Mwanamuziki wa kizazi kipya Diamond Platnum, ameeleza kushangazwa kwake na ukimya wa Serikali akisema unaashiria kutotambua tuzo ya kimataifa aliyoipata hivi karibuni kupitia MTV.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, nyota huyo alidai kuwa hali hiyo inachangia kuwakatisha tamaa wasanii, huku Baraza la Sanaa la Taifa, (Basata) likieleza kuwa haikuwa na taarifa za siku rasmi ya kurejea Diamond ndiyo sababu wameshindwa kushiriki.
Diamond anayetamba na wimbo wa Nana, wiki iliyopita alinyakua Tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Afrika mjini Durban, Afrika Kusini na ambayo ilishindaniwa pia na Mr Flavor wa Nigeria, Micassa wa Afrika Kusini, To Fun wa Togo na Big Nuz wa Afrika Kusini.
Alisema kuwa licha ya Watanzania wengi kumpongeza kwa mafanikio hayo, hakuna kiongozi wala taasisi ya Serikali iliyozungumza chochote kuhusu ushindi huo uliopatikana kwa mara ya kwanza nchini Tanzania.
“Nilitarajia taasisi za Serikali zinazohusika na sanaa, zingekuwa mstari wa mbele kuonyesha furaha kutokana na mafanikio haya, lakini mpaka leo hakuna niliyemsikia akizungumzia, wakati ni tuzo kubwa na imeleta heshima kubwa kwa Watanzania,”alisema Diamond.
Kwa upande wake, Meneja wa Msanii huyo Salam Sharaf alisema wakati umefika wa Serikali kugeukia nyanja zingine za burudani badala ya kuweka mkazo kwenye mpira pekee.
“Sidhani kama timu ya taifa ikishinda watakosekana viongozi wa Serikali kwenda kuipokea, ushindi wa Diamond ni heshima kwa taifa na taarifa zilisambaa kila kona juu ya ujio wetu, lakini hakuna aliyetutafuta mpaka leo,”alisema.
Siku chache baada ya kushinda tuzo hiyo jina la Diamond limeonekana kung’ara kwenye tuzo za AFRIMMA zinazotolewa nchini Marekani akiwa ametajwa kuwania vipengele saba.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza alisema hawakuwa na taarifa za siku rasmi ya kurejea Diamond, ndiyo maana hawakuwepo kwenye mapokezi yake.
“Licha ya kuwa wakati anaondoka hakusema chochote, lakini Basata hatuna sababu ya kumtelekeza. Tungekuwa na taarifa muda gani anawasili tungekuwepo uwanja wa ndege kumpokea, maana ameleta heshima kubwa kwa taifa. Nampongeza sana kwa mafanikio hayo.
Tunafahamu msanii akitoka nje haendi kama mtu binafsi, bali anakwenda kuiwakilisha nchi basi tuwe tunapeana taarifa,”alisema.
Akizungumzia tuzo za AFRIMMA juzi, Diamond alisema ataendelea kuwa mwema na kuufanya muziki wake kama kazi kwani umetambulika kimataifa.
“Nawashukuru kutambua kazi yangu, nadhani sasa watu watajua kwamba kuwania vipengele hivi vyote ina maana gani,” alisema na kuongeza:
“Namshukuru Mungu kwa kuendelea kubariki kazi yangu. Siku zote nitaendelea kuwa mwema na kuhakikisha nafanya kazi kwa bidii kwani vipengele sita katika tuzo za AFRIMMA si kitu kidogo.”
Wakati huohuo msanii huyo alijibu tuhuma zinazoendelea kuenezwa dhidi yake kufuatia picha na maelezo aliyoweka kwenye mtandao wa Instagram vinayodaiwa kumdhalilisha mwanamitindo Jokate Mwegelo.
Picha hiyo ambayo ilikuwa ikimuonesha Jokate akicheza wimbo wa Diamond, ilisindikizwa na maneno “`..na bado, mtanyooka tu”, ilipokewa kwa hisia tofauti na mashabiki pamoja na Jokate mwenyewe ambaye alimjibu nyota huyo akisema:
“Lakini wasiwasi wangu ni kwamba huenda anafanya vile kama ilivyo kawaida yake kudhalilisha wanawake aliotoka nao ili waonekane hawana thamani kwa sababu hawako naye.”
Hata hivyo, Diamond alikanusha madai hayo ya udhalilishaji akisema:
“Kimsingi sikueleweka, lengo kuu lilikuwa ni kupeleka ujumbe kwa wapinzani wa jadi, ambao kila siku wamekuwa wagumu kuuelewa muziki wangu ambao kila kukicha unavuka mipaka. Labda kosa langu ni kutumia picha ya Jokate ambaye mimi nilimchukulia kama shabiki, anayejulikana na wengi, ili kufikisha ujumbe kwa urahisi.”
0 comments:
Post a Comment