Showing posts with label kitaifa. Show all posts
Showing posts with label kitaifa. Show all posts

Friday, May 20, 2016

Serikali Yajibu Hoja za Kivuko cha MV Dar es Salaam na Uuzwaji wa Nyumba Zake

Serikali imejibu hoja za upinzani kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali na kutetea ununuzi wa kivuko cha MV Dar es Salaam ambacho kilitakiwa kufanya safari zake kati ya Dar na Bagamoyo.

Hoja hizo ziliibuliwa katika hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, James Mbatia akitaka kutekelezwa kwa azimio la Bunge la urejeshwaji wa nyumba hizo serikalini lililotolewa Aprili 2008.

Pia, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilibainisha upungufu katika kivuko cha MV Dar es Salaam ambao ni kutolipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kutokuwa na kasi kadri ya mkataba na kutokuwapo hati ya makabidhiano.

Hoja hizo za upinzani zilijibiwa juzi jioni na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alisema hakuna taratibu zozote zilizokiukwa wakati wa ununuzi wa kivuko hicho ambacho kwa zaidi ya mwaka hakijaanza kazi.

Alisema wizara ilipata taarifa ya CAG ambayo ilibainisha upungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na kivuko hicho kununuliwa kwa Dola za Marekani 4.9 milioni (Sh7.9 bilioni) bila kulipiwa VAT, lakini akasisitiza kwamba hakukuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu za ununuzi.

“Ni kweli kivuko kina mapungufu ikiwamo kasi ndogo, lakini hakuna ukiukwaji wowote wa taratibu wakati wa ununuzi. Temesa ilitangaza zabuni na baada ya maombi kupitiwa, kampuni ya MS Jones Gram Hansen ilishinda zabuni hiyo kwa kuwa na bei nafuu,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema baada ya kivuko kuletwa nchini Desemba 2014, kilifanyiwa majaribio na kubainika kwamba hakikuwa na kasi ya kuridhisha. Alisema makubaliano yalikuwa ni kujenga kivuko chenye kasi ya nots20, lakini hicho kilikuwa na kasi ya nots 15.7.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilimtaka mkandarasi kurekebisha kasoro hiyo kwa gharama zake na kuwa ameshawasilisha andiko juu ya namna atakavyoifanya kazi hiyo.

“Mpaka sasa mzabuni huyo hajalipwa asilimia 10 ya malipo yaliyokubaliwa mpaka pale atakapokamilisha kazi hiyo. Kwa hiyo, taratibu zote zilifanyika kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kuhusu nyumba, Profesa Mbarawa alisema Serikali iliidhinisha mpango huo Aprili 24, 2008 baada ya kupata ridhaa ya Bunge ilipopeleka suala hilo kujadiliwa.

“Suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali, pia taratibu zilifuatwa. Serikali ilileta mpango huo bungeni na kupata ridhaa ya wabunge wote. Kwa hiyo, niwaambie tu wabunge kwamba suala hili lilipata baraka zao,” alisema waziri huyo.

Uuzwaji wa nyumba za Serikali na ununuzi wa kivuko cha Mv Dar es Salaam vilifanyika wakati Rais John Magufuli akiwa waziri wa ujenzi kwa nyakati tofauti.

Kambi ya upinzani imekuwa ikisisitiza kwamba kuna ukiukwaji wa sheria uliofanyika wakati wa uuzaji wa nyumba na ununuzi wa kivuko hicho. Hata hivyo, Serikali imeshikilia msimamo wake kwamba sheria zilifuatwa.
Share:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aapa Kukomesha Lumbesa

WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa, ametoa onyo kwa wafanyabiashara wanaodhulumu wakulima kwa kununua mazao kwa kuyafunga kwenye magunia bila kuzingatia vipimo sahihi maarufu kama lumbesa, na kutaka viongozi kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mikoa kusimamia.

Alisema serikali itapambana na wafanyabiashara wanaoendelea kulazimisha kufungasha mazao katika magunia bila kuzingatia vipimo sahihi hivyo kuwapunja na kuikosesha serikali mapato.

Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Saumu Sakala (CUF) katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Majaliwa alikiri kuwa serikali ilishazuia matumizi ya kipimo cha lumbesa na kuahidi kwamba awamu hii, itakomesha dhuluma hiyo.

Awali mbunge huyo alitaka kauli ya serikali dhidi ya vitendo hivyo kuendelea ingawa kupitia viongozi mbalimbali wa serikali, vilishapigwa marufuku.

Waziri Mkuu alitoa mwito tena kwa wakuu wa wilaya, halmashauri zao, maofisa biashara katika halmashauri hizo kuhakikisha unyonyaji huo unakomeshwa.

“Jambo hili wala siwaachii wakuu wa wilaya peke yao bali nawaagiza hata wakuu wa mikoa kupitia kamati zao za ulinzi na usalama kuhakikisha agizo hili linatekelezwa, swali hili la mbunge linaashiria mambo haya bado yanafanyika,” alisema.

Pia aliwaagiza watendaji wa vijiji na kata, kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanaouza mazao kwenye maeneo yao, hawauzi mazao kwa kipimo cha lumbesa.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema tayari maelekezo yametolewa kwa Wakala wa Vipimo, kuhakikisha biashara yote ya mazao ya kilimo nchini yanauzwa kwa vipimo vya kilogramu na siyo kwa kufungashwa lumbesa.

Alisema ingawa kuna vijiji visivyokuwa na mizani, hali hiyo siyo kigezo cha kuhalalisha lumbesa, badala yake alisema magunia yote nchini yametengenezwa kwa vipimo hivyo mazao yanapojazwa gunia lazima lifungashwe kwa kushonwa kwa uzi au kamba.
Share:

Rais Magufuli Atoa Salamu za Pole kwa Wakazi wa Jiji la Mwanza Kufuatia Mauaji ya Watu Watatu Msikitini

Rais John Magufuli ametoa salamu za pole kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza, kutokana na mauaji ya watu watatu, waliouawa kwa kukatwa mapanga wakiwa msikitini.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli amesema yupo pamoja na wakazi wa mkoa huo wa Mwanza katika kipindi hiki cha majonzi, kuomboleza watu hao na pia alisema anawaombea wale waliojeruhiwa wapone.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Ndani imesema imesikitishwa na mauaji ya watu hao watatu, waliouawa msikitini katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.

Kauli hiyo ya Serikali, ilitolewa bungeni mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Yussuf Masauni.

Masauni alisema kuwa Serikali inawapa pole wakazi wa Mwanza, viongozi wa mkoa na wilaya ya Nyamagana na mbunge wa jimbo hilo, Stanslaus Mabula.
Share:

Thursday, May 19, 2016

Majaliwa: Rais Magufuli hakukosea kuzuia sukari kuingia nchini kiholela

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema kauli ya Rais John Pombe magufuli ya kuzuia kuingizwa kwa sukari kiholela nchini ilikuwa ni katika kulinda viwanda vya ndani.

Aidha Majaliwa amesema kuingia kwa sukari Tani 70,000 toka nje ya nchi hakutaathiri uzalishaji wa viwanda unaotarajiwa kuanza mapema mwezi julai.

Akijibu swali la kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni na mbunge wa jimbo la Hai, Freeman Mbowe, Majaliwa amesema uhaba wa sukari ni tani 100,000 na uwezo wa viwanda kuzalisha ni tani 320,000 huku mahitaji ya sukari kwa mwaka mzima ni tani 420,000.

Amesema katika kukabiliana na uhaba uliopo Serikali kupitia bodi ya sukari imeagiza sukari nje ya nchi na tayari Serikali imeshaanza kupanga mikakati ya kudumu ya kumaliza tatizo la sukari kwa miaka ijayo.

Akiuliza swali la nyongeza Mbowe alimtaka waziri mkuu kuwahakikishia watanzania kuhusu bei elekezi na kutaka kujua ni lini uraismu wa uanzishwaji wa shamba/kiwanda eneo la bagamoyo utakavyo malizwa.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema swala la kuanzisha shamba katika eneo la bagamoyo lina mchakato mrefu na halina urasimu wowote.

Amesema shamba hilo limepakana na mbuga ya saadani na kwamba linategemea sana maji ya mto Wami, lakini pia wanyama nao wanategemea maji ya mto huo.

