Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema tatizo la sukari nchini limetokana
na uamuzi usio sahihi wa Rais Dk. John Magufuli, kwa kupiga marufuku
uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi bila kufanya tathmini.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari, Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu, alisema agizo hilo lilitolewa kwa
kukurupuka na ndilo lililosababisha sukari kuadimika.
Komu
ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini, alisema kama malengo ni kulinda
viwanda vya ndani, basi lisifanyike kwa sukari pekee kwa sababu viwanda
vipo vingi na bado bidhaa zinaingia kutoka nje nchi.
Alisema
kuna harufu ya upendeleo kutokana na Rais kuwa swahiba wa Rais mstaafu
wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye ni mmiliki wa mashamba ya
Mtibwa, hivyo amefanya hivyo kwa kupewa ushauri mbaya huku nchi ikiingia
kwenye upungufu mkubwa wa sukari.
Alihoji
kwa nini apige marufuku kwenye sukari tu wakati kuna viwanda vya nondo,
saruji na vinginevyo na vinaleta bidhaa kutoka nje.
Alisema kilichofanywa na Rais ni kukurupuka na ni kuvunja sheria.
Komu
alisema kitendo cha Rais kutoa amri ya walioficha sukari
wany’ang’anywe, ni kupora haki za watu na kuua mitaji yao kibiashara.
“Hakuna
sheria ambayo inaruhusu kwenda kukagua maghala ya wafanyabiashara na
kugawa bidhaa bure, hii hali hata wawekezaji wataogopa kuja kuwekeza
nchini kwa sababu wataona mazingira ya hapa nchini ni hatarishi," alisema Komu.
Alisema serikali iandae njia mbadala ya kuwafidia watu walionyang’anywa maana wengine wamekopa kwenye taasisi za kifedha.
“Agizo
la Rais lina walakini, kwani ni nani katika biashara za
watu...tunakokwenda ni kubaya kwani upungufu wa sukari ulijulikana tangu
Februari, lakini akapiga marufuku sukari kutoka nje,” alisema Komu.
Alisema
katika tafiti mbalimbali ikiwamo ripoti iliyotolewa na Shirika la BBC,
mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 590,000, lakini uwezo uliopo
ni tani 300,000, hivyo serikali ilikuwa ni busara iruhusu kuingizwa kwa
sukari kwa sababu viwanda vya ndani vimekosa uwezo.
Alisema
Rais anatakiwa kukemewa na kuambiwa kwamba anakwenda kinyume na kwamba
wao kambi ya upinzani hawatetei wanaoficha sukari, lakini serikali
itafute namna ya kukabili hali hiyo.
Naye
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema taifa lina viwanda vinne
vikubwa vya sukari, lakini bado havina uwezo wa kuzalisha sukari ya
kutosha.
Alisema serikali imefanya sukari ionekane kama dawa za kulevya kutokana na kuadimika huko.
Alisema
sukari hadi iletwe nchini, ni takriban wiki tano na wanaoingia kwenye
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani watahitaji sukari kushinda vitu vingine.
“Sisi
hatutetei walioficha, lakini wamenunua ili kuuza kwa taratibu kulingana
na bei ya soko wasibughudhiwe maana kuna hatari ya benki kushindwa
kurejeshewa fedha zilizokopwa,” alisema Kubenea.
0 comments:
Post a Comment