CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya mkoani Mara kimesema watu
wanaokejeli juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli si wazalendo ,
wanapaswa kuchunguzwa na Serikali.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye alisema hayo jana
jijini Mwanza alipokuwa akizungumzia juhudi zinazofanywa na Rais
Magufuli kuchukua hatua dhidi ya watu wanaoiba fedha za umma.
“Kumeibuka tabia chafu kutoka kwa baadhi ya watu nchini kwa sasa,
wanapotosha wananchi juu ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli
katika kuwashughulikia mafisadi na wanaoiba rasilimali za nchi,
”alisema.
Alisema taifa haliwezi kukubali kuona kazi nzuri inayofanywa na Rais
ikipotoshwa na watu wachache aliosema hawaitakii mema nchi. “Nani haoni
kazi kubwa inayofanywa na Rais ..., ameimarisha ukusanyaji wa mapato na
ameboresha sekta ya afya, miundombinu, hivi watu hawa wanataka Rais
awafanyie nini?,” alihoji na kuongeza:
“Ni aibu kuona watu wanahoji mambo ambayo hata kwa mtu ambaye hakwenda
shule anaona mafanikio makubwa aliyofanya Rais Magufuli katika kipindi
kifupi ambacho amekuwa madarakani.”
“Huko nyuma walikuwa wanamlaumu aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya
Kikwete kuwa alikuwa mpole, leo tumempata Rais anayesimamia ukuaji wa
uchumi wa nchi wanaleta siasa, sisi Rorya tunasema tuko imara na
tutakufa na Rais Magufuli”.
Aliwataka wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuanza mkakati wa
kuwashughulikia watu wanaomjadili Rais kwa lengo la kupinga mafanikio ya
serikali ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Kiboye alisema CCM wilayani humo inaanza
kuwashughulikia makatibu wa CCM wa Kata ambao ni majipu wanaoanza kuiba
fedha za chama. “Kuna baadhi ya watendaji wabovu katika chama wameanza
kuonekana kuiba fedha za makatibu wa tawi, hawa nao ni majipu muda
ukifika tutawatumbua”, alisema.
0 comments:
Post a Comment