Wabunge wamemcharukia Waziri wa Habari, Nape Nnauye kwamba aliwahi kuwaita mawaziri
wa Serikali iliyopita mizigo, lakini yeye amezuia matangazo ya moja kwa
moja ya Bunge, ili wananchi washindwe kumpima kama ni mzigo au lumbesa.
Hayo yalijitokeza jana wakati wabunge walipochangia hotuba ya bajeti ya
Wizara ya Habari kwa mwaka 2016/2017, iliyowasilishwa bungeni na Waziri
Nape.
Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) alieleza kushangazwa
na hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhimiza wananchi kudai risiti
wanaponunua bidhaa, lakini haitaki wananchi waone inavyopanga matumizi
yake.
Alisema Nape akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliwaita
baadhi ya mawaziri ni mizigo, lakini amepewa wizara hiyo amezuia
mijadala ya wazi ambayo ingesaidia wananchi kumpima.
“Nilipoona amepewa
wizara ya habari nikajua ataruhusu mijadala ya wazi ili tumuone yeye
kuwa hatakuwa mzigo, lakini yeye akawa lumbesa. Hilo amelizuia kwa hiyo
tunashindwa kumpima,” alisema.
Alisema waziri huyo hawezi kukwepa lawama
ya hicho kinachoendelea cha kuzuia matangazo ya Bunge, kwa vile
wanaopiga picha na kuhariri taarifa zinazorushwa ni watumishi wa TBC.
Udhibiti wa Bunge
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act-Wazalendo),
alisema kuwa wabunge wote waliopinga Bunge kutoonyeshwa ‘live’ na
kusababisha mtafaruku bungeni, wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya
Bunge.
“Wabunge hapa tulisimama tukapinga na wapo waliounga mkono,
lakini kiti chako kimetuita wabunge wote tuliopinga kauli ya Serikali
kwenye kamati ya maadili. Jana mimi nimepata barua,” alisema Zitto.
“Kwamba mnatubana kusema. Mnazuia Bunge lisionekane. Hata kutoa maoni
ndani ya Bunge tunakwenda kuhojiwa? TBC ni chombo cha umma, siyo chombo
cha Serikali, inaendeshwa kwa kodi za wananchi,” alisisitiza.
Baada ya
mchango huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema si kweli wabunge hao
wanahojiwa kutokana na michango yao, bali wanahojiwa kutokana na mambo
waliyoyafanya kwa kutotii maagizo ya kiti wakati wa mjadala wa ‘Bunge
Live’.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliunga
mkono hoja ya Zitto ya kuifanya TBC iendeshwe kama inavyoendeshwa BBC
kwa kupewa leseni maalumu.
Pia, aliitaka Serikali kupeleka muswada
bungeni utakaowabana wamiliki wa vyombo vya habari kuwa na mikataba na
waandishi wanaowaandikia, pia, akadai baadhi ya vyombo haviwalipi
waandishi wake.
Hata hivyo Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Marwa (CCM)
alitetea uamuzi wa Serikali kuondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge,
akisema wabunge wanaodai hilo ni wale waliokuwa wakiuza sura.
Katika
hatua nyingine, Waitara alisema kitendo cha Nape kuwaalika wabunge
kwenye muziki, baada ya bajeti yake kupita ilikuwa ni kuwahonga.
Juzi
jioni wakati akitoa matangazo kabla ya kuahirisha Bunge, Naibu Spika
alisema baada ya kupitisha bajeti ya Wizara ya Habari, wanamuziki
Diamond Plutnum na King Kiki watatumbuiza katika viwanja vya Bunge.
“Mnaposema mnabana matumizi hao wanamuziki wameletwa kwa gharama za
nani,” alihoji mbunge huyo.
“Wabunge wote ambao wataenda katika hiyo
miziki ili kuunga mkono habari ya Nape mtakuwa mmekula rushwa,”
alisisitiza Waitara, kauli ambayo ilimfanya Naibu Spika, Dk Tulia
kufafanua, akisema suala hilo lilitangazwa bungeni kama mengine,
lisiingizwe kosa la jina la rushwa.
Upinzani na udikteta
Msemaji mkuu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Habari, Utamaduni,
Wasanii na Michezo, Joseph Mbilinyi, alisema kitendo cha Serikali
kuminya uhuru wa habari ni kuelekea kwenye udikteta.
“Kana kwamba
haitoshi, Serikali sasa imezuia Televisheni ya Umma, inayoendeshwa na
kodi ya wananchi (TBC1) kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mijadala
inayofanyika bungeni. Dalili hizi siyo njema kwa ukuaji wa demokrasia na
uhuru wa habari hapa nchini na zinatoa taswira ya utawala wa
ki-dikteta,” alisisitiza.
“Tunaitaka Serikali kuliomba radhi Bunge
hili, kwa kosa la kuminya uhuru wa habari kinyume na Katiba na kuviacha
vyombo vya habari hususan vya umma kufanya kazi zao za kuhabarisha umma
kwa uhuru,” alisema.
0 comments:
Post a Comment