Mkeka umegeuka shubiri kwa kampuni ya michezo ya bahati nasibu na
kubashiri matokeo ya michezo, Super Bets ya jijini Dar es Salaam baada
ya kushindwa kuwalipa wateja wake waliodai kushinda kiasi kikubwa cha
fedha.
Mmoja kati ya wateja hao anadaiwa kushinda shilingi milioni 164
Jumatatu hii. Msimamizi wa Super Bets aliyejitambulisha kwa jina la
Amani, aliongea na kipindi cha Sports Extra cha Clouds FM kuwa watu hao
walishinda kimakosa. Amedai kuwa moja ya vyanzo vinavyowapatia matokeo
ambayo kwenye mkeka zinaitwa odds ilikuja ndivyo sivyo.
“Baada ya hapo timu yetu ya masoko ilipogundua kuna tatizo hilo
limetokea ina maana wakaja wakalifanyia kazi wakatujulisha tukagundua
kuwa kuna tatizo fulani lilitokea tukalifanyia marekebisho. Baadhi ya
wateja walikuja hapa wakasema wameshinda kutokana na zile odds za 98,
tukawaambia wasubiri kwamba tunalishughulikia kwamba kuna matatizo ya
kimtandao yalitokea. Tutawalipa kutokana na correct odds ambazo
zilitolewa katika mtandao baada ya kurekebishwa hilo tatizo,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya michezo ya kubahatisha
nchini, Abbas Tarimba amedai kuwa wateja hao wamewasilisha malalamiko
yao na wanayafanyia kazi.
Amedai kuwa maafisa wa bodi hiyo walienda kwenye ofisi za Super Bets
kufanya uchunguzi kwenye server zao ili kubaini ukweli na wamewaomba
walalamika siku mbili kukamilisha uchunguzi huo.
Miaka ya hivi karibuni betting kwenye michezo imekuwa biashara kubwa
huku kukiwepo na makampuni mengi yanayochezesha na kuwavutia watu wengi
hasa vijana.