Wizara
ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa
madini Tanzania (TAMIDA) iliendesha Maonesho ya tano ya Kimataifa ya
Madini ya Vito yaliyofanyika Jijini Arusha katika Hoteli ya Mount Meru
kuanzia tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2016.
Maonesho
haya hufanyika kila mwaka Jijini Arusha na hukutanisha washiriki
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wachimbaji, Wafanyabiashara wa madini ya
vito wa ndani na nje, wanunuzi wa madini wa ndani na nje, na wataalam
mbalimbali wenye uzoefu wa shughuli za madini ya vito.
Maonesho
hayo yalihudhuriwa na washiriki 813 kutoka katika nchi 26 duniani
ambazo ni Tanzania Marekani, Sri Lanka, India, Kenya, China, Ujerumani,
Namibia, Australia, Austria, Israel, Italia, Uingereza, Hong Kong,
Switzerland, Zambia, Madagascar, Afrika Kusini, Msumbiji, Urusi,
Cameruni, Canada, Malawi, Sudani, Malta, na Thailand).
Aidha,
wanunuzi (buyers) wa madini walikuwa 353, Walioshiriki kuonesha madini
kwenye mabanda (Exhibitors) 300, na wageni mbalimbali 160.
Lengo
kubwa la Maonesho haya ni kama ifuatavyo: kufanya Arusha kuwa kitovu
cha madini ya vito katika Afrika ili hatimaye iwe ni kitovu cha biashara
ya madini hayo; fursa ya masoko kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa
mdini ya vito nchini; na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani
madini ya vito hapa nchini.
Katika maonesho hayo, madini yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.5, sawa na Shilingi Bilioni 9.9 yaliuzwa.
Serikali
ilipata jumla ya Shilingi bilioni 1.71, ambapo Shilingi bilioni 1.3
zilitokana na mnada wa madini yaliyokamatwa na kutaifishwa na Serikali,
Shilingi milioni 388 zilitokana na mrabaha uliolipwa kutokana na madini
yaliyonunuliwa, na Shilingi milioni 26 zilitokana na vibali vya
kusafirisha madini nje ya nchi.
Manufaa
mengine yaliyopatikana wakati wa maonesho ni pamoja na wageni kuingiza
fedha za kigeni hapa nchini ambazo hutumika kwa ajili ya malazi,
usafiri, chakula na kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii hapa
nchini.
Ili
kuweka utaratibu utakaodhibiti shughuli za madini ya vito hususani
tanzanite, Serikali inakusudia kuanzisha minada ya ndani mbali na mnada
unaofanyika wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Vito Jijini Arusha.
Minada hiyo itatoa fursa kwa wafanyabishara wa ndani kununua madini kwa
ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani madini
hayo na kutengeneza vidani mbalimbali.
Ili
kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito nchini,
Serikali inakusudia kuimarisha Kituo cha Jimolojia kilichoko Arusha
(Tanzania Gemmological Centre -TGC) ili kufundisha na kuzalisha vijana
wa Kitanzania wa kutosha wenye ujuzi wa kusanifu na kung’arisha madini
ya vito. Tayari vijana 29 wameshapata mafunzo ya miezi 6 ya ukataji wa
madini ya vito kutoka kwenye kituo hicho tangu 2014. Wanafunzi wengine
18 wanaendelea na mafunzo ya miezi 6 yaliyoanza mwezi Machi, 2016.
Aidha,
upo mpango wa kuanzisha EPZ eneo la Merelani ambapo ni karibu na
machimbo ya tanzanite kwa lengo la kupata eneo maalum ambapo shughuli za
biashara ya madini na uongezaji thamani madini ya tanzanite zitafanyika
kwa uhuru na wazi. Pamoja na juhudi zote hizo, Serikali itaendelea
kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini mbalimbali nje ya nchi
ikiwemo Tanzanite kwenye viwanja vya ndege na kwenye migodi ambapo
madini yanazalishwa.
Wito
wa Serikali ni kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini
kuzingatia sheria zilizopo wakati wa kufanya shughuli zao.
Imetolewa na;
KAIMU KAMISHNA WA MADINI
MHANDISI ALLY SAMAJE
0 comments:
Post a Comment