Kambi ya upinzani imeliibua upya bungeni sakata la Escrow, Richmond na
umiliki wa kampuni ya IPTL, huku ikihoji sababu za Rais John Magufuli
kutoheshimu maazimio ya Bunge ya kumwajibisha Sospeter Muhongo, badala
yake kumteua tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Hoja hizo
ziliibuliwa na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika wakati
akiwasilisha maoni ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/16 na
makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17.
Muhongo
alikuwa akiiongoza wizara hiyo wakati kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya
Sh300 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa
kuhifadhi fedha za malipo umeme kusubiri kumalizika kwa mzozo wa
kimkataba baina ya kampuni ya IPTL, inayozalisha umeme na Shirika la
Umeme (Tanesco).
Bunge lilimuona Profesa Muhongo kuwa alishindwa
kuwajibika na kusababisha Serikali kupoteza mapato.
Profesa Muhongo
alilazimika kujiuzulu wadhifa huo saa chache kabla ya Rais wa Serikali
ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutangaza baraza jipya.
Hata
hivyo, Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lilimsafisha na kashfa hiyo
iliyohusisha malipo yaliyofanywa kwa mawaziri, majaji, wabunge na
watumishi waandamizi wa umma.
Jana, Mnyika, ambaye ni mbunge wa
Kibamba (Chadema), alirejea maazimio ya Bunge la Kumi akisema
lilishafanya maamuzi kuhusiana na mikataba ambayo Serikali inaingia na
kampuni mbalimbali, hasa kwenye sekta ya nishati na madini.
“Katika
maazimio ya Bunge kuhusiana na fedha, ufisadi uliofanyika katika
akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa IPTL yanayohusu sekta ya nishati
na madini, bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake,” alisema Mnyika.
Akinukuu Azimio Namba 2, Mnyika alisema liliagiza kwamba Serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha inazolipa kwa kampuni
hiyo binafsi.
Alisema kambi hiyo inasikitika kuona kwamba mbali
ya Serikali kushindwa kununua, bado inaendelea kulipia gharama za
uwekezaji na hivyo kuendelea kukiukwa kwa azimio hilo.
Akizungumzia
azimio la saba linalohusu kuwajibishwa kwa mawaziri na watendaji wakuu
wa wizara na bodi ya Tanesco, Mnyika alisema Profesa Muhongo naye
aliwajibishwa kwa uteuzi wake kutenguliwa, lakini Rais Magufuli amemteua
tena kuongoza wizara hiyo.
“Rais bila ya kujali nini Bunge
lilishaazimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya azimio
hilo, akamteua Muhongo kuendelea kuiongoza wizara hii. Kambi ya upinzani
inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge na ni fedheha binafsi
kwake,” alisema.
Alisema kambi ya upinzani imelazimika kunukuu
maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa
kutekeleza maazimio ya Bunge na badala yake mikataba hiyo inaendelea
kutekelezwa kama ilivyoingiwa.
“Mfano mzuri ni Tanesco kuendelea
kuilipa IPTL fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi
kuliondolea shirika hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwa
kuwa haliwezi kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kusambaza umeme
kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha,” alisema.
0 comments:
Post a Comment