
Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM) imesema uamuzi wa aliyekuwa kada wa chama hicho, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kukihama chama hicho ni ukosefu wa uungwana katika dhana ya siasa pamoja na uimla usiokubalika katika siasa za kileo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa
Umoja huo, Shaka Hamdu alisema licha ya Kingunge kukulia ndani ya umoja
huo na kushika nyadhifa mbalimbali ameshindwa kuheshimu matokeo ya
mchuano wa nguvu ya hoja na kutaka kulazimisha fikra zionekane sahihi.
Shaka
alisema umoja huo unamshangaa Mzee kingunge ambaye amekuwa mwanachama
wa jumuiya hiyo hadi kufikia kuwa Katibu Mkuu wa Pafmeca Youth kuibuka
na kukiponda chama alichokitetea katika uhai na maisha yake yote na
kuapa kuwa hakitatokea chama bora nchini kitakacholingana na CCM.
“Tokea
akiwa kijana mdogo, Mzee Kingunge amekuwa mwanachama wa jumuiya yetu
hadi kufikia kuwa Katibu wa Pafmeca Youth iliyokuwa na makao yake makuu
nchini Algeria…. lakini amekosa uungwana katika dhana ya siasa,
alichofanya ni uimla na ufashishti usiokubalika katika siasa za kileo” alisema Shaka.
Alisema
tangu awali kada huyo wa zamani wa CCM alikataa kusimamia taratibu za
kumsaka na kumpata mgombea urais kulingana na sifa na badala yake
akamtaka mgombea aliyepungukiwa na sifa na vigezo.
Aliongeza
kuwa, Kingunge alishindwa kukubali ukweli kuwa urais ni taasisi adhimu
yenye staha na kujikita kumpigania mgombea mmoja ambaye hakuwa na sifa
zinazolingana na hadhi ya chama hicho.
0 comments:
Post a Comment