CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kimemtaka Rais Dk John Magufuli kuacha ‘kutumbua majipu’ bila
kufuata taratibu na kanuni za nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Vicent
Mashinji, wakati alipokuwa akifungua kongamano la Baraza la Vijana
Chadema (Bavicha) na Umoja wa wanachadema Vyuo vikuu (Chaso).
Dk. Mashinji alisema kuwa tangu aingie madarakani Rais Magufuli amekuwa
na utaratibu ambao umepewa jina la utumbuaji majipu ambao amekuwa
akiuendesha bila kufuata sheria za nchi.
Alisema kuwa pamoja na kuwa Chadema wanaunga mkono kitendo cha
kuwashughulikia mafisadi pamoja na watumishi wasio timiza majukumu yao
ipasavyo lakini hawakotayari kuendelea kushuhudia ambavyo amekua
akivunja sheria za nchi.
“Watumishi wengi wamedhalilishwa na serikali hii ambayo imekuwa ikitumia
mabavu kuwawajibisha watu bila kufuata sheria za nchi,”alisema Dk,
Mashinji.
“Suala la rushwa katika nchi ni jambo la kimfumo ambapo kila unapoona
kunamtu katumbuliwa kwaajili ya rushwa basi kuna idadi kubwa ya watu
ambao wanashiriki katika rushwa hiyo,” aliongeza Dk Mashinji.
Aidha, alisema kuwa utaratibu wa Rais kuwatumbua watumishi kwenye
mikutano ya hadhara kwa kutumia ushabiki wa wananchi hauwezi kulisaidia
taifa kufanikiwa katika kuwaletea mabadiliko ya kweli wananchi wake.
“Magufuli ametumbua watumishi wengi sana tangu aingie madarakani lakini
niwaulize sukari imeshuka bei au mchele umeshuka bei lakini kila siku
tunasikia watu wametumbuliwa bila kuwa na tija kwa taifa,”alisema.
Aliwataka vijana wa vyuo vikuu nchini kuungana na Chadema katika
kuhakikisha serikali inaruhusu kuonyeshwa kwa vipindi vya Bunge moja kwa
mpja kama ilivyo kuwa hapo awali.
“Bunge maana yake ni mkutano wa hadhara ambao wote tunatakiwa kushiriki
lakini kutokana na udogo wa eneo wanakwenda wawakilishi wetu lakini na
sisi tunatakiwa tufuatilie kupitia runinga zetu moja kwa moja ili tuweze
kujua kinachofanywa bungeni na wawakilishi wetu,”alisema.
Pia aliwataka vijana kuacha ushabiki wa kushabikia siasa bali waikosoe
serikali ili iweze kufanya kazi ambayo ni kuwaletea maendeleo wananchi
wake kwakua huo ndio wajibu wake.
Akizungumza na wenyeviti wa CCM wa Mikoa na Wilaya Ikulu, Rais Magufuli
alisema wanaotetea watu wanaotumbuliwa na wao ni majipu hivyo ataanza
kuwachunguza.
Alisema inasikitisha kuona watu wanatetea watumishi ambao wamekuwa
wakiwaibia watanzania miaka mingi lakini wanapofukuzwa kazi
wanalalamika.
“Kama wamekuwa wakiwaibia wananchi hadharani nasisi tutawafukuza na
kuwatangaza hadharani, inasikitisha kuona baadhi yetu tunatetea watu
wanaofukuzwa kazi,” alisema Rais Magufuli
0 comments:
Post a Comment