WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa,
ameitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuwa na utaratibu wa kupima
utendaji wa watumishi wake ili kubaini watendaji wavivu waondolewe
kazini.
Waziri Mbarawa alitoa kauli hiyo juzi, alipotembelea ofisi za TMA
zilizopo jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam kwa lengo la kufahamiana
na kupeana mikakati ya kazi.
Aliwataka watendaji kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano, ambayo imedhamiria kuondoa kero za wananchi.
Prof. Mbarawa alisema ili kufanikisha malengo ya TMA ya kuchochea
maendeleo katika jamii kwa kutoa taarifa za hali ya hewa za uhakika,
lazima wafanyakazi wawe na uadilifu, uwazi na ubunifu.
Alisema wafanyakazi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa ukaribu na
kuthaminiana kuanzia ngazi ya juu hadi chini ili kupeana taarifa kwa
urahisi.
“Kuanzia mwaka huu, tutapeana mikataba ya kazi, mimi nitaingia
mkataba na mkurugenzi wa bodi kwa kupeana mikakati ya kazi na baada ya
muda nitakuja kuikagua, kama atakuwa hajaitekeleza, basi mlango
alioingilia ndiyo atakaotokea.
“Mkurugenzi mkuu ataingia mkataba na Katibu Mkuu wa Wizara na yeye
ataingia mkataba na wakurugenzi wake ambao nao wataingia mkataba na
watendaji wao ili atakayeshindwa kwenda na kasi hii aondoke kwa kutumia
mlango alioingilia,” alisema Prof. Mbarawa.
Aliwataka kutumia fursa za utunzaji wa takwimu kwa kutumia kituo kipya cha kutunzia takwimu kilichopo Mwananyamala.
Alisema wanatakiwa kuacha kuandika madokezo kwa kutumia karatasi
kutokana na kuwa wanaiingizia Serikali gharama ambazo hazina sababu za
msingi na badala yake wanatakiwa kwenda na wakati kwa kutumia mitandao.
0 comments:
Post a Comment