Polisi mkoani Mara inamshikilia mganga wa zahanati katika Kijiji cha
Rwamchanga wilayani Serengeti kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito
aliyejifungua pacha na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Mei 15.
“Tunamshikilia
kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi na kushindwa
kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, tunaendelea na mahojiano
yatakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Ng’anzi.
Akisimulia
chanzo cha mwanae kupoteza maisha, Shida Mugesi akiwa katika Hospitali
ya Nyerere alisema alifika zahanati saa 12 asubuhi na kumuomba mganga
amuhudumie, lakini alikataa.
“Nilikaa kwa muda wa saa mbili bila
kupatiwa huduma, ghafla nilihisi uchungu wa kusukuma mtoto tukamuita
mganga wa zamu ili anisaidie aligoma na kudai nimsubiri anakwenda kuoga
na wakati huo alikuwa anazungumza kwa simu bila kuonyesha ushirikiano.
Nilianza kujifungua mwenyewe,” alisema.
Muuguzi ambaye hakutaka
jina lake litajwe alisema walipopima uzito wa watoto kwa mjamzito huyo
walibaini kuwa aliyefariki alikuwa na kilo 2.5 na mwingine 2.3.
Muuguzi
wa zahanati hiyo, Frida Kasonga alisema aliposikia taarifa ya kuwapo
kwa mgonjwa huyo alilazimika kurudi kituoni kumsaidia lakini alikuta
mtoto mmoja ameshafariki dunia.
“Haikuwa zamu yangu ila nililazimika kurudi baada ya kusikia mganga aliyekuwa zamu kagoma kuwasaidia,” alisema Frida.
Ofisa
mtendaji kata, Fadhila Nyamburapi na Mwenyekiti wa kitogoji cha Kazi,
Samwel Nyakande walilaani kitendo hicho na kutaka sheria ichukue mkondo
wake.
0 comments:
Post a Comment