Showing posts with label BUNGE. Show all posts
Showing posts with label BUNGE. Show all posts

Friday, May 20, 2016

Sakata la Escrow na IPTL Laibuka Upya Bungeni

Kambi ya upinzani imeliibua upya  bungeni sakata la Escrow, Richmond na umiliki wa kampuni ya IPTL, huku ikihoji sababu za Rais John Magufuli kutoheshimu maazimio ya Bunge ya kumwajibisha Sospeter Muhongo, badala yake kumteua tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Hoja hizo ziliibuliwa na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika wakati akiwasilisha maoni ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/16 na makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17.

Muhongo alikuwa akiiongoza wizara hiyo wakati kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo umeme kusubiri kumalizika kwa mzozo wa kimkataba baina ya kampuni ya IPTL, inayozalisha umeme  na Shirika la Umeme (Tanesco).

Bunge lilimuona Profesa Muhongo kuwa alishindwa kuwajibika na kusababisha Serikali kupoteza mapato.

Profesa Muhongo alilazimika kujiuzulu wadhifa huo saa chache kabla ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutangaza baraza jipya.

Hata hivyo, Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lilimsafisha na kashfa hiyo iliyohusisha malipo yaliyofanywa kwa mawaziri, majaji, wabunge na watumishi waandamizi wa umma.

Jana, Mnyika, ambaye ni mbunge wa Kibamba (Chadema), alirejea maazimio ya Bunge la Kumi akisema lilishafanya maamuzi kuhusiana na mikataba ambayo Serikali inaingia na kampuni mbalimbali, hasa kwenye sekta ya nishati na madini.

“Katika maazimio ya Bunge kuhusiana na fedha, ufisadi uliofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa IPTL yanayohusu sekta ya nishati na madini, bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake,” alisema Mnyika.

 Akinukuu Azimio Namba 2, Mnyika alisema liliagiza kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha inazolipa kwa kampuni hiyo binafsi.

Alisema kambi hiyo inasikitika kuona kwamba mbali ya Serikali kushindwa kununua, bado inaendelea kulipia gharama za uwekezaji na hivyo kuendelea kukiukwa kwa azimio hilo.

Akizungumzia azimio la saba linalohusu kuwajibishwa kwa mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na bodi ya Tanesco, Mnyika alisema Profesa Muhongo naye aliwajibishwa kwa uteuzi wake kutenguliwa, lakini Rais Magufuli amemteua tena kuongoza wizara hiyo.

“Rais bila ya kujali nini Bunge lilishaazimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya azimio hilo, akamteua Muhongo kuendelea kuiongoza wizara hii. Kambi ya upinzani inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge na ni fedheha binafsi kwake,” alisema.

Alisema kambi ya upinzani imelazimika kunukuu maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa kutekeleza maazimio ya Bunge na badala yake mikataba hiyo inaendelea kutekelezwa kama ilivyoingiwa.

“Mfano mzuri ni Tanesco kuendelea kuilipa IPTL fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi kuliondolea shirika hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwa kuwa haliwezi kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kusambaza umeme kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha,” alisema.
Share:

Keissy Amvaa John Mnyika......Asema Hapaswi Kumfananisha Profesa Muhongo na Edward Lowassa

Jina la aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa, jana liliingia tena katika Bunge la Kumi na Moja na kuzua mvutano.

Lowassa alitajwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), wakati akijibu hoja za Mbunge wa Kibamba, John Mnyika aliyekuwa akihoji na kuonesha kushangazwa na uteuzi wa Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati alijiuzulu bungeni hapo baada ya kuelemewa na kashfa ya akaunti ya ‘Tegeta Escrow’.

Akijibu hoja hizo, Keissy ambaye siku zote ni mbunge mwenye hoja machachari alimvaa Mnyika  na kuhoji mbona wao ( UKAWA) walimchukua  Lowassa na kumfanya  kuwa mgombea wao wa Urais  wakati alijiuzulu uwaziri Mkuu kwa kashfa ya Richmond.

“Mnabeza  uteuzi wa Muhongo wakati Lowassa alivyojiuzulu hapa hapa bungeni mlimchukua mkamtembeza nchi nzima. Leo angekua Rais mgesema nini?" Alihoji Keissy .