Hivyo amesema serikali na wadau wanaendelea kuangalia suala hilo kwa umakini ili kutoa maamuzi yatakayo leta tija kwa taifa.

Kuhusu bei elekezi ya sukari amesema tayari bodi ya sukari imeshaanza kusimamiasuala hilo, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote watakaopandisha sukari kiholela
Share:

Sakata la Lugumi: CHADEMA Yajipanga Kumng'oa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema uzito wa Rais John Magufuli kumwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kutokana na kutajwa kuhusika na Kampuni ya Lugumi inayodaiwa kulitapeli Jeshi la Polisi, utasababisha waanze harakati za kumng’oa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais John Magufuli hana budi kuchukua hatua haraka kumwajibisha Waziri Kitwanga kama alivyofanya kwa watumishi wengine wa umma katika operesheni ya kutumbua majipu.

Waziri Kitwanga anadaiwa kuwa na hisa kwenye Kampuni ya Infosys Ips Tanzania Limited ambayo ilipewa zabuni ya kutoa huduma za kitaalamu na Kampuni ya Kimarekani ya Biometrica kuhusu uwekaji wa mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi. 
Mkataba wa kuweka mashine hizo uliingiwa kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises ambayo ililipwa Sh34 bilioni kati ya Sh37 bilioni za mkataba, wakati kazi ya kufunga mashine hizo ilifanyika kwenye vituo 14 tu hadi wakati Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipofanya ukaguzi.

Hata hivyo, kampuni hiyo inadai kuwa Kitwanga, ambaye ni mmoja wa waasisi wa Infosys, alijiondoa kwenye uendeshaji tangu mwaka 2010, wakati mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011.

Chadema bado inaona kuwa Rais Magufuli anatakiwa kumwajibisha waziri huyo wa Mambo ya Ndani.

“Kama Rais akishindwa kuchukua hatua katika hili, Serikali itang’oka madarakani. Sisi Chadema tutaiondoa. Haiwezekani wakati Lugumi inachunguzwa mhusika mkuu (Kitwanga) aendelee kuwa waziri, tena wa wizara inayohusika na mkataba wa Lugumi,” alisema Mwalimu.

Mwalimu alisema, Rais anapaswa kujitokeza hadharani na kueleza uhusiano wake na Kitwanga na awaeleze Watanzania kuwa kutokana na uswahiba wao ndiyo sababu ya kutomchukulia hatua.

“Mbona anawatumbua marafiki wa wenzake? Kwa nini marafiki zake anashindwa kuwatumbua? Ukiwa kiongozi mwenye kubagua katika uamuzi ni hatari kwa uchumi wa Taifa, ni sawa na baba anayewabagua watoto wake matokeo yake ni kuzalisha chuki tu.”

Licha ya Mwalimu kutotaka kuweka wazi mpango huo, kwa mujibu wa Ibara ya 53 A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
 Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inapaswa kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.

Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 372, kati yao wabunge wa upinzani ni 118.

“Hilo tutalifanya iwapo tu Rais atashindwa kumwajibisha Kitwanga. Ila huyu waziri naye anapaswa ajipime mwenyewe ili kumlinda bosi wake (Waziri Mkuu). Afanye kama Edward (Lowassa-waziri mkuu mstaafu) aliamua kujiuzulu wadhifa wake ili kumlinda Jakaya (Kikwete-Rais wa Awamu ya Nne) kwa kosa ambalo yeye hakulifanya,” alidai Mwalimu.

Mwalimu alidai kwamba Serikali imezuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kuhofia uchafu wa viongozi, likiwamo sakata la Lugumi.

“Ndiyo maana tunasema CCM ni ileile maana wametumbua majipu, sasa imebaki mitoki. Ni kama imewashinda maana ipo sehemu mbaya,” alisema.

Licha ya mkakati huo wa Chadema, Aprili 19 mwaka huu, Kitwanga alisema kuwa hahusiki katika sakata hilo na juzi alijibu hoja ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) lililomtaka ajiuzulu, akisema hawezi kuwajibu watoto ili kuonyesha tofauti yake na wao.

