Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga, akiongea na waandishi wa
habari katika uzinduzi wa stika za upimaji uzito katika
mizani kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Sekta ya Ujenzi), Eng.Joseph Nyamhanga ametambulisha utaratibu mpya
utakaotumika kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha ili kurahisisha
biashara na usafirishaji kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya
nchi.
Utaratibu
huo unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu utawezesha magari yanayosafiri
nje ya nchi kukagulia katika vituo visivyozidi vinne ili kupunguza muda
wa safari kwa magari yaendayo nje ya nchi na kuvutia wasafirishaji
kutumia bandari ya Dar es Salaam.
“Tumetayarisha
stika zitakazobandikwa kwenye magari yanayokwenda nje ya nchi ambayo
yatasimama na kukaguliwa katika vituo vitatu kwa magari yanayotumia
barabara ya kanda ya kati na vinne kwa yanayotumia kanda ya Dar es
salaam yaani TANZAM ”amesema Eng. Nyamhanga.
Eng. Joseph Nyamhanga akitoa ufafanuzi kuhusu stika
za upimaji uzito katika mizani kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda
nje ya nchi.
Eng.
Nyamhanga amevitaja vituo hivyo vya barabara ya ukanda wa kati kuwa ni
Vigwaza mkoani Pwani, Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera
na kwa ukanda wa Dar es salaam yaani barabara kuu ya TANZAM- Dar es
salaam hadi Tunduma na Uyole hadi Kasumulu vitatumika vituo vine ambavyo
ni Vigwaza mkoani Pwani,Mikumi mkoani Morogoro, Makambako mkoani Njombe
na Mpemba mkoani Songwe.
Vituo
hivyo vya ukaguzi wa pamoja vitakuwa na huduma ya Mizani, Vituo vya
Polisi, Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), na maeneo ya kupumzikia
madereva wanaosafiri kwenda nje ya nchi.
Katika
hatua nyingine Eng. Nyamhanga amesema ili kurahisisha biashara ya
usafirishaji kati ya Tanzania na Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC), na Jumuiya ya Soko
la Pamoja kwa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) Serikali
inaendelea kutoa huduma za pamoja mipakani one stop border post
inayolenga kurahisisha huduma za forodha,uhamiaji na usimamizi wa ubora
wa bidhaa na huduma ,ulinzi na usalama kwa kutoa huduma hizo upande
mmoja wa mpaka kwa nchi mbili husika.
Vituo
hivyo vinavyojengwa katika mipaka ya Holili, Namanga, Horohoro,Sirari,
Mtukula, Rusumo, Kabanga, Tunduma na Kasumulu vitaimarisha huduma za
forodha,uhamiaji ulinzi na usalama.
0 comments:
Post a Comment