Viongozi
wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu
Mkuu, Vincent Mashinji jana walijifungia kutwa nzima kujadili hatua za
kuchukua dhidi ya kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na
mikutano ya chama hicho ya kisiasa.
Tangu
asubuhi jana, viongozi hao walikuwa na kikao katika ukumbi wa Mandela,
hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza na wakati wa mapumziko mafupi saa
kumi jioni, Mbowe alisema chama hicho kitatoa kauli rasmi leo baada ya
kikao kingine kilichotarajiwa kufanyika jana usiku.
“Tutatoa
kauli rasmi kesho (leo), baada ya vikao. Ninachoweza kuthibitisha ni
kwamba tunaendelea kushauriana njia sahihi ya kuchukua,” alisema Mbowe.
Juni
7, mwaka huu polisi ilitangaza kupiga marufuku kwa muda usiojulikana
maandamano na mikutano yote ya kisiasa kwa kile kilichodaiwa ni taarifa
za kiintelijensia za kuwapo tishio la kiusalama na kuwa wanakwenda
kushawishi wananchi kuipinga Serikali.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema miongoni mwa
masuala ya msingi yaliyokuwa yakijadiliwa jana ni pamoja namna bora na
sahihi ya kuendelea kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya
hadhara bila vikwazo.
“Katika hili, tutatumia mbinu zote kuanzia zile za kisiasa, kisheria na kijamii,” alisema Mwalimu.
Ingawa
hakuna kiongozi wa Chadema aliyekuwa tayari kukanusha wala kuthibitisha
kilichosababisha vikao vyao vya jana kuchukua muda mrefu na mvutano
miongoni mwa wajumbe kuhusu hatua za kuchukua.
Akizungumza
kwa sharti la kutotajwa jina , mmoja wa wajumbe alisema baadhi ya
wajumbe walitaka chama hicho kuendelea na ratiba yake ya mikutano ya
hadhara bila kujali zuio la polisi walilosema halina misingi ya
kisheria, isipokuwa jeshi hilo linatumika kisiasa kuhujumu vyama vya
upinzani kwa maslahi ya chama tawala cha CCM.
“Baadhi
yetu, nikiwamo mimi tulitaka chama kutumia mkondo wa kisheria kupinga
zuio hilo badala ya kuendelea kutunishiana misuli na polisi,” alisema mtoa taarifa wetu.
Baadhi
ya mawakili wa Chadema, akiwamo Paul Kipeja, John Mallya, jana
walionekana katika viunga vya hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza katika
kilichoelezwa na vyanzo vyetu kuwa ni maandalizi ya chama hicho kufungua
shauri mahakamani dhidi ya Jeshi la Polisi.
0 comments:
Post a Comment