Katika maelezo yake, Mwalimu aliorodhesha utumbuaji ambao Rais Magufuli ameufanya tangu aingie madarakani, ukiwamo wa watendaji waliofanya vurugu tu katika vikao kwa kusisitiza kuwa ni ajabu kuona mpaka sasa hajamchukulia hatua yoyote Kitwanga wakati ukweli uko wazi kuwa anahusika na sakata la Lugumi. 
Baada ya ripoti ya CAG kuibua udhaifu huo kwenye mkataba, Kamati ya Hesabu za Serikali ya Bunge iliunda kamati ndogo kufuatilia tuhuma hizo baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuhusu mkataba huo.

Kampuni ya Infosys ni wakala wa kampuni maarufu duniani ya kutengeneza kompyuta ya Dell, ikijihusisha na usambazaji wa vifaa hivyo, matengeneza na utoaji huduma za kitaalamu.

Kaimu katibu mkuu huyo wa Chadema alisema, chama hicho pia kinajipanga kuanza ziara yake nchi nzima na ajenda kuu itakuwa kuanika mambo yote mabaya yanayofanywa na Serikali.
Share:

Edward Lowassa na Fredrick Sumaye Watajwa Katika Sakata la Uuzwaji wa Nyumba za Serikali.......Mbowe Atoa Ufafanuzi

Uuzwaji wa nyumba za serikali umegeuka mwiba huku wabunge wakiendelea kuhoji hatua zilizochukuliwa kutokana na kadhia hiyo

Hatua hiyo iliyotekelezwa mwaka 2002  hadi 2004 ilizusha malalamiko mengi tangu wakati huo na sasa imeibuka tena bungeni

Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano jana, mbunge wa Nachingwea, Hassani Masala (CCM) alihoji mfumo uliotumika kuuza nyumba za serikali

Alisema haungi mkono kwa vile umesababisha viongozi wapya wa serikali wanaoteuliwa kujikuta wakiishi katika nyumba za wageni.

Mjadala huo uliibuliwa juzi na msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni kupitia kwa waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema kabla ya Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan Zungu kumtaka kuondoa baadhi ya maneno katika hotuba yake likiweo suala la uuzwaji wa nyumba za serikali.

Ritha Kabati Amvaa Lowassa

Akichangia mjadala huo jana, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati alimtaja aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa kuwa alinunua nyumba ya serikali iliyouzwa mwaka 2002 yenye jengo namba 68.

Alisema hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilisema nyumba za serikali 7,921 ziliuzwa tangu mwaka 2002 hadi 2004 na kutaka serikali ya awamu ya tano kurejesha nyumba hizo kutokana na walionunua kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.

“Naomba niwaambie usiangalie boriti lililo katika jicho la mwenzako wakati kwako lipo, kwani hata mgombea wao wa urais Edward Lowassa alihusika kwa kununua nyumba ya plot namba 68 na Fredrick Sumaye alikuwa Waziri Mkuu na kuhusika kuuza nyumba hizo,” alisema Kabati.

Baada ya kueleza hayo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliomba kumpa taarifa mbunge huyo kuwa taarifa hiyo ni kwa maslahi ya taifa, hata kama mhusika atakuwa katokea kambi ya upinzani sheria itachukua hatua.

"Kambi ya upinzani tunapoibua jambo huwa linakuwa kwa maslahi ya Taifa, hivyo ni vyema wabunge wote mtambue kuwa kosa likifanywa na kiongozi  ni lazima hatua zichukuliwe bila kujali ni wa Chadema, CUF au CCM.

"Tunapokuwa tunatoa uamuzi kama kambi ina maana sheria ifuate mkondo wake." Alisema Mbowe huku akishangiliwa na wabunge wa UKAWA

Awali katika michango mbalimbali ya wabunge wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kuuzwa nyumba hizo za serikali na kudai kuwa watumishi wapya wengi walioajiriwa, wamekuwa wakikosa maeneo ya kuishi.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) akichangia mjadala huo alilalamikia kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na nyingine za Tazara zipatazo 500 na kuamua kumpatia Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ripoti aliyodai inaonesha nyumba hizo zilivyouzwa.
Share:

Magari Ya Washawasha Kugeuzwa ya Zimamoto

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusufu Hamad Masauni, amesema Serikali iko katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kubadili matumizi magari ya polisi ya kuzuia ghasia kwa kurusha maji ya kuwasha maarufu washawasha yaweze kutumika kuzima moto.

