Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ameitaka serikali
itaje umri wa Jaji Mkuu, Othman Chande, ama kuweka wazi ni lini
atastaafu.
“Hivi umri wa kustaafu kwa jaji mkuu ni miaka mingapi?" Aliuliza Lissu
Bungeni juzi wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
"Ina maana Jaji Mkuu hajafikia umri wa kustaafu? Wenzake wote aliokuwa
nao darasa moja akiwemo Jaji (Januari) Msofe, Jaji Masatu, (Jaji) Dk.
(Steven) Bwana wamestaafu miaka mingi.
"Tunataka kujua ni lini (Jaji Mkuu) atastaafu.”
Aidha Lissu alisema kumekuwa na mahakama ya mafisadi nchini tangu mwaka
1984, na akashangaa kusikia kuwa serikali imepanga kuianzisha wakati kwa
miaka 32 iliyopita imekuwa ikiitwa Mahakama ya Wahujumu Uchumi.
Alisema mahakama hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria, katika kipindi
cha uongozi wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Sokoine aliyeanzisha
vita dhidi ya wahujumu uchumi na walanguzi.
Lissu alisema mahakama kuu inaposikiliza kesi zote za rushwa, kesi za
kutakatisha fedha haramu, kesi za kuhujumu uchumi, chini ya sheria za
madawa ya kulevya huwa inakaa kama mahakama ya mafisadi.
“Sasa ninashangaa ninapomsikia mtu akisema ninampongeza mheshimiwa Rais
(John Magufuli) kwa kuanzisha mahakama ya mafisadi," alisema Lissu.
"Nani aliyewaambia hakuna mahakama ya mafisadi? Kama mnataka kuibatiza
semeni halafu ukiuliza huo muswada upo wapi, wanasema itaanzishwa kama
Divisheni ya Mahakama Kuu.
"Divisheni ya mahakama kuu inahitaji sheria. Ipo Divisheni kwenye Mahakama Kuu ya Ardhi na imeundwa kwa mujibu wa sheria.”
Alisema mahakama hiyo ya mafisadi ambayo inaanza, haelewi inaazishwa kwa sheria ipi.
Akiwasilisha bajeti ya Ofisi yake Bungeni mwezi uliopita, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alisema serikali itaanzisha Mahakama ya Mafisadi ikiwa
ni Divisheni ya Mahakama Kuu kuanzia mawezi ujao.
Lissu alisema kutokana na uzoefu aliokuwa nao katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, kuna tatizo kubwa la uendeshaji wa kesi za ufisadi.
0 comments:
Post a Comment