Mnyika alikuwa alisoma hatuba ya kambi ya upinzani kwa Wizara ya Nishati na Madini ambayo ilikuwa ikiponda uteuzi wa Profesa Muhongo
Share:

Thursday, May 19, 2016

Mbunge wa CCM Anusurika Kupigwa na Wabunge wa UKAWA

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jackline Msongozi juzi jioni alinusurika kipigo kutoka kwa wabunge wanawake wa UKAWA baada ya kuwaeleza kuwa upande huo una wabunge wawili tu wenye michango ya maana ambao ni Upendo Peneza (Viti Maalumu Chadema) na Magdalena Sakaya (Kaliua - CUF).

Akichangia mjadala wa bajeti kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Msongozi aliishambulia kambi ya upinzani akieleza kuwa kuna mlevi mmoja amechangia upande wa upinzani kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali wakati waliohusika na uuzwaji huo wamehamia upinzani ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Msongozi alisema hakuna mke mwenza anayeweza kumsifia mwenzake, hivyo upinzani hauwezi kuisifia CCM kutokana na kazi wanayoifanya.

Baada ya kusema maneno hayo na wabunge wengine kuchangia, Bunge lilipoahirishwa wabunge wanawake wa upinzani wakiongozwa na Sabrina Sungura na Ester Matiko walimfuata Msongozi wakitaka kumshambulia, lakini aliondoka moja kwa moja pasipo kusimama popote.

Sungura alipoulizwa alisema kuwa mbunge huyo angesimama wangemshughulikia.
Share:

Zitto Kabwe, Halima Mdee na John Heche Wawekwa Kitimoto.....Wahojiwa Kwa Dakika 90 Kwa Kufanya Fujo Bungeni

MBUNGE wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) na wenzake wawili, jana wamehojiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika kwa kufanya fujo bungeni kuhusu suala la Bunge kutorushwa ‘live’.

Mbali na Zitto, wengine waliohojiwa ni pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema). Wabunge hao walihojiwa kwa tuhuma za kufanya fujo bungeni wakati ilipotolewa hoja ya Bunge kutorushwa moja kwa moja ‘live’, akiwa pamoja na wabunge wawili; Mdee na Heche.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kamati hiyo, kimesema Zitto alihojiwa na kamati hiyo kwa muda wa zaidi ya saa moja kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kufanya fujo bungeni Januari 27, mwaka huu.

Taarifa hizo zilieleza kuwa Zitto alifanya fujo hizo baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, kuahirisha kujadili hoja ya serikali iliyowasilishwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kuhusu Bunge kutorushwa ‘live’.

Hatua hiyo inatokana na hoja iliyowasilishwa na Zitto aliyetaka kuahirishwa kujadili hotuba ya Rais kutokana na kauli ya Waziri Nape ya kutorushwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Zitto, alihojiwa na kamati hiyo ya Mkuchika kwa kilichoelezwa alisimama na kuomba mwongozo kuhusu jambo ambalo limekwishatolewa uamuzi kinyume na Kanuni ya 72 (1) na 68 (10 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

Mbali na hilo pia anadaiwa kusimama na kuzungumza bila utaratibu kinyume na Kanuni ya 60 (2) na 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, jambo ambalo lilileta fujo na kuvunja shughuli za Bunge.

Katika barua za mwito zilizosainiwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah, Mei 12, mwaka huu, inaelezwa kwamba pamoja na mambo mengine na Mwenyekiti wa Bunge kumsihi mbunge huyo bado aliendelea kuzungumza na kusimama ikiwa ni kuonesha dharau kwa mamlaka ya Spika na shughuli za Bunge kinyume na kifungu namba 24 (d) na (e) cha Sheria ya Kinga na Haki za Bunge.

Barua hiyo ilieleza kuwa kutokana na vitendo hivyo vinavyokiuka Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Sura namba 296 na Kanuni za Bunge, wabunge hao walionywa kuwa endapo wasingefika mbele ya kamati hiyo jana hatua za kisheria zingechukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa kifungu cha 15 na 31 (1)(a) na sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge.
Share:

Saturday, May 14, 2016

Nape Nnauye Asulubiwa Bungeni ......Wabunge Wamwita ni Waziri Mzigo ( Lumbesa)

Wabunge wamemcharukia Waziri wa Habari, Nape Nnauye kwamba aliwahi kuwaita mawaziri wa Serikali iliyopita mizigo, lakini yeye amezuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, ili wananchi washindwe kumpima kama ni mzigo au lumbesa. 

