Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuchoshwa na utendaji wa Rais John Magufuli katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Prof. Lipumba alitoa kauli hiyo jana mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya CUF iliyopo Buguruni, Dar es Salaam.
Katika
kukabiliana na changamoto za nchi hususani sekta ya uchumi, Prof.
Lipumba amemshauri Rais Magufuli kutafuta ushauri sambamba na taratibu
za kujenga uchumi wa soko shirikishi kutoka kwa Benjamin Mkapa, Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu.
Alisema,
uzoefu wa Rais Mkapa wa kujenga utawala wa serikali unaweza kumsaidia
kufanya uamuzi sahihi utakayosaidia wananchi badala ya kukagandamiza.
Mchumi huyo alieleza
kuwa, vitisho na ubabe wa Rais Magufuli vinaweza kuwaogopesha watendaji
wake wakiwemo mawaziri na hivyo kushindwa kumueleza hali halisi na
kwamba, kitendo hicho kinaweza kuathiri maendeleo ya nchi.
“Kuna
dalili kwa baadhi ya watendaji wa serikali hasa mawaziri, wakuu wa
mikoa na wilaya za kushindwa kutoa fikra zao zenye lengo la kuimarisha
uchumi wa nchi au kueleza hali halisi iliyopo kwa kuhofia vitisho vya
rais ili wasitumbuliwe,” amesema.
Prof. Lipumba ametoa
kauli hiyo wakati nchi ikiwa kwenye sintofahamu ya upatikanaji wa
sukari ambapo kwa mujibu wake (Lipumba), uhaba huo umesababishwa na
agizo la rais la kuzuia uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
“Agizo
alilolitoa Rais Magufuli Februari 28, 2016 wakati akiwashukuru
waandishi wa habari, wasanii na makundi yaliyoshiriki kwenye kampeni
zake za uchaguzi 2015 ndilo lililosababisha haya,” alisema na kuongeza;
“Kauli
ya serikali ya kuzuia utolewaji wa vibali vya uingizwa wa sukari kutoka
nje ndiyo iliyosababisha upungufu wa sukari, asiuaminishe umma kuwa
sababu ni wafanyabiashara kuficha sukari.
“Kwa
mwenendo huu nchi haitaendelea kutokana na kwamba badala ya vyombo vya
dola kushughulikia masuala ya msingi ili kuleta tija katika maendeleo ya
Taifa, vinahaha kutafuta sukari zilizofichwa.”
Alitoa
mfano wa kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) cha kutafuta wafanyabiashara wanaoficha sukari badala ya
kushughulika na masuala nyeti ya ubadhilifu wa mali za umaa kama Tegeta
Escrow.
“Wafanyabiashara
wanaopata kibali na wanaopitisha sukari kwa magendo wanapata faida
kubwa kwa sababu bei ya sukari katika soko la dunia mwezi Agosti 2015
ilikuwa Dola za Marekani 250 kwa tani moja,” amesema.
Alifafanua
kuwa, kama dola moja ni sawa na Sh. 2000 tani moja ya sukari iliuzwa
Sh. 500,000 sawa na Sh. 500 kwa kilo moja na kwamba, ukiongeza na
gharama za usafiri kila kilo moja ya sukari itafika kwa Sh. 600.
“Wafanyabiashara
wakubwa na wa kati wanaoingiza sukari nchini hupata faida kubwa
ukilinganisha na viwanda vya ndani kutokana na kwamba, uzalishaji sukari
viwandani unagharimu mtaji mkubwa na kupelekea bei kuwa kubwa na
kusababisha kupoteza soko,” alisema.
Alishauri
kuwa, kama serikali ina lengo la kulinda viwanda vya ndani ihakikishe
inaanda mfumo wa mnada wa ugawaji wa leseni ili kutoa fursa kwa
wafanyabiashara na viwanda kupata leseni za kuingiza sukari inayotoka
nje ili viwanda vipate masilahi pamoja na wafanyabiashara.
“Ingawa
utolewaji wa vibali utaathiri viwanda vya ndani kutokana na kushindwa
kushindana na wafanyabiashara, ni vema serikali ikatoa vibali kwa watu
wote,” alisema.
Kama
serikali inataka kujenga uchumi wa viwanda haina budi kutoa motisha kwa
wawekezaji ili wavutiwe kuwekeza katika sekta zote nchini.
“Rais anahitaji aelewe uchumi wa soko shirikishi, awape nafasi wahusika, asifanye maamuzi kwenye mikutano ya siasa au hadhara,” alisema.
0 comments:
Post a Comment