IDADI
ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa
imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994.
Ripoti
iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo
kwa waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, imebainisha kuwa hakuna
hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba
2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.
Ripoti
hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za
Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa
kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na
wanawake ni 20.
Wanaharakati
Akiwasilisha
ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya,
alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali
kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa
zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu
hiyo.
Baadhi
ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The
Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika
wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe
mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.
Hata
hivyo, Mponezya alisema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka
adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa
Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri
zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri
kisaikolojia.
“Tume
inasisitiza Serikali iangalie upya hukumu hii na kuiondoa kwa sababu ya
utekelezaji wake. Tangu mwaka 1994 hadi leo watu 465 wanasubiri adhabu
hiyo, hakuna aliyenyongwa. Kila mlango unapogongwa unahisi ni wewe kumbe
la, tunadhani iondolewe maana haitekelezwi,” alisema Mponezya.
Wananchi wagawanyika
Tume
hiyo ilikiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa
miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu
hukumu hiyo.
Wapo
wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na
ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.
Wakili
wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na
kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo,
alikiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna
mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.
“Tume
kadhaa zilizoundwa kupata maoni ya wananchi, zilitoa matokeo kuwa
wananchi wengi bado hawataki adhabu iondolewe, wanataka iendelee kuwapo,
sasa Serikali inafanya kazi kwa matakwa ya wananchi, si vinginevyo,” alisema Mulumbo.
Akifafanua
zaidi, alisema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni
mwafaka kufuta adhabu hiyo.
Marais
Kuhusu
marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa
aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.
Alisema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini.
“Siwasemei
kwamba imani zao ni sababu, lakini huenda ni sababu.Ila kisheria rais
hahukumiwi akisaini hukumu hiyo, sasa hilo mimi siwezi kulisemea ila
sheria zinaweza kuangaliwa zaidi, ili zimpe rais nafasi ya kumpa mhusika
kifungo cha maisha.
“Lakini
hapo napo kuna mtazamo mwingine, maana kuna hoja kwamba kwa nini
aliyeua na kupatikana na hatia afungwe maisha. Je, iko wapi haki ya
aliyeuawa?” Alifafanua Mulumbo kwa mtazamo wake.
Wanaoipenda
Mwanasheria
wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro,
ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, alisema kwamba, utafiti uliofanywa na
taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo,
umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.
Senkoro
alisema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa
dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi
nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa
imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo
muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.
“Wengi
wa jamii yetu wanataka hukumu iendelee kuwapo mpaka hapo mauaji kwa
albino yatakapokoma na itekelezwe. Wauaji wa albino wanaua kwa imani si
tabia, wanatumwa na watu wenye fedha, kiungo kinauzwa Dola za Marekani
2,000, tena tunaona wanaokamatwa ni vidagaa, bado mapapa hatuyaoni,
tunaomba Serikali (ya Magufuli) iwatafute vigogo na tuone hukumu hii
ikitekelezwa ili kumaliza imani hizi zinazowanyima haki baadhi yetu ya
kuishi,” alisema Senkoro.
Pamoja
na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu,
bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa
utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta
adhabu ya kifo.
Mkutano
huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu
nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo
nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.
Ripoti
mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International,
imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa
hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia
50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa
hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa
zinatajwa kuwa kubwa.
Nchi
zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan
na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa.
0 comments:
Post a Comment