Hayo yalijitokeza jana wakati wabunge walipochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari kwa mwaka 2016/2017, iliyowasilishwa bungeni na Waziri Nape. 

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) alieleza kushangazwa na hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhimiza wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa, lakini haitaki wananchi waone inavyopanga matumizi yake. 

Alisema Nape akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliwaita baadhi ya mawaziri ni mizigo, lakini amepewa wizara hiyo amezuia mijadala ya wazi ambayo ingesaidia wananchi kumpima.

“Nilipoona amepewa wizara ya habari nikajua ataruhusu mijadala ya wazi ili tumuone yeye kuwa hatakuwa mzigo, lakini yeye akawa lumbesa. Hilo amelizuia kwa hiyo tunashindwa kumpima,” alisema. 

Alisema waziri huyo hawezi kukwepa lawama ya hicho kinachoendelea cha kuzuia matangazo ya Bunge, kwa vile wanaopiga picha na kuhariri taarifa zinazorushwa ni watumishi wa TBC. 

Udhibiti wa Bunge 
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act-Wazalendo), alisema kuwa wabunge wote waliopinga Bunge kutoonyeshwa ‘live’ na kusababisha mtafaruku bungeni, wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge. 

“Wabunge hapa tulisimama tukapinga na wapo waliounga mkono, lakini kiti chako kimetuita wabunge wote tuliopinga kauli ya Serikali kwenye kamati ya maadili. Jana mimi nimepata barua,” alisema Zitto. 

“Kwamba mnatubana kusema. Mnazuia Bunge lisionekane. Hata kutoa maoni ndani ya Bunge tunakwenda kuhojiwa? TBC ni chombo cha umma, siyo chombo cha Serikali, inaendeshwa kwa kodi za wananchi,” alisisitiza. 

Baada ya mchango huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema si kweli wabunge hao wanahojiwa kutokana na michango yao, bali wanahojiwa kutokana na mambo waliyoyafanya kwa kutotii maagizo ya kiti wakati wa mjadala wa ‘Bunge Live’. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliunga mkono hoja ya Zitto ya kuifanya TBC iendeshwe kama inavyoendeshwa BBC kwa kupewa  leseni maalumu. 

Pia, aliitaka Serikali kupeleka muswada bungeni utakaowabana wamiliki wa vyombo vya habari kuwa na mikataba na waandishi wanaowaandikia, pia, akadai baadhi ya vyombo haviwalipi waandishi wake. 

Hata hivyo Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Marwa (CCM) alitetea uamuzi wa Serikali kuondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, akisema wabunge wanaodai hilo ni wale waliokuwa wakiuza sura. 

Katika hatua nyingine, Waitara alisema kitendo cha Nape kuwaalika wabunge kwenye muziki, baada ya bajeti yake kupita ilikuwa ni kuwahonga. 

Juzi jioni wakati akitoa matangazo kabla ya kuahirisha Bunge, Naibu Spika alisema baada ya kupitisha bajeti ya Wizara ya Habari, wanamuziki Diamond Plutnum na King Kiki watatumbuiza katika viwanja vya Bunge. 

“Mnaposema mnabana matumizi hao wanamuziki wameletwa kwa gharama za nani,” alihoji mbunge huyo.

 “Wabunge wote ambao wataenda katika hiyo miziki ili kuunga mkono habari ya Nape mtakuwa mmekula rushwa,” alisisitiza Waitara, kauli ambayo ilimfanya Naibu Spika, Dk Tulia kufafanua, akisema suala hilo lilitangazwa bungeni kama mengine, lisiingizwe kosa la jina la rushwa. 

Upinzani na udikteta 
Msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Joseph Mbilinyi, alisema kitendo cha Serikali kuminya uhuru wa habari ni kuelekea kwenye udikteta.

 “Kana kwamba haitoshi, Serikali sasa imezuia Televisheni ya Umma, inayoendeshwa na kodi ya wananchi (TBC1) kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mijadala inayofanyika bungeni. Dalili hizi siyo njema kwa ukuaji wa demokrasia na uhuru wa habari hapa nchini na zinatoa taswira ya utawala wa ki-dikteta,” alisisitiza. 

