WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini zipitie upya riba zake ili
Watanzania waweze kukopa na kurejesha kwa urahisi.
Amesema
riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma zisizokidhi mahitaji
na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni miongoni mwa changamoto
wanazokabiliana nazo wananchi wanapotaka huduma za kifedha.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 15, 2016) wakati wa ufunguzi
wa mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT) mjini
Dodoma.
Mkutano
huo ulijumuisha wajumbe kutoka mikoa 10 ya Kigoma, Lindi, Simiyu,
Manyara, Katavi, Mbeya, Mwanza, Morogoro, Singida na Dodoma kati ya
mikoa 18 ya Tanzania Bara ambayo bado haina Benki za Wananchi ila ipo
katika hatua za kuanzisha.
Amesema
changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za sheria na
taratibu ambazo zinakwamisha ufanisi wa kiutendaji kwa baadhi ya taasisi
hasa zile zinazolenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini.
“Tunahitaji
kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi, na Benki za Wananchi ni
kiungo muhimu katika kushughulikia changamoto zinazokabili utoaji wa
huduma za kifedha,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema ni muhimu kuanzisha Benki za Wananchi katika kila Mkoa ili
kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi na walengwa, hali ambayo
itasaidia kupunguza umasikini kupitia ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Amesema
Serikali itaangalia uwezekano wa kuiwezesha mikoa ambayo itaonyesha ari
zaidi ya kuanzisha benki zao na akatoa wito waandae mikakati ya
kuhamasisha wananchi ili wakusanye mitaji ya kutosha.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa COBAT, Bibi Elizabeth Makwabe amesema
Jumuiya yao ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanachama saba na sasa hivi
wamefikia 10 huku wananchi wanaowahudumiwa na benki hizo ni zaidi ya
milioni mbili.
Amesema
Jumuiya za Benki ya Wananchi inakabiliwa na changamoto mbalimbali
zikiwemo mfumo hafifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
pamoja na ufinyu wa mitaji.

0 comments:
Post a Comment