Kauli hiyo ilitokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga aliyeuliza ni kwanini Serikali inanunua magari ya washawasha yasiyo na tija ambayo hutumika nyakati za uchaguzi tu badala ya kununua magari ya zimamoto.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Masauni alisema magari ya washawasha bado yana tija kwani Serikali inafanya taratibu ili magari hayo yatumike kuzima moto kwenye majanga na isiwe kwa washawasha pekee na kuwataka wabunge hasa wa upinzani kuondoa fikra za kuyapinga magari ya washawasha kwani sasa itakuwa ni neema kwao badala ya kutumika kwa kudhibiti vurugu pekee. 

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana Serikali ilinunua magari ya washawasha 777 kwa bei ya kati ya Sh150 milioni na Sh400 milioni, hata hivyo taarifa zingine zilisema magari yaliyotumika wakati wa uchaguzi ni 50.

Awali Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), aliuliza swali la msingi kwamba ni lini Serikali itapeleka huduma ya zimamoto katika mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea.

Naibu Waziri Masauni alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika halmashauri ya Mji wa Tunduma lina kituo katika eneo la mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe, kinachohudumia wilaya yote ukiwamo mpaka huo.

Alisema kwa sasa kituo hicho kina gari moja ambalo nalo liko kwenye matengenezo mjini Mbeya likiendelea kufanya matengenezo huku askari wakiendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na majanga ya moto.

Masauni alisema ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya zimamoto katika maeneo ya nchi ikiwamo Tunduma, mpango huo unategemea upatikanaji wa fedha kwa Serikali.

Kuhusu ujenzi wa kituo cha Polisi cha Mbozi, alimuomba mbunge wa eneo husika avute subira ili waweze kuona namna bora ya kufanya kwani bajeti ya Serikali ni ndogo na vituo vinavyotakiwa kujengwa ni vingi.
Share:

Wednesday, May 18, 2016

Mwanasheria Mkuu wa Serikali awataka Mawakili wa Serikali kutoa ushauri wa Mikataba kwa makini

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wa Serikali kuwa makini na kutoa ushauri kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu pindi wanapotoa ushauri wa kisheria kuhusu mikataba mbalimbali.

Mhe. Masaju ameitoa kauli hiyo alipokuwa akiongea  na Mawakili  wa Serikali wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanayohusu uhakiki wa mikataba ya ununuzi wa umma leo Mjini Dodoma.

Alisema ni vyema wakatekeleza jukumu hilo kwa makini kwani ushauri unaotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia mawakili hao ndio msimamo wa Serikali.

“Ninapenda kuwakumbusha kwamba ninyi ni watumishi wa umma na mnaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2003” alisema Mhe. Masaju na kuongeza kuwa:

“Kama walivyo watumishi wengine wa umma na kwa msingi huu, ninyi ni sehemu ya Serikali na nafasi yenu katika Serikali ni kubwa”.

Pia aliwataka wanasheria wa Serikali kujengewa uwezo kuhusu uhakiki wa mikataba na iwapo watashindwa kutekeleza wajibu huo ipasavyo watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.

Alisema kuwa kutokana na kuongezeka kwa thamani ya mikataba inayohakikiwa na wanasheria wa taasisi  ya manunuzi ni wazi kwamba kuna umuhimu wa Maafisa Sheria kupatiwa mafunzo hayo.
 
“Wanasheria wa Serikali wanaohakiki mikataba hii wanawajibika kuzingatia sheria zinazohusiana na mikataba husika pamoja na maadili ya Wanasheria wa Serikali katika Utumishi wa Umma kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 27 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 2005”,alisema Mhe. Masaju.
 
Mhe. Masaju alishauri utaratibu wa mikataba yote kuhakikiwa Dar es Salaam ubadilike kwani unasababisha ongezeko la gharama kwa taasisi za Serikali na kuchelewesha miradi.

