Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wakuu wa mikoa ya Geita, Arusha
na Kagera kuhakikisha wanaondoa mifugo itokayo nje ya nchi pamoja na
kuwaondoa wanachi waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa (Tanapa) ifikapo
Juni 30 mwaka huu.
Aidha
ameagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanatenga maeneo
maalumu kwa ajili ya mifugo inayotolewa ndani ya hifadhi na kupunguza
mgogoro kwa wananchi wengine.
Samia
alitoa maagizo hayo jana jijini Arusha, wakati alipokuwa akikabidhi
hundi ya thamani ya Sh bilioni moja kwa wakuu wa mikoa 19 inayozunguka
hifadhi za taifa (Tanapa) kwa ajili ya kununua madawati.
Alisema, wakuu wa mikoa wakizembea kutekeleza uondoaji mifugo ndani ya hifadhi za taifa serikali itawawajibisha.
Alisema
waliohifadhi mifugo ndani ya hifadhi hiyo waondoke na mifugo yao hadi
Juni 30 mwaka huu kwani mkoa wa Kagera una ng’ombe milioni mbili
wanaotoka nje ya nchi, na mikoa ya Arusha na Geita ina ng’ombe milioni
tatu kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia
kuhusu kukabidhi madawati 16,500 katika wilaya zote 55 zilizopo kwenye
mikoa 19 nchini, Samia aliipongeza Tanapa kwa kusaidia elimu nchini
kwani baada ya serikali ilipotangaza kuwa elimu bure wanafunzi wengi
wamejitokeza huku kukiwa na changamoto ya madawati
Samia
alisema, kutokana na msaada huo wanafunzi wataondokana na adha ya kukaa
chini na kuumia migongo kwani kila wilaya itapata madawati 300 huku
wanafunzi 49,500 wakiwa wanakaa kwenye madawati na kuongeza usikivu
zaidi.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema Tanapa
wanatambua mchango wa elimu ndio maana wametoa msaada huo kwa mikoa 19
inayopakana na hifadhi za taifa.
Mkurugenzi
wa Tanapa, Allan Kijazi alisema Tanapa itaendelea kushirikiana na
serikali katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi
wanasoma kwa bidii pamoja na kujua jinsi ya kuhifadhi maliasili za
Taifa.
Akitoa
salamu za shukrani kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Said Meck Sadiki aliishukuru Tanapa kwa kutoa madawati kwa wakuu wa
mikoa na kusema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umepiga marufuku usafirishaji
wanyama pori kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)
kuanzia jana.
0 comments:
Post a Comment