Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imesitisha kwa muda ajira zote kwenye vyombo
vya ulinzi na usalama vilivyomo ndani ya wizara hiyo, ikiwemo Jeshi la
Polisi ili kupitia upya utaratibu wa kutoa ajira na kuondoa uwezekano wa
watu wasio na sifa kujipenyeza.
Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema hayo jana
bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu
(Chadema), aliyetaka kufahamu ni kwa nini Serikali inasitisha ajira
katika Jeshi la Polisi, wakati bado nchi inakabiliwa na uhaba wa askari
ndani ya jeshi hilo wakiwemo askari wa kike.
“Tumesitisha
kutoa ajira ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuondoa uwezekano wa
watu wasio na sifa kujipenyeza na kupata ajira ndani ya vyombo vilivyo
chini ya wizara hiyo,” alisisitiza.
Miongoni
mwa vyombo hivyo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
mbali na Jeshi la Polisi ni Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na
Uhamiaji.
Mbali
na Komu, Mbunge mwingine ambaye ni wa Viti Maalumu, Hawa Mwaifunga
(Chadema), alitaka kufahamu Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha
askari wasio na sifa wanachukuliwa hatua, ambapo pia alitaka kufahamu
utaratibu wa uhakiki vyeti vya askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la
Polisi umefikia wapi.
Akizungumzia
Jeshi la Polisi, Masauni alisema Jeshi la Polisi limo kwenye utaratibu
wa kuwachukulia hatua za kisheria askari wachache, wanaochafua taswira
na kazi nzuri inayofanywa na Polisi kwa kukiuka sheria, kanuni na
taratibu kwa kujihusisha na vitendo vinavyokinzana na maadili.
Kuhusu
uhakiki wa vyeti, waziri huyo alielezea kuwa, uhakiki huo unahusu
askari wasio na sifa ndani ya Jeshi la Polisi unaendelea na mpaka sasa,
askari 19 wamechukuliwa hatua za kisheria baada ya kugundulika kuwa
walipata ajira kwa njia zisizokubalika.
Kuhusu
uhaba wa askari wa kike, Waziri huyo alikiri kuwa kuna uhaba wa askari
wa kike katika Jeshi la Polisi na kutoa mwito kwa wanawake wahamasike
zaidi kujiunga na vyombo vya usalama.
Mwaka
jana Idara ya Uhamiaji iliyokuwa chini ya Wizara hiyo, ililazimika
kufuta ajira mpya 200 za makonstebo na makoplo, baada ya kubaini
upatikanaji wa ajira hizo, ulifanyika kwa upendeleo.
0 comments:
Post a Comment