“Tunaitaka Serikali kuliomba radhi Bunge hili, kwa kosa la kuminya uhuru wa habari kinyume na Katiba na kuviacha vyombo vya habari hususan vya umma kufanya kazi zao za kuhabarisha umma kwa uhuru,” alisema.
Share:

Friday, May 13, 2016

Spika Job Ndugai Awagomea Wabunge Waliotaka Utaratibu wa Kusaini Mara Mbili Kwa Vidole Ufutwe

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amejibu mwongozo ulioibuliwa na wabunge bungeni wa kutaka utaratibu wa kusaini kwa kutumia kidole mara mbili kwa siku uondolewe, kwa kusisitiza kuwa utaratibu huo hautabadilishwa.

Majibu ya mwongozo huo aliyatoa bungeni Dodoma jana wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), aliyemtaka Spika autolee majibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Konde Khatib Said Haji hivi karibuni wa kutaka utaratibu huo ufutwe.

“Mheshimiwa Spika inaonesha kuna dalili ya Bunge lako kutojibu miongozo inayoulizwa hapa bungeni. Hivi karibuni tuliuliza juu ya namna ya kusaini kwa kutumia madole sijui kidole lakini mpaka leo hatujapatiwa majibu,” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Ndugai alijibu kwa kifupi kuwa utaratibu wa kusaini wabunge ni mara mbili kwa siku na wanatakiwa wakandamize kidole chao hadi taa ya kijani iwake ndipo watakuwa wamesajiliwa rasmi.

“Nataka nitoe ufafanuzi, nasikia kuna malalamiko juu ya utaratibu wa kusaini, maagizo ni hivi, unaposaini pale kandamiza kidole chako hadi taa ya kijani iwake, utakuwa tayari umesajiliwa si kugusa tu. Ule mfumo unaitwa press and hold,” alisema Spika na kufunga mjadala wa suala hilo.

Hivi karibuni, Mbunge Haji, aliomba mwongozo na kuitaka ofisi ya Bunge iwaondolee mara moja utaratibu wa kusaini kwa kutumia vidole mara mbili kwa siku kwa kuwa wao si wanafunzi.

Katika mwongozo wake, alisema kitendo cha kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku ni kero kwa wabunge na uonevu kwa kuwa hata Bunge hilo limekuwa likitumia muda wa mapumziko wa wabunge kwa kazi za Bunge.

“...tatizo langu ni kitendo cha wabunge kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku asubuhi na jioni, wakati mwingine tunatoka hapa saa saba, wabunge tunashughulikia mambo mpaka saa 12, mbunge anatumia muda wake wa mapumziko na ule wa kuhudhuria kikao cha jioni,” alisema.

Alisema inasikitisha kuona mbunge anatolewa kwenye kazi za kujenga taifa ili aje tu asaini kwa kidole tena mara ya pili. 

Alisema jambo hilo linawatatiza wabunge kwa kuwa wanajiona kama wanachukuliwa kama wanafunzi kwa kufuatiliwa kwani hata kwenye benki wafanyakazi hawasaini na kufuatiliwa kama ilivyo kwa wabunge hao.

Alifafanua kuwa kabla ya kuomba mwongozo huo, alifanya utafiti kwenye benki mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao nao wana utaratibu kama huo wa Bunge lakini hakuna mahali wanapotakiwa kusaini kwa vidole mara mbili.

Kwa upande wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson wakati akijibu mwongozo huo alisema kutokana na namna wabunge hao walivyopokea suala hilo, pamoja na kwamba kikanuni jambo hilo halikutakiwa kuombewa mwongozo bado litaangaliwa. 

“Hata hivyo nifafanue kuwa kusaini mara mbili lengo lake si kuwafanya wabunge wanafunzi, ila lengo ni kutaka kujua nani wapo humu ndani (bungeni),” alisema Dk Ackson.
Share:

Mbunge Apewa Siku 3 Atoe Ushahidi wa Magari 777 ya Washawasha

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amempa siku tatu Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema) awasilishe mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge, maelezo ya utetezi dhidi ya madai aliyotoa bungeni kuhusu Serikali kununua magari ya washawasha 777.

