Alitoa kauli hiyo jana jijini hapa baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua mradi wa mabasi hayo.
Mwinyi ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee Ruksa, alianza ziara hiyo
kwa kupanda basi la mwendo kasi katika eneo la Morocco, Kinondoni na
kwenda hadi Gerezani Kariakoo. Baadaye alielekea Kivukoni ambako
alihitimishia ziara yake hiyo.
Kwa mujibu wa Mwinyi, usafiri huo ni mzuri na mabasi husika yana
mazingira bora yanayomfanya abiria afike katika eneo alilokusudia kwa
wakati.
“Usafiri huu ni mkombozi kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwani
kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida ya usafiri unaosababishwa na
msongamano wa magari katika maeneo ya mjini.
“Leo nimejionea ujuzi na uroda kama mnavyosema, kwa kweli nimefurahia
mazingira ya mabasi haya kwa sababu ni bora na hayana usumbufu.
“Hata msongamano wa abiria kama ilivyokuwa zamani haupo, huu ni usafiri mzuri sana,” alisema Mwinyi.
Kutokana na hali hiyo, aliutaka uongozi wa mabasi hayo (DART),
uangalie uwezekano wa kuleta mabasi yenye ghorofa ili kuwawezesha abiria
kuburudishwa na mazingira ya Jiji la Dar es Salaam.
“Nadhani ni vema pia wakaleta mabasi ya ghorofa ambayo yapo wazi juu ili kuwapa nafasi abiria kutalii mji wetu huu,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuheshimu njia za mabasi hayo ili kuepusha ajali zisizokuwa za ulazima.
“Najua kuna changamoto mbalimbali kama ile ya kunyang’anyana abiria
ambapo wenye daladala wanataka na bodaboda nao wanataka. Yote hayo ni
sawa, lakini mabasi haya yanatakiwa kuachiwa uhuru katika njia zake ili
yafanye kazi kama inavyotakiwa.
“Tumeona msongamano wa magari umepungua sasa, lakini nadhani kuwekwe
mfumo maalumu ambao mwisho wa mabasi yaendayo kasi ndio uwe mwanzo wa
usafiri binafsi,” alisema.
Wakati Mwinyi akisema hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa DART, David
Mgwassa, alisema wananchi wameanza kuelimika juu ya matumizi ya barabara
za mabasi yaendayo kasi.
Alisema mazingira hayo ya kuelimika yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazotokea katika maeneo hayo.
0 comments:
Post a Comment