Hatimaye
uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umevunja mkataba wa
uwekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) na Kampuni ya Simon
Group Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara, Robert Kisena.
Mkataba
huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele ndani na nje ya Serikali, umetajwa
kutokufuata taratibu za kisheria na kukiuka Sheria ya Manunuzi (PPRA).
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Meya wa Jiji la Dar es
Salaam, Isaya Mwita alisema uamuzi huo umefikiwa, baada ya kufanyika
kikao halali cha Baraza la Madiwani.
Aidha
baraza hilo la madiwani pia limeamua kwamba, asilimia 51 ya hisa
zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni hiyo zirudishwe chini ya uongozi wa
jiji hilo.
Mwita
alisema madiwani walipitia upya mkataba wa uwekezaji kati ya kampuni
hiyo na Halmashauri ya Jiji, ambapo walibaini udhaifu katika maeneo
mbalimbali wakati wa makabidhiano.
Meya
huyo anayetokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na waziri mwenye dhamana
ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoshirikishwa wakati wa makabidhiano.
“Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam, imevunja mkataba wa makubaliano ya kuuza
Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa mfanyabiashara Robert Kisena,
baada ya kubaini kuwapo udhaifu wakati wa kuuza shirika hili,” alisema.
Mwita
alisema halmashauri ya jiji kipindi hicho, haikufuata utaratibu wa
utangazaji wa zabuni wakati wa kuuza shirika hilo, hali iliyoonyesha
wazi viongozi waliokuwa madarakani wakati huo, walikuwa na maslahi
binafsi katika kukabidhi shirika hilo mikononi mwa kampuni hiyo.
Alisema
hadi sasa shirika hilo bado limesajiliwa kwa jina la Halmashauri ya
Jiji kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hali inayowapa
nguvu ya kuvunja mkataba huo kwa sababu mmiliki wake kisheria bado ni
jiji.
“Tuliambiwa
Simon Group, alikuwa anakwenda benki kuchukua mikopo kwa hati ya
Shirika la UDA, tumefuatilia benki mbalimbali tumebaini hakuna hata hati
moja ya shirika iliyowasilishwa kwenye benki kama dhamana ya mikopo,”alisema.
Alisema
shirika hilo hadi sasa lina Sh bilioni 5.9 ambazo zililipwa na Simon
Group kama malipo halali ya kuuziana shirika, jambo ambalo haliko sawa.
“Hatuwezi
kuona mikataba ya kifisadi inaendelea kuimaliza Serikali, lazima
tuchukue hatua ambazo ni pamoja na kuangalia taratibu za kisheria ili
kuivunja,’ alisema.
Alisema
kutokana na hali hiyo, baraza hilo limeunda timu ya watu watatu
wakiongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ili kuangalia athari ambazo
zinaweza kujitokeza wakati wa kuvunjwa kwa mkataba huo.
Akizungumzia
hatua hiyo, Ofisa Habari wa Kampuni ya Simon Group, Deus Bugaywa
alisema hadi sasa halmashauri ya jiji haijatoa taarifa yoyote ya
kuonesha kama mkataba huo umevunjwa, licha ya magari ya UDA kuanza kazi
leo.
“Hatujapewa
taarifa yoyote ambayo inasema mkataba kati ya UDA na Halmashauri ya
Jiji umevunjwa, tunaamini bado ni wana hisa halali tutafanya kazi kwa
ubia kama ulivyo mkataba wetu,”alisema Bugaywa.
Alisema kampuni hiyo, ilifuata taratibu zote za kisheria wakati wa kuingia makubaliano, wala hakukuwa na ukiukwaji wa kisheria.
Alisema kama watakabidhiwa barua ya kuvunjika kwa mkataba huo, wataangalia taratibu za kisheria ili waweze kudai haki yao.
0 comments:
Post a Comment