SHAHIDI, Pamphilly Mholeli, katika kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake ya kukutwa na silaha
kinyume cha sheria, amedai mahakamani kwamba, siku ya tukio aliwakamata
mshtakiwa pili hadi wa nne wakiwa na begi lenye silaha wakati askofu
huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Amedai kabla ya kulikagua begi walitilia mashaka ujio wa mshtakiwa wa
pili hadi wa nne nje ya wodi namba 113 ya hospitali ya TMJ, jijini Dar
es Salaam saa 9:00 alfajiri wakati Askofu Gwajima alipokuwa amelazwa
huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi na baada ya kulikagua begi
walilokuwa wamebeba walikuta bastola moja, risasi 17 na vitu vingine.
Ushahidi huo ulitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian
Mkeha, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
jijini Dar es Salaam.
Akiongozwa na mawakili wa serikali waandamizi, Shadrack Kimaro na
Jackline Nyantori, shahidi huyo alidai kuwa, siku ya tukio akikuwa ofisa
wa polisi wa zamu kwa mkoa wa kipolisi Kinondoni, usiku wa manane
alipokea agizo kutoka kwa bosi wake Costantine Masare kwamba kuna kundi
kubwa la watu limekusanyika katika Hospitali ya TMJ.
“Nilikwenda eneo la tukio na tuliwatawa wale watu, lakini tulipoikwenda
kuangalia lindo la polisi nje ya wodi namba 113 ghorofa ya kwanza
aliyokuwa amelazwa Gwajima, tuliwakuta washtakiwa pamoja na askari
aliyekuwa akilinda, nilipowauliza washtakiwa wanahitaji nini muda ule na
begi lao, walijieleza kwamba walikwenda kumuona mgonjwa”alidai na
kuongeza:
“Nilishangaa saa 9:00 alfajiri walikuwa wanakwenda kumuona mgonjwa gani,
nililitilia shaka lile begi nikawakamata na kuwaweka chini ya ulinzi,
baada ya kulikagua ndani lilikuwa na bastola moja, risasi 17 pamoja na
vitu vingine, tukashangaa kwanini walikuja na silaha wakati askofu yuko
kwenye mikono salama ya Jeshi la Polisi” alidai Mholeli.
Shahidi huyo aliomba mahakama ipokee hati yenye orodha ya vitu
vilivyokutwa kwenye begi hilo baada ya kupekuliwa na ombi hilo
lilikubaliwa na kupokelewa kielelezo.
Kesi hiyo ilitajwa Mei 2, mwaka huu ilipopangwa tarehe ya kuendelea kusikilizwa na dhamana ya washtakiwa inaendelea.
Mbali na Gwajima wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Askofu Msaidizi
wa kanisa hilo, George Mzava, Mfanyabiashara Yekonia Bihagaze na
Mchungaji Georgey Milulu, wote wanakabiliwa na mashitaka ya kukutwa na
bastola bila kibali.
0 comments:
Post a Comment