Alifafanua kuwa Divisheni ya Mikataba iko Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee hivyo, mikataba yote ya mikoani ni lazima ipelekwe Dar es Salaam kwa ajili ya kuhakikiwa.

“Hii inasababisha wadau hasa wa kwenye Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa, Jiji na wengine walioko mikoani kusafiri na kupeleka mikataba Dar es Salaam kwa ajili ya uhakiki” alisema Mhe. Masaju.

Hivyo alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali wa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko Mikoani ili hatimaye baadhi ya Mikataba kutoka kwa wadau walioko wilayani na mikoani iwe inapelekwa katika Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali zilizoko mikoani.
Share:

Polisi Akamatwa na Noti Bandia Zenye Thamani ya Sh. 870,000

ASKARI Polisi Ezekiel Dinoso (32) mkazi wa tarafa ya Mgeta, wilayani Mvomero mkoani Morogoro amekutwa na noti bandia za Sh 10,000 zenye thamani ya Sh 870,000, akijiandaa kuzitumbukiza katika akaunti ya mtandao wa Tigo Pesa katika duka mojawapo eneo la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana kuwa tukio hilo ni la Mei 14, mwaka huu saa 1:00 usiku katika eneo la Mawezi , Manispaa ya Morogoro.

Mtuhumiwa alikutwa katika duka la Hadija Hamis (35) mkazi wa Chamwino, wakati alipohitaji kuwekewa fedha hizo, mwenye duka alimtilia shaka hivyo kuarifu Polisi. 

Mtuhumiwa alipokamatwa na askari baada ya kutolewa taarifa Kituo cha Polisi, alikutwa akiwa na noti bandia 87 za Sh 10,000.

Alitaja namba za noti hizo ni BX 7287490 zikiwa noti 22 , BX 728792 zikiwa noti 20, BX 728791 noti 19 na BX7287487 zikiwa noti 15 na kufanya jumla ya thamani ya Sh 870,000 ambazo ni bandia.

Kamanda Matei alisema mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na baada ya uchunguzi kukamilika atafikishwa mahakamani.

Katika tukio jingine, Rashidi Shabani (30) na Michael Lukasa (39), wote wakazi wa Ngerengere wanashikiliwa na Polisi kwa kuwakuta na nyama ya nyati kilo 300 na silaha aina ya gobole iliyotumika kumuulia mnyama huyo.

Kamanda wa Polisi wa Morogoro, Matei, alisema walikamatwa Mei 14, mwaka huu saa 2:00 usiku katika kijiji cha Kinonko, kata ya Gwata, wilaya ya Morogoro. 

Matei alisema, kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na jitihada zinazofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi katika kukomesha vitendo vya uhalifu.
Share:

Tuesday, May 17, 2016

Katibu Mkuu Chadema Ziarani Ghana

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Vincent Mashinji ameanza ziara ya kikazi ya siku tano nchini Ghana ambako pamoja na shughuli nyingine, atashiriki mkutano wa kimkakati kuhusu masuala ya uchaguzi.

Katika ziara hiyo, Mashinji anatarajiwa kukutana na mgombea urais wa chama rafiki na Chadema, New Patriotic Party (NPP), Nana Akufo Addo kwa ajili ya kushauriana, kubadilishana uzoefu wa kisiasa na kupeana mikakati ya ushindi katika uchaguzi.

Dk Vincent Mashinji pia atakutana na Dk Klaus Schuler ambaye ni meneja wa kampeni wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel. Dk Schuler pia ni Meneja Mkuu wa chama tawala Ujerumani cha CDU.

Katika ziara hiyo, Dk Mashinji ameambatana na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita alikuwa meneja wa kampeni wa mgombea urais wa Chadema aliyewakilisha Ukawa, Edward Lowassa.

 Mbali ya Tanzania, nchi nyingine 15 zinazotarajiwa kushiriki mkutano huo ni pamoja na Kenya, Uganda, Zimbabwe, DRC, Angola, Namibia, Nigeria, Senegal, Ivory Coast, Togo, Burkina Faso, Benin, Afrika Kusini, Ghana na Ujerumani.
Share:

Serikali Kuajiri Askari Wapya 3700....... Askari 7000 na Wakaguzi 1300 Watapandishwa Vyeo

Serikali  inatarajia kumwaga ajira kwa askari  katika mwaka ujao wa fedha.Taarifa juu ya ajira hizo, zilitolewa jana bungeni  na  waziri  mwenye dhamana.

