Ufungaji
wa vifaa vya kielektroniki katika hospitali za Serikali katika mikoa
mbalimbali, umeibua fukuto la ufisadi mkubwa, uliokuwa ukifanywa katika
makusanyo ya fedha wanazolipa wagonjwa kwa ajili ya huduma.
Akizungumza
bungeni mjini Dodoma jana katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Selemani Jafo, alisema tangu mfumo huo wa kielektroniki
uanze kutumika katika hospitali nyingi nchini, mapato yameongezeka.
Jafo
alisema mafanikio hayo ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa
elektroniki, yamesababisha katika sekta ya afya kwa sasa ajenda kuu iwe
kuongezea mapato ya hospitali zote nchini, kuendane na utoaji wa huduma
bora.
Hospitali ya Rufaa Mbeya
Akitoa
mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jafo alisema kabla ya kufungwa
kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya Sh milioni 70 kwa mwezi, lakini
baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato yameongezeka zaidi ya mara saba na
kufikia Sh milioni 500 kwa mwezi.
Taarifa
zinaonesha pamoja na ongezeko hilo la mapato, bado hospitali hiyo
iliendelea kukosa vifaa muhimu vya tiba, ikiwemo mashine ya CT-Scan,
kiasi cha kusababisha mwanzoni mwa mwaka huu Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla
kuwajia juu watendaji wake.
Dk
Kigwangalla alielezea kushangazwa kuona hospitali hiyo ikikusanya Sh
milioni 500 kwa mwezi, huku ikidai kukosa CT-Scan na kutoa siku 60 kifaa
hicho kifungwe.
Katika
maelezo aliyopewa, Dk Kigwangalla alielezwa kuwa ingawa ni kweli
hospitali hiyo inakusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, lakini mahitaji ya
dawa pekee yanachukua zaidi ya Sh milioni 300, kabla ya gharama nyingine
ikiwemo za usafiri wa magari.
Alielezwa
kuwa hospitali hiyo imejipanga kuchukua mkopo kutoka Mfuko wa Bima ya
Afya ya Taifa (NHIF), kwa kuwa ili kupata mashine hiyo, wanapaswa kuwa
na kuanzia Sh milioni 800 mpaka Sh bilioni 1.2.
Sekou Toure
Mbali
na Mbeya, katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa mujibu
wa Jafo, kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya kati ya
Sh 150,000 mpaka 200,000 tu kwa siku.
Jafo
alisema baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato hayo yaliongezeka mpaka
karibu mara 21 na kufikia Sh milioni 3.2 kwa kila siku.
Hospitali ya Tumbi
Mbali
na Mwanza, Naibu Waziri huyo wa Tamisemi, alisema mkoani Pwani katika
Hospitali ya Tumbi, nako kabla kufungwa vifaa hivyo, makusanyo yalikuwa
Sh 200,000 kwa siku lakini baada ya kufungwa, mapato yakaongezeka mara
20 na kufikia Sh milioni nne kwa siku.
Kutokana
na mafanikio ya hospitali hizo, Jafo aliwataka wabunge wote kufuatilia
kwa makini hospitali katika halmashauri zao za wilaya, ili kila moja
iweke mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato katika huduma
ya afya.
Aliwataka
wabunge hao kuweka kipaumbele katika kuhakikisha hospitali zote katika
maeneo yao, zinafungwa mifumo hiyo ya kielektroniki, ili fedha
zikusanywe kusaidia katika kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.
“Tusipozingatia
haya, hata tukipeleka fedha bado tutakuwa na matatizo, ndio maana
ajenda yetu kuu ni kutumia mifumo ya kielektroniki, ili kuongeza mapato
katika sekta ya afya,” alisisitiza.
Awali
Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alitaka kufahamu kama
Serikali haioni umuhimu wa kuiongezea fedha Hospitali ya Mji wa Mafinga,
ili ihudumie kwa ufanisi idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria
hospitali hiyo.
Pia
Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuiongezea
hospitali hiyo watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata, ili iwe
na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa kazi.
Akijibu
maswali ya mbunge huyo, Jafo alisema Serikali imekuwa ikiipatia
Hospitali ya Mji wa Mafinga Sh milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na Sh
milioni 90 kwa matumizi mengineyo ; na kwamba inaweza kuongezewa fedha
hizo kulingana na wigo wa upatikanaji wa fedha.
Kuhusu
watumishi, alisema hospitali hiyo ina watumishi 209 na upungufu uliopo
ni wa watumishi 95, sawa na asilimia 31.3 na kwa mwaka wa fedha 2016/17
imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18.
0 comments:
Post a Comment