Ndugai alitoa amri hiyo kutokana na mwongozo ulioombwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni juzi akitaka Lyimo athibitishe au afute kauli yake juu ya madai hayo wakati serikali imenunua magari 32.

“Hata kwa akili ya kawaida haiwezekani Serikali ikaagiza magari yote hayo 777 ya washawasha. Ninachokumbuka mimi Waziri huyu aliwahi kusema hapa bungeni kuwa magari hayo 777 ni idadi ya magari yote ya aina mbalimbali yaliyonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya polisi,” alisisitiza Ndugai.

“Sasa nakutaka uniandikie rasmi majibu vizuri kuhusu kauli yako hii, nakupa siku tatu uwe umeniletea na baadaye nitaipeleka taarifa yako kwa Kamati ya Maadili ya Bunge, ili kujadili suala hili kwa mapana,”alisisitiza Ndugai.

Awali mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Ndugai alimpatia mbunge huyo nafasi ya ama kufuta kauli yake hiyo au aithibitishe kabla ya hatua za kikanuni za Bunge hazijachukuliwa dhidi yake.

Lyimo alikataa kufuta kauli hiyo na kudai kuwa anao uthibitisho juu ya idadi hiyo ya magari aliyoitamka na kusisitiza kuwa amenukuu taarifa za idadi hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na mtandao wa Jamii forum pamoja na taarifa za Hansad za Bunge.

“Mheshimiwa Spika mimi ni mtu mzima siwezi kwenda kwa hisia za watu, ni kweli jana niliombewa mwongozo bahati mbaya sikuwepo ndani ya Bunge. Nathibitisha kauli yangu na wala siifuti kwa kuwa nina uhakika na idadi ya magari niliyoisema,” alisisitiza mbunge huyo.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 63 (2) ya Bunge, mbunge hatasema uongo endapo chochote atakachokisema ndani ya Bunge atakuwa amekirejea kwenye chombo cha habari au taarifa za Bunge.
Share:

Thursday, May 12, 2016

Mbunge wa Ulanga, Godluck Mlinga (CCM) Atoa Tuhuma nzito kwa TRA, TCRA, EWURA

Mbunge wa Ulanga, Godluck Mlinga (CCM) ameyatuhumu mashirika ya umma ambayo hayajajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuwa watendaji wake wakuu wamepewa malipo ya asilimia 10 ili mashirika hayo yajiunge na kampuni binafsi za bima.

Ameyataja baadhi ya mashirika hayo ya umma yaliyokaidi kujiunga na NHIF licha ya kulazimishwa kisheria kuwa ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Yapo mashirika ya umma yanakataa kujiunga na NHIF wakati sisi wabunge tumejiunga, wao ni nani? Wakubwa wao wanapata asilimia 10 na wanajiunga na kampuni za bima ya afya binafsi…

“Mimi niliwahi kuwa Compliance Officer wa NHIF nikaenda TRA, nikawaeleza umuhimu wa kujiunga NHIF unachangia pesa kidogo unapata huduma nyingi lakini bosi wao akanijibu pesa si tatizo na afadhali ametumbuliwa huyo bosi wao, yule angekuwa ofisini kwangu asingetoka,” alisema Mlinga na kuongeza:

“Kila sehemu wananitaja Mlinga Mlinga, napata vitisho vingi lakini serikali inanilinda na kama jeshi (JWTZ) limeweza kusambaratisha M23 itashindwa kunilinda mimi…wengine wananiita teja hivi teja anavaa suti iliyonyooka kama mimi, siwezi kukasirika kwa sababu si kweli lakini wangeniita mbilikimo ningekasirika kwa sababu kweli.”

Mbunge huyo alitaka serikali ikomeshe tabia ya wanaume kubaka wazee na kufafanua “najiuliza wanawake wa mikoa yenye ubakaji wa wazee ni wagumu kuelewa hadi wazee wabakwe?”

Naye Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM) amesema sasa ataanza kuacha kuwashawishi wananchi wake kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kutokana na mfuko huo kutopeleka dawa na chanjo za watoto kwenye vituo vya afya, badala yake inapeleka kondomu na vifaa visivyo muhimu kwa wananchi.
Share:

Tuesday, May 10, 2016

Mbunge Adai Kuna Wabunge Wanavuta Bangi na Madawa ya Kulevya Bungeni

Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Msabaha (Chadema) ametoa tuhuma nzito kuwa ndani ya Bunge kuna wabunge vijana wanaovuta bangi na kutumia dawa za kulevya.

