“KIFOO kifoo, kifoooo kifoo, kifoo hakina huruma…, ndivyo
wanavyokumbuka wakazi wa Kongo na wapenda muziki kwa ujumla duniani kote
katika kuomboleza vifo vya watu wawili mashuhuri katika muziki wao.
Baba
wa mwanamuziki nguli barani Afrika, Koffi Olomide ‘Mopao Mokonzi’
anayetamba na wimbo wa ‘Selfie’, Charles Agbeba aliyekuwa mcheza mpira
maarufu nchini humo katika timu ya AS Vita ya nchini Kongo.
Mzee huyo amefariki dunia Jumamosi iliyopita akiwa nchini Ufaransa
huku Koffi akitoa shukrani kwa wasanii mashuhuri waliofika nyumbani
kwake na kumfariji kutokana na kumpoteza baba yake huyo.
Leo nguli wa muziki Papa Wemba anatarajiwa kupumzishwa katika nyumba
yake ya milele nchini humo, baada ya kufariki akiwa jukwaani akifanya
shoo nchini Ivory Coast.
Rais Kabila atoa machozi
Rais wa Kongo (DRC), Joseph Kabila, alijikuta akishindwa kujizuia
hadi machozi yakamtoka aliposikia salamu maalumu za familia kutoka kwa
binti wa kwanza wa Papa Wemba, Tellier Shungu Anaendo Caddy.
Binti huyo alianza salamu hizo kwa kusema kwamba ni wajibu wao kutoa
salamu za heshima na shukurani kwa Rais wao Kabila kwa msaada mkubwa
alioutoa kufanikisha mazishi ya baba yao mpendwa.
Binti huyo alizungumzia baadhi ya kumbumkumbu ambazo wengi
hawazifahamu akisema kuwa baba yake amefariki kwa mapenzi ya Mungu,
ingawa wanakabiliwa na kazi ngumu ya kumzungumzia baba yao aliyekuwa
kipenzi na rafiki wa watu hasa raia wa Kongo DR.
Aliendelea
kusema kuwa baba yao alikuwa akiitunza na kuilea kwa upendo na ukarimu
uliopindukia familia yao. Hakusita kuwachukua watoto yatima na kuishi
nao kama familia moja, Caddy aliendelea kusema wanajivunia kuwa na baba
aliyekuwa na tabia nzuri kwa kuwafundisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na
kuwa na tabia nzuri, utu na maadili mema.
Binti huyo alimuelezea baba yake kuwa na uwezo mkubwa wa kuchanganya
maisha ya kiasili na ya kisasa, huku akikumbuka kwamba baba yao amekufa
akiaacha ahadi kwa mjukuu wake, Ambre ambaye ni mtoto Caddy kwamba
angekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha harusi yake.
Ripoti ya daktari
Caddy anasema kabla ya marehemu baba yake, Papa Wemba hajakwenda
nchini Ivory Coast kuhudhuria tamasha aliloalikwa, daktari wake
alimthibitishia kwamba alikuwa na afya nzuri ndiyo maana walimruhusu
kwenda huko.
“Msiba kwa familia za Kiafrika ni alama tosha ya umoja, ushirikiano,
kusameheana na kuimarisha uhusiano hivyo raia wote wa Kongo DR katika
kipindi hiki cha maombolezo tuwe wamoja, kifo cha mzee Wemba kiwe chanzo
cha kuamsha ari ya uzalendo na utamaduni wa Kongo na nyanja za
kimataifa.
“Kifo cha baba yangu kiwe jukwaani, kiwe chanzo cha kuunganisha
historia ya tamaduni za nchi mbili, Kongo DR na Ivory Coast,’’ alimaliza
binti huyo na kuwatoa machozi watu wengi waliokuwa wakimsikiliza kwa
makini.
Nyimbo zatungwa
Katika hatua nyingine wanamuziki mbalimbalia akiwemo, Adolphe
Dominguez wa bendi ya Wenge Tontatonya, ametunga wimbo maalumu kwa ajili
ya marehemu Papa Wemba ‘Embleme De La Musique Africaine (Nembo ya
muziki wa Kiafrika).
Katika wimbo huo aliouimba kwa hisia kali za kuomboleza, amemuelezea
Wemba kuwa ni mfalme wa muziki wa rhumba na askari wa muziki wa Kongo DR
pia amezitaja baadhi ya nchi mbalimbali za Afrika pamoja na Asia, Ulaya
kwamba nao wanamlilia.
Ratiba ya mazishi
Katika ratiba ya mazishi iliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo chini
ya kamati ya maandalizi iliyowashirikisha baadhi ya ndugu wa marehemu,
wanamuziki, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali na Wizara ya
Mawasiliano na Utamaduni, inasimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Jiji la
Kinshasa, Andre Kimbuta.
Ratiba hiyo ilianza juzi katika viwanja vya Bunge la nchi hiyo mwili
wa marehemu Wemba uliagwa huku Rais Joseph Kabila akimtunuku nishani
maalumu kisha mwili wake ukarejeshwa nyumbani kwake katika Kijiji cha
Molokai.
Kisha mwili wa nguli huyo ulirudishwa tena kwenye viwanja vya Bunge
ambapo wageni mbalimbali walialikwa kutoa salamu zao za mwisho
wakishirikiana na wananchi wa kawaida na kusogezwa mbele hadi leo ili
watu wengi waweze kuuaga mwili huo.
Wakati hayo yakiendelea shuhuda mbalimbali za kumuelezea nguli huyo,
kuweka mashada ya maua na bendi yake aliyoiacha ilikuwa ikipiga nyimbo
za kuomboleza, huku vikundi mbalimbali vya ngoma na muziki navyo
vikipata nafasi ya kuomboleza msiba huo mkubwa.
0 comments:
Post a Comment