Ofisi ya Waziri Mkuu
itatumia usafiri wa bajaji na bodaboda kuendesha shughuli zake kuanzia
mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017 ikiwa ni mkakati wa kubana matumizi wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Mpango
huo umo kwenye hotuba ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu
iliyosomwa jana bungeni na Kassim Majaliwa, na baadaye kusifiwa na
mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, Mohamed Mchengerwa
wakati akisoma maoni ya kamati kuhusu bajeti hiyo.
Wizara iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni ya Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu.
Akiwasilisha
maoni ya kamati hiyo, Mchengerwa alisema uamuzi wa aina hiyo unaendana
na dhana ya kubana matumizi ya fedha wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Hata
hivyo, hotuba iliyosomwa na Waziri Majaliwa haijaeleza pikipiki hizo za
magurumu mawili na matatu zitatumiwa na watumishi wa kada gani.
Serikali
ya Awamu ya Tano imekuwa kwenye mkakati mkali wa kubana matumizi yasiyo
ya lazima na tayari Rais John Magufuli ametangaza kuwa kuanzia mwaka
mpya wa fedha hakuna mtumishi wa umma atakayelipwa zaidi ya Sh15
milioni, huku akifuta sherehe za maadhimisho ya siku za kitaifa,
zikiwamo za Muungano na Uhuru.
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC)
Katika
maoni yake, kamati hiyo imeitaka Serikali kutoa tamko kuhusu maandalizi
na utekelezaji wa mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Pia
kamati hiyo ilitaka Nec kuweka utaratibu mpya wa ratiba ya upigaji kura
ili chaguzi zote za rais, wabunge, madiwani na viongozi wa Serikali za
mitaa zifanyike kwa wakati mmoja.
“Hii itasaidia kupunguza gharama zinazotumika kwa nyakati mbili tofauti pamoja na kusaidia kupunguza mtikisiko wa amani nchini,”alisema.
Uchaguzi
wa viongozi wa Serikali za mitaa hutangulia takriban mwaka mmoja kabla
ya Uchaguzi Mkuu ambao huhusisha uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.
0 comments:
Post a Comment