo
la kuokoa maisha ya watoto walio na ugonjwa wa moyo.
Balozi Sutheland alisema ni wajibu wa kila mtu kuwasaidia watoto
wenye matatizo ya moyo ili waweze kuishi na kusogeza ndoto zao kwani
mtoto ndiyo jicho la pili katika nchi.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya
Jakaya, Dk. Tulizo Sanga, alisema ni vyema wajawazito kuhakikisha
wanapata chanjo kamili katika kipindi chote cha ujauzito.
Dk. Sanga alisema wajawazito kutozingatia taratibu za chanjo pamoja
na kumeza dawa ovyo bila ushauri wa daktari wakati wa ujauzito,
husababisha kujifungua watoto wenye ugonjwa wa moyo.
Utafiti uliofanywa duniani mwaka 2012 hadi 2015 umeonyesha kuwa zaidi
ya wagonjwa 400 hadi 600 wanaosafirishwa nje ya nchi kutoka katika nchi
za Afrika, asilimia 50 wamekumbwa na tatizo la ugonjwa wa moyo.
0 comments:
Post a Comment