Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
akijitetea kwa kutoongeza mshahara, Bara wafanyakazi wamelia kunyanyaswa
na wawekezaji, huku walimu watoro wakinyooshewa kidole.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo ya Mei Mosi, Dk Shein aliwaacha hoi
wafanyakazi pale aliposema kuwa katika utekelezaji wa ahadi ya
kuimarisha masilahi yao, hawezi kufanya usanii na hawezi kuahidi
yasiyotekelezeka.
“Ni kweli mimi
nilikuwa msanii nikiigiza nilipokuwa nasoma shule, miaka ya 60 na 70,
nikicheza michezo ya kuigiza pamoja na kuimba, lakini kwa sasa mimi ni
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi siwezi kufanya
mzaha na haki ya watu ninaowaongoza, hii ni haki ya wananchi”,
alifahamisha.
Akikumbushia ahadi aliyotoa wakati wa kampeni alipokuwa akiomba kuchaguliwa tena kabla ya Oktoba 25, 2015, Dk Shein alisema:
“Serikali
itaendelea kuimarisha masilahi ya wafanyakazi kwa kutekeleza ahadi
yangu niliyoitoa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu, nilipokuwa nikinadi
Ilani ya CCM ya kutoa mshahara wa kima cha chini cha Shilingi 300, 000
kwa mwezi”.
Hata hivyo katika
utekelezaji wa ahadi hiyo iliyosubiriwa kwa hamu na wafanyakazi hao, Dk
Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliwataka
Wazanzibar kuwa na subira wakati Serikali ikiandaa kuangalia upya suala
la mafao na posho za watumishi.
“Nakuombeni
sana muwe na subira kwani subira huvuta heri tutayaangalia upya mafao
na posho nyingine za watumishi ili ziende na wakati kwa kadri hali yetu
ya uchumi inavyoruhusu,”alisema.
Pamoja
na ahadi hiyo iliyosababisha sehemu ya wafanyakazi kuguna na kuinamisha
vichwa wakati wa hotuba hiyo, Dk Shein alibainisha changamoto iliyopo
katika kukabiliana na madeni ya wafanyakazi, pensheni za wastaafu,
pamoja na walimu wanaoidai Serikali.
“Vile
vile tutafanya kila tuwezalo ili tulipe viinua mgongo kwa wakati na
tulipe malimbikizo ya malipo ya wafanyakazi hasa walimu, ninafahamu
kwamba bado walimu wanadai haki yao ambayo bado hawajalipwa; tutawalipa
walimu deni lao ambalo ni haki yao ambayo bado hawajalipwa, tutaandaa
utaratibu bora zaidi wa namna ya kulimaliza deni hilo”.
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (Zatuc),
Khamis Mwinyi Mohamed, akisoma risala ya watumishi wa sekta ya umma na
binafsi katika kilele hicho alisema, ni vyema Rais akatekeleza ahadi
zake kwa wafanyakazi kila anapozitoa, ili kuwapa moyo katika utekelezaji
wa majukumu yao ya kila siku.
Alisisitiza
haja ya waajiri kuzingatia mazingira ya utoaji wa bima ya afya kwa
wafanyakazi, ili kuwapa moyo na kuwahakikishia usalama wakati na baada
ya utumishi wao.
Kilimanjaro
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Meck Sadiki amesema wafanyakazi hewa ni
pamoja na walimu ambao hawaingii darasani kufundisha na badala yake
wanafanya biashara nyingine.
Akihutubia
umati wa wafanyakazi katika viwanja vya Ushirika Mjini Moshi mkoani
hapa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, alisema kuwapo
kwa walimu hewa shuleni kumechangia ongezeko la kushuka kwa daraja la
elimu kimkoa.
“Kiwango cha ufaulu
mkoani hapa ni tofauti na miaka iliyopita, kwani mkoa huu ulikuwa
ukishika nafasi za mwanzo katika viwango bora, na mwaka huu umeshika
nafasi ya 17 kati ya mikoa yote, hii ni kutokana na walimu kutoingia
madarasani kufundisha,’’alisema Sadiki.
Sadiki
alilaani unyanyasaji wa waajiriwa ambao wamekuwa wakinyimwa haki zao za
msingi kama likizo, malimbikizo na nyongeza ya mshahara.
“Kila
mfanyakazi lazima apate stahiki zake iwe ni wa serikalini au ni wa
kutoka shirika binafsi, lazima apewe haki zake zinazohitajika na mwajiri
akienda kinyume basi sheria itachukuliwa dhidi yake,’’ alisema Sadiki.
Mbeya waangua kilio
Wakati
hayo yakijiri Kilimanjaro, mkoani Mbeya wafanyakazi zaidi ya 20 wa
kampuni ya kutengeneza marumaru za miamba, maarufu kwa jina la Marmo and
Granito Mines (T) Limited, waliamua kujiangusha chini na kulia kwa
sauti wakidai Serikali iwaokoe na manyanyaso.
Tukio
hilo lilitokea wakati wafanyakazi wakiandamana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Amos Makalla aliyekuwa akiyapokea maandamano hayo ya Mei Mosi
Uwanja wa Sokoine.
Wafanyakazi hao
walisema mwajiri wao anawanyanyasa kwa matusi, kuwapiga, kuwalipa
mshahara mdogo na kwamba Serikali haijawasaidia tangu walipowasilisha
kero hizo miaka kadhaa iliyopita.
Tukio
hilo lilisababisha vicheko kwa watu mbalimbali huku, Mwenyekiti wa
Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi mkoa wa Mbeya (Tucta), Pilipili Zege
Kokoko akisema kilio hicho ni cha kuashiria kero kubwa na ya siku
nyingi.
Kokoko alimwomba Mkuu wa mkoa
kulifuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba wawekezaji wengi wamekuwa
kero kwa Watanzania kutokana na kuwalipa mishahara midogo na
kuwanyanyasa.
Naye Kaimu Katibu wa
Tucta mkoani hapa Juma Bwikitia akisoma risala alisema kampuni za
ujenzi, migodi, viwanda na mashambani ndizo zinazoongoza kwa
kuwanyanyasa wafanyakazi pamoja na kushindwa kutoa mikataba kwa
wafanyakazi.
Bwikitia alisema kampuni
za aina hiyo pia ndizo zinazoongoza kwa kuajiri wafanyakazi wa kigeni na
wasiofuata taratibu ambao wanapata mishahara mikubwa ikilinganishwa na
ile ya wanaopata Watanzania.
Akizungumzuia
suala la wafanyakazi kwa ujumla, Mkuu wa mkoa alisema tatizo la
wafanyakazi waliolia uwanjani hapo, atalishughulikia wiki hii
atakapokwenda kiwandani ili kuzungumza na wafanyakazi wote wakiwa na
waajiri wao.
Makalla alisema atahakikisha anazishughulikia kero za wafanyakazi kupitia kwa wakuu wa wilaya na viongozi wengine.
0 comments:
Post a Comment