Diwani wa Kata ya Mindu, Manispaa ya Morogoro amefukuzwa kwenye mkutano wa hadhara na wananchi kwa madai ya kutokuwa na imani naye.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya kuunda kamati ya watu 10 ya kwenda Dodoma kupeleka kero kwa Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuhusu jengo la shule lililobomoka na Manispaa ya Morogoro imeshindwa kulikarabati.
Wananchi hao wanaulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kushindwa kuwasaidia ufumbuzi wa jengo la Shule ya Msingi Lugala, lililoanguka na kusababisha wanafunzi zaidi ya 80 kukikosa masomo kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Wakizungumza kabla ya kuanza kwa mkutano huo juzi shuleni hapo, wananchi hao walianza kwa kumtaka Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Sanga Mkulago amtimue Diwani Hamis Msasa kwa madai kuwa ni msaliti.
Ameshindwa kutoa msaada katika vikao vya maendeleo vya baraza la madiwani tangu achaguliwe.
Wakazi Joseph Zambi na Mbena Chunda, walidai kuwa diwani huyo ameshindwa kuzisemea kero za mtaa huo barazani ili zipatiwe ufumbuzi ikiwamo ya Shule ya Lugala.
“Tuna kero nyingi na hazijatatuliwa na viongozi wetu, lakini kubwa zaidi ni jengo lililojengwa chini ya kiwango kuanguka na wanafunzi hawajaenda shuleni kwa mwezi mmoja,” alisema Zambi.
Baada ya kuzongwa na wananchi wakimtaka aondoke mkutanoni hapo, Diwani Msasa aliamua kuondoka.
“Niacheni naondoka kwa hiyari yangu na hakuna haja ya kunishika na sipendi mnisukume,” alisema Msasa huku akiondoka.
Ofisa wa Serikali ya Mtaa wa Lugala, Makame Kai aliwaeleza wakazi hao lengo la mkutano huo kuwa ni kuunda kamati ya watu 10 akiwamo mwenyekiti wa serikali ya mtaa na wengine 9 kwenda kwa Waziri Mkuu Dodoma kupeleka kero zinazowakabili.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment