FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza kushangazwa na
Serikali ya Rais John Magufuli kupenda kusifiwa zaidi na kuchukia
kukosolewa.
Sumaye bila kumtaja jina Rais Magufuli ameleza
kushangazwa na hatua ya serikali kuminya uhuru wa habari na kwamba,
kufanya hivyo kunalenga kuficha madudu yanayofanywa na watendaji wake.
“Wapowatawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana kusifiwa.
Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa
zake tu.
“Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa
habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,”
amesema Sumaye.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika
maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyoratibiwa na
Chama cha Waandishi wa Habri za Siasa (TAPOREA), Sumaye amesema,
serikali inakiuka Katiba ya nchi.
Amesema, serikali yoyote inayopambana na vyombo vya habari na kuminya
uhuru wa kufanya kazi zao huwa ina tatizo kwa upande wa wanaotawala.
Akitolea mfano wa hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja
ya bunge Sumaye amesema, kwa kufanya hivyo serikali imevunja Katiba.
“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge, kwanza
ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu ana haki
ya kupewa taarifa wakati wote.
“Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ (moja kwa moja) wewe serikali
unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa
unayoitaka wewe,” ameeleza Sumaye.
Kuhusu sababu iliyotolewa kwamba, matangazo hayo yanatumia gharama ya Sh. 4 bilioni amesema haina mashiko.
Sumaye amesema, hata kama matangazo hayo yatarushwa na ofisi za bunge
bado, gharama zitaongezeka zaidi kwa sababu Bunge litahitaji kununua
mitambo pamoja na kuajiri wafanyakazi wake.
Sumaye amesema, serikali yenye demokrasia ya kweli lazima ikubali wananchi wake kutoa maoni.
“Serikali yoyote yenye utawala bora, ingependa mambo yake
inayoyafanya kwa ajili ya wananchi wake mambo hayo yajulikane kwa
wananchi hao.
“Ukiona serikali inaficha mambo yake lazima kuna mambo wanayoyafanya ambayo hayafai na wasingependa jamii ijue,” amesema Sumaye.
George Maziku, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPOREA amesema, ripoti ya hali
ya uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari
kimataifa, iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka
lenye Makao Makuu yake nchini Ufaransa haipendezi.
Amesema, ripoti hiyo inaonesha kuwa, katika miaka 10 iliyopita zaidi
ya waandishi wa habari 800 kutoka mataifa mabalimbali duniani wameuawa
wakiwa wanatekeleza kazi zao.
“Kitisho kingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ni utamaduni
mpya ulioasisiwa na kuimarishwa na watawala wa sasa na kuvishinikiza
vyombo vya habri kutomkosoa Rais John Magufuli na serikali yake.
“Matokeo yake, vyombo vingi vya habari nchini vimelazimika kuandika habari za kumfurahisha Rais Magufuli,” amesema Maziku.
0 comments:
Post a Comment