VILIO, simanzi na hofu vimetanda kwa wakazi wa Kitongoji cha Lotii,
Kijiji cha Mwitikira, Tarafa ya Olboloti, Wilaya ya Kiteto mkoani
Manyara baada ya watu watano wa familia moja kufariki dunia kwa namna ya
kutatanisha.
Watu hao wanadaiwa kufikwa na mauti baada ya kula nyama ya mbuzi
iliyotolewa kutekeleza mila ya kutatua mgogoro uliojitokeza katika
familia mbili zilizopo Kijiji cha Kaachini kilichopo wilayani humo.
Akisimulia tukio hilo la aina yake kijijini hapo, mmoja wa majirani
wa familia hiyo, Juma Kijaji, aliliambia MTANZANIA kwa simu jana kuwa
chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya familia ya Kilangazi Mbao na
majirani zao (majina tunayo).
Kijaji alisema kuwa awali familia hizo zilikubaliana kulipana mbuzi
baada ya kutofautiana katika masuala kadhaa kulingana na mila na desturi
za jamii yao.
Alisema baada ya siku sita, walikubaliana mbuzi huyo achinjwe na
nyama hiyo igawanywe kwa majirani wengine katika kitongoji hicho.
“Hata hivyo siku chache baadaye kulizuka uvumi kijijini hapa kwamba
nyama hiyo haikupaswa kuliwa na familia ya Mzee Mbao, jambo ambalo
lilifuatiwa na vifo vya mfululizo kutoka familia hiyo,” alisema.
MWENYEKITI WA KITONGOJI
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Ally Msambo, aliieleza Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto kuwa kabla ya vifo hivyo,
wanafamilia hao walivimba mwili mzima.
Msambo aliwataja wana familia waliotangulia kufariki dunia kuwa ni watoto wawili, Juha Mbao (3) na Mwajuma Mbao (5).
Alisema siku moja baadaye babu yao, Chirangas Mbao naye alipatwa na
ugonjwa huo huo wa ajabu na kufariki dunia akiwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kiteto.
Katika mfululizo huo wa vifo, mtoto mwingine, Agnes Mbao naye
alipoteza maisha na kufuatiwa na baba yake Chilangas Chilangas aliyefia
katika kitongoji hicho baada ya kutoroka hospitalini na kukamilisha
idadi hiyo ya watu watano wa familia moja kupoteza maisha katika
mazingira ya kutatanisha.
Mwenyekiti huyo wa kijiji aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya
wanakijiji kushtushwa na vifo hivyo, walikubaliana kutozika miili ya
mtoto na baba yake hadi kwanza wapate ufumbuzi wa kiini cha vifo hivyo.
MKUU WA WILAYA
Akisimulia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, alisema
hali hiyo imesababisha wananchi kuingiza imani za kishirikina kwa kudai
kuwa kuna kitu kimefanywa ili kiweze kuwadhuru wanafamilia hao.
Alisema tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji hicho.
Nzoka ambaye alikiri kuwapo kikao hicho cha upatanishi, alisema mama
mmoja ambaye mumewe na watoto wake walifariki katika tukio hilo, alienda
kukopa mbuzi kwa jirani yake ambaye ni Mmasai.
Baada ya kupata mbuzi huyo, alitakiwa amchinje ili wananchi
waliojitokeza kwenye kikao kilichokuwa kinafanyika kijijini hapo wale
ile nyama.
“Baada ya kula nyama hiyo, mtoto wa mama huyo alifariki, siku
iliyofuata alifariki mtoto mwingine na siku ya tatu alifariki baba mdogo
wa watoto hao,” alisema Nzoka.
Alisema wananchi walichukua maiti hizo na kwenda kuzika, lakini baadaye alifariki mtoto mwingine wa familia hiyo.
“Siku iliyofuata (juzi) alifariki baba mzazi wa watoto hao, hali
iliyosababisha kujitokeza kwa hofu kwa wananchi wa kijiji hicho na kudai
kuwa mbuzi huyo amefanyiwa mambo ya kishirikina ili watu wa familia
hiyo waweze kufariki.
“Nilikwenda jana (juzi) mimi na timu yangu ya madaktari kutoka
wilayani kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao na kuchukua
hatua stahiki kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo,” alisema Nzoka.
Alisema baada ya kuzifungua maiti, zilikuwa zimevimba sana hivyo
madaktari walizifanyia upasuaji kwa kuchukua sampuli kwa ajili ya
uchunguzi zaidi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa madaktari ambaye alihusika kufanyia uchunguzi maiti ya
watoto wawili waliofia hospitalini, alisema mapafu yalikutwa
yameharibika.
VIFO VINGINE FAMILIA MOJA
Kutoka mkoani Mara, watoto wanne wakiwamo watatu wa familia moja
wamekufa maji katika matukio mawili tofauti yaliyotokea ndani ya wiki
moja Manispaa ya Musoma na wilayani Butiama.
Watoto watatu wa familia moja walikufa maji katika Kijiji cha Mirwa
wilayani Butiama baada ya kunasa kwenye tope wakiwa wanaogolea kwenye
mto Mei 9, mwaka huu, saa 8 mchana.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Leonard Chacha, aliliambia MTANZANIA
kuwa watoto hao waliokuwa wakiishi na mama yao, Mtabutwa Cherehani,
waliondoka nyumbani kwa lengo la kwenda kuoga mtoni.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Wambura Kizengo (11) mwanafunzi wa
darasa la tano, Dismas Kizengo (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza, wote
katika Shule ya Msingi Mirwa na Mkirya Kizengo (4) mwanafunzi wa
chekechea.
Chacha alisema baada ya kupata taarifa za watoto kupotelea mtoni,
ilipigwa ngoma kwa ajili ya kuwakusanya wananchi kwa lengo la kwenda
kuwakoa, lakini walipofika mtoni walikuta tayari wamefariki dunia.
Diwani wa Kata ya Mirwa, Pitalis Odero, alisema wamesikitishwa na vifo vya watoto hao.
Katika tukio jingine lililotokea Manispaa ya Musoma, mvua iliyoambata
na upepo mkali iliyonyesha juzi jioni, imesababisha kifo cha mwanafunzi
Benaderta Aley (12) aliyekuwa anasoma darasa la pili Shule ya Msingi
Kamnyonge.
Kaka wa mwanafunzi huyo, Delta Aley, alisema mdogo wake akiwa na
wenzake walikwenda kusaga mashineni, wakati wanarudi mdogo wake
alianguka kwenye mtaro uliokuwa unapitisha maji kwa kasi na kusombwa.
Alisema mwili wa marehemu ulipatikana baada ya siku mbili ukiwa umbali wa kilomita mbili.
0 comments:
Post a Comment