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato ya Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2016/17 kuhusu ajira za askari, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alisema wataajiriwa askari wapya 3,700 katika mwaka wa fedha 2016/17.

Waziri Kitwanga alisema mbali ya kuajiri askari hao, pia watawapandisha vyeo askari 7,140, wakaguzi 1,325 na maofisa 991.

Alisema katika mwaka 2015/16, jumla ya askari polisi wapya 3,882 waliajiriwa, na askari wakaguzi na maofisa 4,065 wa vyeo mbalimbali walipandishwa vyeo kwa kufuata utaratibu wa ajira.

“Aidha, serikali imeendelea kuhuisha viwango vya mishahara na posho mbalimbali, ikiwemo posho ya chakula ambayo iliongezwa kutoka Sh 180,000 hadi kufikia Sh 300,000 kwa mwezi,” alieleza Waziri Kitwanga.

Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Jeshi la Polisi litaongeza umakini katika kusimamia nidhamu kwa askari wake kwa kufanya uchambuzi wa kina (vetting) kwa kuchukua vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wanaoomba kujiunga na Jeshi la Polisi ili kuwa na askari wenye nidhamu na moyo wa dhati wa kulitumikia Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wa Jeshi la Magereza, alisema linatarajia kutoa mafunzo kwa maofisa na askari 4,975 katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na yale ya Taaluma ya Urekebishaji.

Alisema ili kukabiliana na changamoto ya uchache wa miundombinu ya makazi kwa askari Polisi, serikali kupitia mkopo kutoka Serikali ya China inakusudia kujenga nyumba 4,136 chini ya usimamizi wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi.

Akizungumzia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, alisema jeshi hilo linahitaji vituo 152 Tanzania Bara, lakini kwa sasa lina vituo 57 na kati ya hivyo, 38 vipo katika miji na 19 katika viwanja vya ndege. 

Alisema huo ni upungufu wa vituo 95 hali inayosababisha maeneo mengi kukosa huduma za zimamoto na uokoaji.

Inategemea kujenga kituo kimoja cha zimamoto na uokoaji katika eneo la Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam na kuendelea na ujenzi wa Jengo la Makao Makuu Tazara - Mchicha, Dar es Salaam.

Aidha, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kupambana na makosa yanayovuka mipaka hususani ugaidi, uharamia, biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya kusafirisha binadamu, wizi wa vyombo vya moto hususani magari, wizi wa kutumia mitandao ya Tehama, bidhaa bandia, na biashara haramu ya silaha na uchafuzi wa mazingira.
Share:

Makamu wa Rais Atema Cheche.....Wakuu wa Mikoa na Wilaya Watakaopuuza Agizo Lake Watatumbuliwa

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wakuu wa mikoa ya Geita, Arusha na Kagera kuhakikisha wanaondoa mifugo itokayo nje ya nchi pamoja na kuwaondoa wanachi waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa (Tanapa) ifikapo Juni 30 mwaka huu.

Aidha ameagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya mifugo inayotolewa ndani ya hifadhi na kupunguza mgogoro kwa wananchi wengine.

Samia alitoa maagizo hayo jana jijini Arusha, wakati alipokuwa akikabidhi hundi ya thamani ya Sh bilioni moja kwa wakuu wa mikoa 19 inayozunguka hifadhi za taifa (Tanapa) kwa ajili ya kununua madawati. 

Alisema, wakuu wa mikoa wakizembea kutekeleza uondoaji mifugo ndani ya hifadhi za taifa serikali itawawajibisha.

