Uchunguzi uliofanywa na ripota wetu, umebaini kuwa imani za kishirikina na tukio la trafiki aliyemgonga mwendesha bodaboda na kumvunja mguu, ndiyo asili ya vurugu hizo.
Habari kutoka chanzo chetu wilayani Masasi zinasema, kilichosababisha vurugu ni askari wa usalama barabarani aliyemgonga dereva wa bodaboda na kumvunja mguu kisha polisi wa Kituo cha Polisi cha Sokoni kukataa kutoa PF 3 ili majeruhi akatibiwe.
Chanzo chetu kilisema, baada ya tukio hilo, madereva wa bodaboda waliungana na wa bajaj kwenda kwa kamanda wa polisi wa wilaya lakini hawakuruhusiwa kumuona.
“Katikati ya maandamano ndipo watu hao wakaibuka kudai haki kwa jumla, ikiwemo gesi kutosafirishwa kutoka Mtwara. Kabla ya hapo Masasi hakukuwahi kuwa na maandamano ya kupinga gesi kusafirishwa,” kilisema chanzo chetu.
UHARIBIFU WA MALI MASASI
Mali zilizoharibiwa ni pamoja na nyumba za wabunge, Mariam Kasembe (Masasi Mjini), Anna Abdallah (Viti Maalum), majengo ya Mahakama ya Mwanzo, Ofisi ya CCM ya Wilaya, Ofisi za Halmashauri ya Wilaya, Kituo cha Polisi Sokoni na magari 12.
Nyumba ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa haikosogelewa kutokana na ulinzi mkali uliowekwa na polisi japokuwa haipo mbali na ofisi zilizounguzwa na waandamanaji.
MTWARA NA UCHAWI
Kata ya Chikongola, Manispaa ya Mtwara Mikindani, wananchi waliizingira nyumba ya diwani wa kata hiyo, Mohammedi Chehako kwa madai ya kuwahifadhi wachawi ndani ya nyumba yake.
Chanzo chetu kilieleza: “Wananchi walikuta ungo ukiwa na tunguri ndani, wakadai ile ni ndege ya wachawi ambayo huitumia kusafiria angani.
“Diwani kukata mzizi wa fitina, aliuchoma moto ule ungo pamoja na tunguri lililokuwemo lakini wananchi waliendelea kusisitiza wapewe wachawi waliodondoka na ungo na kuhifadhiwa ndani ya nyumba ya diwani.
“Kadiri muda ulivyosogea ndivyo na watu walivyoongezeka, hali ikawa mbaya nyumbani kwa diwani, kwa hiyo Diwani Chehako akapiga simu polisi kuomba msaada.
“Polisi walipofika pale nyumbani kwa diwani waliwasihi wananchi kutawanyika kwa kuwa ungo na tunguri vilishachomwa moto mbele yao.
“Yale mabomu ya machozi yakaibua vurugu kubwa, kwa hasira wananchi wa Mtwara wakaamua kukumbushia na sakata la gesi, maandamano yakawa makubwa zaidi, lakini ukweli chanzo chake ni ule ungo na tunguri nyumbani kwa diwani.”
DIWANI ANENA
Akisimulia mkasa huo, Diwani Chehako alibainisha kuwa ni kawaida yake kuamka alfajiri kwa ajili ya sala ya asubuhi, lakini asubuhi ya tukio alishindwa kufanya hivyo, japo hakuhisi chochote.
“Ilipofika saa 12 asubuhi nikaanza kusikia watu wakishangaa kitu nje ya nyumba yangu, nilipotoka nikakuta ungo na tunguri ndani yake. Mara wakaja vijana wawili na pikipiki wakachukua ule ungo na kukimbia nao.
“Nikawatuma vijana wawafuate waurudishe, walifanikiwa na ungo ule ulirejeshwa nyumbani hapa na ndipo nilipouteketeza kwa moto, ” alisema.
“Wananchi hao wenye vurugu hawakuishia hapo, wakavamia mahakama ya mwanzo kwa kupiga mawe jengo hilo na kuvuja vioo kisha kuchoma moto matenki ya maji.
“Ilibidi polisi wafanye kazi ya ziada ya kuondoa majalada yote yaliyokuwa ndani ya mahakama hiyo.
“Vurugu zilipamba moto baada ya vijana hao kuanza kuimba, ‘Tunataka gesi yetu’, hivyo kuonekana wazi kuwa wapo walioingia katika vurugu kwa kufuata mkumbo bila kujua chanzo wakafanya maandamano ya hasira kudai gesi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki alisema gari moja la polisi lenye namba PT 1421 limevunjwa kioo cha mbele kwa mawe.
Hata hivyo, hakutaka kuzungumza zaidi badala yake alisema kwa kifupi: “Ndugu mwandishi hali halisi unajionea mwenyewe wala sina cha kuongea.”
Kwa kweli poleni Wana mtwara hayo ndiyo majaribu ila mungu atayasimamia amani itakuwepo poleni
ReplyDelete