Mbunge huyo amemuomba Rais John Magufuli kuagiza wabunge wa aina hiyo ambao hata hivyo hakuwataja wapelekwe Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufundishwa nidhamu.

Msabaha ametoa kauli hiyo Bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya Ulinzi na JKT iliyowasilishwa na Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo, Dk Hussein Mwinyi.

“Wabunge nao waende JKT kwa sababu hili Bunge wameingia vijana wengine ambao ni mateja wa unga na wengine wanavuta bangi. Wengine wanawavua mama zao nguo,” amesema Msabaha.

“Wengine mama zao wameshakufa wanakuja humu wanawatukana mpaka wazazi wao. Kwa hiyo niombe Rais Magufuli vijana wote wabunge ambao hawana nidhamu waende JKT,” alisisitiza.

Mbunge huyo amesema wabunge wa aina hiyo hawana viwango vya kuzungumza ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria hivyo ni vyema waende JKT ili wakirudi wawe wamejua namna ya kuchangia.

Ingawa hakumtaja Mbunge yeyote, lakini mchango  ulioibua mtafaruku bungeni ni wa Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga aliyedai wabunge wa viti maalumu Chadema huitwa Baby ili kupewa nafasi hiyo.

Tafsiri ya kauli hiyo ni kuwa wabunge wa viti maalum Chadema lazima wafanye mapenzi au kuwa na mahusiano na viongozi wa juu wenye mamlaka ndani ya chama hicho ndipo wateuliwe kuwa wabunge.
Share:

Mbunge Apinga Wakunga Wanaume Kuruhusiwa Kuwahudumia Wanawake Wakati wa Kujifungua

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Mngwali amepinga mpango wa Serikali kuajiri wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati kuhudumia wajawazito wakati wa kujifungua kuwa ni udhalilishaji dhidi ya wanawake.

Mbunge huyo ameitaka Serikali kuzingatia mila za Kiafrika, akisema imezoeleka kuwa huduma ya ukunga kwa wajawazito wakati wa kujifungua hutolewa na wataalamu wanawake.

“Serikali haioni kuwa kwa kuweka wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati zake nchini ni kuwadhalilisha wajawazito wanaojifungua?”alihoji Mngwali.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jaffo alisema wakunga wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga inayowataka kutoa huduma ya kumsimamia mjamzito wakati wa uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua bila kujali jinsia.

Alisema pamoja na sheria hiyo, kumekuwa na changamoto zinazotokana na mila na desturi za jamii ambazo husababisha baadhi ya wahitaji wa huduma hiyo kutokubali kuhudumiwa na wakunga wanaume.

“Kutokana na hali hii, Serikali itaendelea kuajiri wataalamu wengi ili pale penye changamoto paweze kupatiwa ufumbuzi bila kukwaza jamii husika,” alisema Jaffo.

Naibu waziri alisema hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mbunge huyo kuuliza swali hilo bungeni, lakini tayari amewasiliana na uongozi wa Mkoa wa Pwani ambao umeeleza kuanza kulifanyia kazi jambo hilo na kwa baadhi ya maeneo wameshaanza kupeleka wakunga wanawake.
Share:

Sunday, May 8, 2016

Kwa Hali Iliyopo Sasa Hivi Ni Ndoto Tanzania Kuwa na Uchumi wa Viwanda

Wabunge wamesema ni vigumu Tanzania kufikia lengo la kuwa na uchumi wa viwanda iwapo Serikali itaendelea kusuasua kutekeleza miradi yenye mchango mkubwa katika sekta hiyo.

Akisoma maoni ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka 2016/17, Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Vicky Kamata alisema hawaridhishwi na namna Serikali inavyotoa fedha za bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Kwa kuzingatia takwimu hizi ni dhahiri miradi mingi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha haitatekelezwa,” alisema Kamata.

Alisema kamati hiyo inaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa azma hiyo.

“Hali hii ikiendelea itakuwa vigumu Tanzania kuwa nchi ya viwanda iwapo Serikali itaendelea kuchelewesha utekelezaji wa miradi yenye mchango mkubwa katika sekta hii,” alisema.

Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu alisema: “Kamwe tusijiaminishe kuwa tunaweza kufikia Taifa la viwanda kwa Sh42.159 bilioni kwenye bajeti ya mwaka kama fedha za maendeleo kwa ajili ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,” alisema.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni jana Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kati ya viwanda 106 vilivyofanyiwa tathmini, viwanda 45 vinafanya kazi, 24 vinasuasua na 37 vimefungwa.

“Mpango wetu ni kuhakikisha kuwa viwanda 35 vilivyobaki vinafanyiwa tathmini haraka na kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi mwaka huu, hatima ya viwanda visivyofanya kazi itajulikana,” alisema.

Alisema hatima ya wenye viwanda visivyofanya kazi ni kwa wamiliki kutekeleza mkataba ya mauzo au kupewa wawekezaji wapya ili waviendeleze,” alisema.

Wizara hiyo imeomba kutengewa Sh 81.87 bilioni katika mwaka wa fedha 2016/17 kati ya hiyo, Sh41.87 bilioni sawa na asilimia 51 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh40 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Share:

Saturday, May 7, 2016

Tundu Lissu Ataka Serikali Itaje Umri wa Jaji Mkuu Chande na Iseme Lini Atastaafu

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ameitaka serikali itaje umri wa Jaji Mkuu, Othman Chande, ama kuweka wazi ni lini atastaafu.

“Hivi umri wa kustaafu kwa jaji mkuu ni miaka mingapi?" Aliuliza Lissu Bungeni juzi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

"Ina maana Jaji Mkuu hajafikia umri wa kustaafu? Wenzake wote aliokuwa nao darasa moja akiwemo Jaji (Januari) Msofe, Jaji Masatu, (Jaji) Dk. (Steven) Bwana wamestaafu miaka mingi.

"Tunataka kujua ni lini (Jaji Mkuu) atastaafu.”

Aidha Lissu alisema kumekuwa na mahakama ya mafisadi nchini tangu mwaka 1984, na akashangaa kusikia kuwa serikali imepanga kuianzisha wakati kwa miaka 32 iliyopita imekuwa ikiitwa Mahakama ya Wahujumu Uchumi.

Alisema mahakama hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria, katika kipindi cha uongozi wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Sokoine aliyeanzisha vita dhidi ya wahujumu uchumi na walanguzi.

Lissu alisema mahakama kuu inaposikiliza kesi zote za rushwa, kesi za kutakatisha fedha haramu, kesi za kuhujumu uchumi, chini ya sheria za madawa ya kulevya huwa inakaa kama mahakama ya mafisadi.

“Sasa ninashangaa ninapomsikia mtu akisema ninampongeza mheshimiwa Rais (John Magufuli) kwa kuanzisha mahakama ya mafisadi," alisema Lissu.

"Nani aliyewaambia hakuna mahakama ya mafisadi? Kama mnataka kuibatiza semeni halafu ukiuliza huo muswada upo wapi, wanasema itaanzishwa kama Divisheni ya Mahakama Kuu.

"Divisheni ya mahakama kuu inahitaji sheria. Ipo Divisheni kwenye Mahakama Kuu ya Ardhi na imeundwa kwa mujibu wa sheria.”

Alisema mahakama hiyo ya mafisadi ambayo inaanza, haelewi inaazishwa kwa sheria ipi.

Akiwasilisha bajeti ya Ofisi yake Bungeni mwezi uliopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema serikali itaanzisha Mahakama ya Mafisadi ikiwa ni Divisheni ya Mahakama Kuu kuanzia mawezi ujao.

Lissu alisema kutokana na uzoefu aliokuwa nao katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuna tatizo kubwa la uendeshaji wa kesi za ufisadi.
Share:

Mbunge Ataka Walawiti na Wabakaji Wahasiwe

MBUNGE wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka (CCM) ametaka watu wanaohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji na ulawiti, wahasiwe ili wawapo gerezani wasiendeleze tabia hizo.

“Tumeshaona wanaohukumiwa kifungo cha maisha, wakiwa huko gerezani wanaendeleza vitendo vya kulawitiana, kwa nini sasa wasihasiwe?” Alihoji. 

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, wakati akimjibu jana alisema, “siwezi kuwa na jibu kwa sababu Bunge ndilo linalotunga sheria, mbunge aje na wazo lake hapa bungeni lipitishwe kama sheria sisi Serikali hatuwezi.”

