SPIKA
wa Bunge, Job Ndugai amejibu mwongozo ulioibuliwa na wabunge bungeni wa
kutaka utaratibu wa kusaini kwa kutumia kidole mara mbili kwa siku
uondolewe, kwa kusisitiza kuwa utaratibu huo hautabadilishwa.
Majibu
ya mwongozo huo aliyatoa bungeni Dodoma jana wakati akijibu mwongozo
ulioombwa na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), aliyemtaka
Spika autolee majibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Konde Khatib Said
Haji hivi karibuni wa kutaka utaratibu huo ufutwe.
“Mheshimiwa
Spika inaonesha kuna dalili ya Bunge lako kutojibu miongozo inayoulizwa
hapa bungeni. Hivi karibuni tuliuliza juu ya namna ya kusaini kwa
kutumia madole sijui kidole lakini mpaka leo hatujapatiwa majibu,” alisema.
Akijibu
mwongozo huo, Ndugai alijibu kwa kifupi kuwa utaratibu wa kusaini
wabunge ni mara mbili kwa siku na wanatakiwa wakandamize kidole chao
hadi taa ya kijani iwake ndipo watakuwa wamesajiliwa rasmi.
“Nataka
nitoe ufafanuzi, nasikia kuna malalamiko juu ya utaratibu wa kusaini,
maagizo ni hivi, unaposaini pale kandamiza kidole chako hadi taa ya
kijani iwake, utakuwa tayari umesajiliwa si kugusa tu. Ule mfumo unaitwa
press and hold,” alisema Spika na kufunga mjadala wa suala hilo.
Hivi
karibuni, Mbunge Haji, aliomba mwongozo na kuitaka ofisi ya Bunge
iwaondolee mara moja utaratibu wa kusaini kwa kutumia vidole mara mbili
kwa siku kwa kuwa wao si wanafunzi.
Katika
mwongozo wake, alisema kitendo cha kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku
ni kero kwa wabunge na uonevu kwa kuwa hata Bunge hilo limekuwa
likitumia muda wa mapumziko wa wabunge kwa kazi za Bunge.
“...tatizo
langu ni kitendo cha wabunge kutakiwa kusaini mara mbili kwa siku
asubuhi na jioni, wakati mwingine tunatoka hapa saa saba, wabunge
tunashughulikia mambo mpaka saa 12, mbunge anatumia muda wake wa
mapumziko na ule wa kuhudhuria kikao cha jioni,” alisema.
Alisema inasikitisha kuona mbunge anatolewa kwenye kazi za kujenga taifa ili aje tu asaini kwa kidole tena mara ya pili.
Alisema
jambo hilo linawatatiza wabunge kwa kuwa wanajiona kama wanachukuliwa
kama wanafunzi kwa kufuatiliwa kwani hata kwenye benki wafanyakazi
hawasaini na kufuatiliwa kama ilivyo kwa wabunge hao.
Alifafanua
kuwa kabla ya kuomba mwongozo huo, alifanya utafiti kwenye benki
mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao nao wana utaratibu
kama huo wa Bunge lakini hakuna mahali wanapotakiwa kusaini kwa vidole
mara mbili.
Kwa
upande wake, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson wakati akijibu mwongozo huo
alisema kutokana na namna wabunge hao walivyopokea suala hilo, pamoja na
kwamba kikanuni jambo hilo halikutakiwa kuombewa mwongozo bado
litaangaliwa.
“Hata
hivyo nifafanue kuwa kusaini mara mbili lengo lake si kuwafanya wabunge
wanafunzi, ila lengo ni kutaka kujua nani wapo humu ndani (bungeni),” alisema Dk Ackson.
0 comments:
Post a Comment