Saturday, May 7, 2016

Mama Salma Akerwa na wanaoubeza utawala wa Mumewe


SALMA Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ameonesha kukerwa na wale wanaoshambulia utawala wa mumewe (Rais Kikwete) na kwamba, hakuna sababu ya kufanya hivyo, anaandika Dany Tibason.

Mama Salma amesema hayo leo kwenye mkutano wa Umoja wa Wanawake (UWT) unaofanyika mjini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa CCM Makao Makuu. 

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kujitokeza hadharani kumkingia kifua mtoto wake Ridhiwani Kikwete kuhusu kuhusika kwake na mkataba wenye utata wa Kampuni ya Lugumi. 

“Kila mwaka naendelea kuisemea serikali iliyopo madarakani mambo mazuri, acheni hali ya kukaa na kuanza kusema kwamba serikali ile ilikuwa vile na serikali hii iko hivi. 

“Wala msisema yule alikuwa vile na huyu yuko hivi, kwa kumalizia hayo napenda kusema mume wangu ambaye ni mwenyekiti wa CCM Taifa anawasalimia sana,” amesema Mama Salma. 

Akizungumzia utumbuaji wa majipu amesema, serikali kwa sasa imeanza kutumbua majipu makubwa kuanzia juu lakini zipo taarifa kuwa, yapo majipu mengine ngazi za chini pia ndani ya CCM. 

Amesema, “kila anayejitambua kuwa ni jipu kabla hajafikiwa ni bora akajitumbua mwenyewe au ajipake spriti ili jipu hilo lipoke mapema kabla halijatumbuliwa.” 

Hata hivyo ameonesha wasiwasi kuwa, kuna uwezekano miradi mingi ya UWT ikachukuliwa kutokana na umoja huo kuwa na mali ambazo zinaonekana kumilikiwa bila kufuata taratibu. 

Amesema, kwa upande wa ardhi kuna viwanja vingi ambavyo havina hati na vimekaa muda mrefu bila kuendelezwa jambo ambalo kwa sasa mameya wanaweza kuvibadilishia matumizi.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger