Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilago amewatuhumu baadhi ya wanasiasa kushiriki katika mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ili kupata ushindi wakati wa uchaguzi.
Akichangia katika semina ya nafasi ya wabunge kukuza na kuimarisha usawa wa watu wenye ulemavu iliyofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa jana, Bilago alisema wakati wa uchaguzi ndiyo albino wamekuwa wakipata shida.
“Wanasiasa ndiyo mnawaua albino wakati wa uchaguzi, lakini unapomalizika (uchaguzi) walemavu hao wanaishi salama. Kwa nini Serikali hamuwanyongi hawa wanaowaua albino wakati wapo wengi wamekamatwa na sijasikia hata mmoja aliyenyongwa,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Dk Abdallah Possi alisema jambo la msingi siyo kuwanyonga kikubwa ni kutoa elimu ili kubadili mtazamo wa jamii kuhusu albino. “Katika uchaguzi wa mwaka jana nilianza kuogopa kuhusu mauaji ya albino lakini hayakutokea kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi zilizopita, lakini hiyo haimaanishi tusipambane na mauaji ya albino kwani hata kidole cha mtu kikikatwa ni athari,” alisema.
Aliwataka wabunge kutoa elimu kwenye maeneo wanayotoka ili kubadili mtazamo wa watu.Alisema tangu afike bungeni hajawahi kujibu swali la watu wenye ulemavu lililoulizwa na wabunge wasio walemavu.
Pia, wabunge wengine waliitaka Ofisi ya Bunge kubadilisha miundombinu yake ili iwe rafiki kwa walemavu na kutolea mfano jengo la utawala lenye ghorofa nne lakini hakuna lifti hivyo kuwafanya wabunge walemavu kushindwa kwenda kwenye baadhi ya ofisi kupata huduma.
Hali hiyo walisema imekuwa ikiwafanya wabunge wenye ulemavu kuandika vikaratasi na kuwaomba watu wawapeleke katika ofisi wanazohitaji huduma.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Ligora (CCM) alilitaka Bunge kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kupata huduma kwa haraka.
“Tuanze bungeni kuweka mazingira rafiki kwa walemavu , leo mbunge mlemavu anakaa miaka 15 hajapanda ghorofa la utawala kwenda ofisi ya fedha kushughulikia malipo yake, mbona mambo mengine mnaweza kuweka kama mfumo wa kuweka dole kuingia ndani ya Bunge,” alisema Ligora.
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Nagenjwa Kaboyoga alihoji Ofisi ya Bunge kushindwa kuajiri watumishi wenye ulemavu.
0 comments:
Post a Comment