Alisema waliohifadhi mifugo ndani ya hifadhi hiyo waondoke na mifugo yao hadi Juni 30 mwaka huu kwani mkoa wa Kagera una ng’ombe milioni mbili wanaotoka nje ya nchi, na mikoa ya Arusha na Geita ina ng’ombe milioni tatu kutoka nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu kukabidhi madawati 16,500 katika wilaya zote 55 zilizopo kwenye mikoa 19 nchini, Samia aliipongeza Tanapa kwa kusaidia elimu nchini kwani baada ya serikali ilipotangaza kuwa elimu bure wanafunzi wengi wamejitokeza huku kukiwa na changamoto ya madawati

Samia alisema, kutokana na msaada huo wanafunzi wataondokana na adha ya kukaa chini na kuumia migongo kwani kila wilaya itapata madawati 300 huku wanafunzi 49,500 wakiwa wanakaa kwenye madawati na kuongeza usikivu zaidi.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema Tanapa wanatambua mchango wa elimu ndio maana wametoa msaada huo kwa mikoa 19 inayopakana na hifadhi za taifa.

Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi alisema Tanapa itaendelea kushirikiana na serikali katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa bidii pamoja na kujua jinsi ya kuhifadhi maliasili za Taifa.

Akitoa salamu za shukrani kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki aliishukuru Tanapa kwa kutoa madawati kwa wakuu wa mikoa na kusema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umepiga marufuku usafirishaji wanyama pori kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuanzia jana.
Share:

Jeshi La Polisi Lanasa Mahausigeli 15 Waliokuwa Wakipelekwa Oman

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata wasichana 15 katika nyumba iliyopo maeneo ya Ukonga, waliokuwa tayari kusafirishwa kwenda Oman kufanya kazi za ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Simon Sirro, alisema wasichana hao walikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa toka kwa msiri kuwa kuna mtu amewaweka wasichana kwa ajili ya kuwasafirisha.

Sirro alisema Polisi walifuatilia na kufika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakuta katika nyumba ya Hadija Mohamed (40) wakiwa wamegawanywa katika vyumba viwili.

Alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa mwanamke huyo anashirikiana na mwenzake Salma Habibu (43) mkazi wa Temeke kuwatafutia masoko nchini Oman na wao ni mawakala wanaoletewa kutoka mikoani na kuwapokea kwa ajili ya kuwasafirisha.

Aidha alisema watuhumiwa hao watapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Pia ametoa onyo kwa watu wenye tabia hiyo kuacha, kwani wasichana hao wakifikishwa nje ya nchi hufanyiwa vitendo vya kikatili na unyanyasaji.

Katika tukio jingine, Polisi kanda hiyo imewakamata vijana 75, ikiwa ni muendelezo wa msako wa vijana wanaofanya matukio ya wizi wa majumbani nyakati za usiku.
Share:

Serikali: Hatuna Msamaha na Wauza Madawa ya Kulevya

Serikali  imesema haitakuwa na msamaha wala suluhu kwa wahusika wote wa biashara haramu ya dawa za kulevya. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alitoa rai kwa watu wote kutojihusisha na uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa hizo.

Kitwanga aliyasema hayo jana bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Alisema, tatizo la biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya limeendelea kuwepo nchini na katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016, kilogramu 141.7 za dawa za kulevya za viwandani ambazo ni heroin, cocaine, cannabis resin, morphine na mandrax zilikamatwa na watuhumiwa 719 (wanaume 644 na wanawake 75) walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Aidha, kilo 18,513 na gramu 415 za bangi na kilo 15,402 za mirungi zilikamatwa ambapo watuhumiwa wanaume 9,935 na wanawake 1,020 walikamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Alisema, katika mwaka 2016/17 Jeshi la Polisi litaendeleza mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.

Akizungumzia vita dhidi ya biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu, alisema wizara ilianzisha Sekretarieti ya Kupambana na Kudhibiti Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu kwa lengo la kudhibiti biashara hiyo.

Kitwanga alisema hilo lilifanyika baada ya ripoti mbalimbali za kitaifa na kimataifa kuitaja Tanzania kama chanzo, njia ya kupitishia na kituo cha mwisho kwa biashara haramu ya kusafirisha binadamu.

Alisema katika mwaka 2015/16 sekretarieti hiyo ilizuia hati na nyaraka za kusafiria za wasichana 31 wa Tanzania kwa lengo la kufanya uchunguzi kubaini mtandao wa wasafirishaji haramu wa binadamu. 

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 Sekretarieti imejipanga kufanya ufuatiliaji na uchunguzi wa wazi juu ya biashara hiyo.
Share:

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger