Joseph Lomayani (18), ni dereva mwingine wa pikipiki kukamatwa kwa tuhuma za kuwarushia bomu waumini waliokusanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti jijini hapa jumapili ya Mei 5, mwaka huu.
Wa kwanza kukamatwa alikuwa Victor Ambroce Kalisti (20). Wote kwa pamoja walikuwa na kituo (kijiwe) cha kufanyia biashara zao za bodaboda eneo la kwa Mrombo nje kidogo
ya jiji la Arusha, barabara iendayo Simanjiro, mkoani Manyara.
Joseph ni mtoto wa watatu kuzaliwa kati ya watoto saba wa Lomayani Sautie Metivani (47) na kati yao wasichana ni watatu na wavulana ni wanne. Mkewe ametangulia siku nyingi mbele ya haki.
Babake anamwelezea Joseph kuwa alimaliza darasa la saba Shule ya Msingi Terrat mwaka 2010, lakini kutokana na umri aliokuwa nao kuwa mkubwa mwaka uliofuata alipata nafasi ya kuanza masomo ya sekondari katika shule ya watu wazima kupitia mpango wa Memkwa.
Hata hivyo, anasema kutokana na mila za kwao Wamasai, alimpeleka mtoto wake kutahiri hali ambayo ilimfanya ashindwe kuendelea na masomo yake kwa mwaka huo kutokana na kutumia muda mwingi kwa shughuli za utamaduni wa kutahiri na pia shule kuwa mbali na nyumbani kwao.
Hata hivyo, anasema alimtafutia shule nyingine ya aina kama hiyo ambayo ipo eneo la Olasiti.
Alipoanza hiyo shule, Lomayani anasema, mtoto wake aliwakuta wenzake wapo mbali kimasomo. Akashindwe kumudu.
“Alipoanza hiyo shule aliwakuta wenzie wapo mbali, akaniambia, baba, kwenda kusoma tena pale kichwa yangu haikamati, hivyo, sitaweza kuendelea tena na hiyo shule, nitakuwa kama vile ninaswagwa tu,” ananukuu maelezo ya mtoto wake.
“Baada ya hapo, nilimtafutia kazi ya ufundi wa karakana ya magari. Ilikuwa mwaka huo huo wa 2012 na gereji hiyo ipo kule kwa Mrombo inayomilikiwa na Olii,” anasema.
Lakini anasema baadaye mwanaye aliugua na kushindwa kuendelea na mafunzo ya kazi hiyo, hivyo akawa yupo tu akiendelea na shughuli za hapa na pale nyumbani kwake.
Kuendelea kukaa nyumbani bure kulimchosha, na kama wiki moja kabla ya mlipuko wa bomu kanisani, alikuwa amepata pikipiki ya Lomyaki Sindiyo, hivyo akawa anaiendesha kwa makubaliano ya kumlipa fedha kila wiki.
“Alianza kuendesha pikipiki hiyo kama wiki moja iliyopita, na wakati yupo pale kijiweni siku ya Jumapili, Victor Ambroce alimwachia simu yake amkamchajie na yeye Victor alikuwa amepata mteja na sijui huyo mteja alikuwa anampeleka wapi,” anadai.
Lomayani anadai kuwa majira ya saa tano hivi asubuhi, alimpigia mwanaye simu akimuuliza yupo wapi naye akamjibu kuwa yupo kwa Mrombo.
“Nilimwambia njoo nyumbani uchukue hela ukatulee mboga na baada ya kuileta (Joseph) akaendelea na shughuli zake,” anadai na kuongeza, mlipuko wa bomu kanisani hapo aliusikia majira ya saa mchana kupitia redio moja ya kijamii ya mkoani hapa.
KUKAMATWA KWA JOSEPH:
Anasema ilikuwa saa 12 asubuhi ya Jumatatu iliyopita, askari polisi walifika pale nyumbani kwake eneo la Mrombo CCM, na kumuuliza: “Tunamhitaji Joseph kwani ana simu ya Victor aliyoichukua.”
“Wakaenda kumwamsha Joseph anakolala na kumuuliza simu ya Victor ipo wapi naye akawawaambia ameiacha dukani kwa George huko huko kwa Mrombo CCM anasema na kuongeza:
“Polisi walienda naye kuichukua ile simu na wakamchukua na George pia na kuwapeleka kituoni na baada ya hapo kulingana na mimi ninavyomjua mtoto wangu hanaga tabia mbaya kabisa na wanaweza kuchunguza hilo.”
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, George ni mmoja wa watuhumiwa wa tukio hilo.
“Mimi nasikitika sana mtoto wangu kusingiziwa kuwa ni mmoja wa watu wanaohusishwa kurusha bomu kanisani. Maaskari hapo hawakuwa hawajatenda vyema.
“Mtoto wangu anaenda kutoswa bila sababu, nikiwa mzazi wake nakiri kabisa huyo mtoto hajafanya suala hilo,” anasema.
Katika tukio hilo la bomu watu watatu walifariki dunia huku wengine zaidi ya 67 wakijeruhiwa, baadhi yao vibaya.
Wengine wamehamishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
0 comments:
Post a Comment