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya hali ya ubakaji na ulawiti, Dk Mwakyembe alisema kila siku nchini kunaripotiwa matukio 19 ya kubakwa na kulawitiwa.

Alisema hali ni mbaya sana na sasa kuna mashauri 2,031 yaliyoripotiwa mahakamani katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu. 

Kati yake mashauri hayo, 111 yameshakamilishwa kwa kuhukumiwa ambapo watu 99 wamefungwa, watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi na kesi 1,920 hazijakamilika.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo aliyehoji mpango wa Serikali kuhakikisha kesi za kubakwa na kulawitiwa hazimalizwi kifamilia, Dk Mwakyembe alisema kumalizwa kwa kesi kifamilia kunachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii.

“Tatizo la kuficha ushahidi na kumaliza kesi hizo kifamilia, haliwezi kumalizwa na vyombo vya dola peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na watuhumiwa. Hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuwa kuficha ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ya jinai kifamilia si kosa peke yake, bali vilevile utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii,” alifafanua.

Ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, alisema Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi.

“Pindi tukio la kubaka au kulawiti litakaporipotiwa, upelelezi hufanyika na mtuhumiwa kufunguliwa mashitaka mara moja, kwa utaratibu huu Serikali inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki jinai,” alisema.

Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana. Pia sheria imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 kwa kosa la kulawiti.
Share:

Friday, May 6, 2016

Kimenuka! Wabunge Wanawake UKAWA Watoka Bungeni Baada ya Mbunge wa CCM Kusema Nafasi Zao Zinapatikana kwa Rushwa ya Ngono

Kikao cha Bunge leo kimechafuka baada ya wabunge wanawake wa Ukawa kutoka nje ishara ya kupinga kitendo cha wao kuambiwa nafasi zao za viti maalumu zinatolewa kwa njia ya ngono ya Ruswa.

Matamshi hayo yametolewa leo na Mbunge wa Ulanga Mh Goodluck Mlinga wakati kikao cha Bunge kikiendelea.

TAZAMA VIDEO HAPO CHINI
Share:

Mwita Waitara Azusha Tafrani Bungeni.......Ni Baada ya Kutaka Kumchapa Ngumi Mbunge wa Kasulu Aliyedai Tundu Lissu na Mnyika Ni Vichaa

Mbunge  wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) ametolewa nje ya Bunge baada ya kutaka kumkwida Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustine Holle (CCM) aliyedai kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wote wa Chadema kuwa wanaugua kichaa.

Waitara alionesha kukerwa na kauli hiyo hasa pale Holle alipokataa kufuta kauli yake, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika, Dk Tulia Akson.

Wakati Holle akichangia, Waitara alinyanyuka kwenye kiti chake na alipofika alipo mbunge huyo alimzungumzisha maneno ambayo hayakusikika na kuonesha kama kutaka kumpiga kabla ya kukaa kwenye kiti kilicho mbele yake ndipo, Holle alisikika akisema “wewe unataka nini” ndipo Naibu Spika alipogundua kuwa Waitara anataka kumpiga Holle na kumuamuru atoke nje lakini hakutii amri hiyo.

Kutokana na kutotii, Naibu Spika aliamuru askari wamtoe ndipo walipoingia zaidi ya askari watano na kutoka naye hadi nje ya geti kubwa la kuingilia bungeni.

Holle wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alimtaja Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo kuwa ana taarifa kuwa Lissu amewahi kuugua ugonjwa wa kichaa na hadi sasa ana faili kwenye Hospitali ya Vichaa ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma.

Hata hivyo, alipopewa nafasi na Naibu Spika kufuta kauli yake akasema “nafuta kauli yangu lakini kwa taarifa zilizozagaa nimeamini ni kweli na mbona kwao(Chadema) wapo wengi hata Mnyika sasa hivi yupo Muhimbili anatibiwa kichaa”.

Kutokana na kauli hiyo, Lissu alisema licha ya kuifahamu Hospitali ya Mirembe, hajawahi hata kuingia kwenye geti la hospitali hiyo wala kuugua ugonjwa huo na kutaka kiti cha Naibu Spika kimtake Holle athibitishe ; na akishindwa kanuni zielekeze hatua za kuchukua kama zilivyowekwa.
Share:

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger