WATU watatu wamehukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatiya ya kumuua mwanamke mmoja, Tabu Makanya mkazi wa Kijiji cha Kwibara Kata ya Mugango Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joachim Demola wa Mahakama Kuu ya Kanda ya Mwanza.
Waliohukumiwa kunyongwa ni Ndaro Sumuni, Aberd Kazimili na Fidelisi Ngewa wote wakazi wa Kijiji cha Kwibara Kata ya Mugango Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Awali watuhumiwa wa kesi hiyo ya mauaji hayo walikuwa watano na mmoja wao alikuwa ni Diwani wa Kata Mugango Wandwi Maguru (CCM) ambaye aliachiwa na Mkurugenzi wa Mashitaka.
Mtuhumiwa mwingine aliachiwa baada ya kubainika kuwa alikuwa na matatizo ya akili.
Katika kesi hiyo ilikuwa na wanasheria wapatao saba kati yao wanasheria watatu wakiwa wanawatetea washitakiwa hao.
Kabla ya hukumu hiyo, Jaji alisema watuhumiwa katika kesi hiyo walienda nyumbani kwa Diwani wa Kata hiyo, Wandwi Maguru ambaye walikubaliana kumuuzia kichwa cha mwanamke kwa Sh milioni 1.5.
Alisema makubaliano hayo ilikuwa kwamba baada ya kupelekewa kichwa hicho diwani huyo angekifanyia mazindiko ya uvuvi wa samaki.
0 comments:
Post a Comment