Tuesday, April 19, 2016

Akiona Chamoto Ukweni Akigombea Maiti ya Mkewe...!

MARA

Mkazi wa Kijiji cha Mwikoro, Kata ya Buruma, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, aliyekuwa akiishi Yombo Kilakala, Dar, Kisika Wambura Mtake (44), amekiona cha moto kutoka kwa mashemeji zake ukweni baada ya kujaribu kuuchukua kwa nguvu mwili wa marehemu mkewe, Ester Mgaya Makoni (41) aliyefariki dunia, Dar ili akauzike nyumbani kwake kijijini Mwikoro, Uwazi lina kila kitu.

Walioshuhudia tukio hilo la aina yake lililotokea Aprili 12, mwaka huu katika Kijiji cha Nyamikoma, Kata ya Kyanyari wilayani Butiama nyumbani kwa mzee Makoni Isandeko ambaye ni baba mzazi wa marehemu walisema kuwa, mapema siku hiyo ya tukio Mtake alifika ukweni hapo akiwa na msafara wa waombolezaji wa marehemu mkewe aliyefariki dunia Aprili 8, mwaka huu nyumbani kwake Yombo Kilakala. 


“Mara baada ya msafara wa marehemu kufika kwa mzee Isandeko, Mtake aliwaeleza ndugu wa mkewe kwamba ameamua kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka kijijini kwake Mwikoro ili akamzike huko lakini mashemeji zake walikuja juu na kugoma kuutoa mwili huo na ndipo vurugu zilipoanza.

“Mashemeji zake walidai kuwa ni lazima dada yao azikwe nyumbani hapo kwa madai kuwa, tangu jamaa huyo aanze kuishi naye mwaka 1992 hakuwahi kumtolea mahari inayomhalalisha kuwa mke wake,”
kilisema chanzo.

Mashuhuda walifafanua kuwa, baada ya ndugu wa marehemu kuamua azikwe nyumbani kwao, mumewe alikuja juu na kusababisha vurugu zilizomfanya kutimua mbio kutoka msibani hapo na kutokomea kabla ya wazee na uongozi wa serikali ya kijiji kuingilia kati na kusuluhisha.

Ndugu hao wa marehemu walipoulizwa na gazeti hili kisa cha vurugu na kumpiga mkwe wao walisema hawakumpiga isipokuwa walikuwa na nia ya kumpiga lakini wakasuluhishwa.

Mara baada ya suluhu hiyo kupita mume wa marehemu aliomba alipe mahari ya ng’ombe watatu ili auchukue mwili wa mkewe akauzike kijijini kwao ambako pia wamezikwa watoto wake wawili aliozaa na marehemu, lakini ndugu hao waligoma kupokea na kuamua kumzika ndugu yao, Aprili 13, mwaka huu. 

Mtake aliliambia Uwazi huku akitokwa machozi mara baada ya mazishi ya mkewe kuwa, wakwe zake hawakumtendea haki kuuzika mwili wa mkewe nyumbani kwao badala ya kwake kwa madai kuwa ameshatoa kishika uchumba cha fedha na mbuzi wawili na pia aligharamia kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Dar mpaka Mara ambapo alitumia shilingi 2,500,000.

CREDIT: GPL
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger