KAMBI ya Upinzani bungeni, imesema kitendo cha Serikali kusitisha
matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, kinazua maswali mengi, pengine ina
mpango wa siri wa kufuja fedha za umma katika matumizi yasiyo ya lazima.
Kauli hiyo, ilitolewa na Waziri Kivuli wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Japhary Michael wakati
akiwasilisha Hotuba ya Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na
matumizi Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2016/17.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kufuta mara moja
katazo la kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kupitia television ya
Taifa na vyombo vingine vya habari vilivyokuwa vikirusha matangazo hayo
awali, ili wananchi ambao ndio msingi wa mamlaka ya serikali wapate
haki yao ya msingi ya kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa fedha zao
katika bajeti ya serikali kutoka moja kwa moja bungeni.
“Wananchi wana haki kujua serikali yao inafanya nini na serikali
inawajibika kuwapatia wananchi taarifa juu ya utendaji wake wa kazi.
“Katika hali ambayo haijaeleweka bado serikali ya awamu ya tano
imeamua kwa makusudi kutumia mabavu kukataza urushwaji wa moja kwa moja
wa vipindi vya majadiliano ya Bunge ili wananchi wasijue kinachoendelea
bungeni.
“Ni muhimu wabunge wakafahamu, bajeti ya Tamisemi inayoombwa
kuidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2016/17, ni Sh trilioni 6.8
sawa na asilimia 23 ya bajeti yote ya serikali.
“Fedha hizi ni za walipa kodi, kujadili na kupitisha matumizi ya
fedha za umma nyingi namna hii bila wananchi kuwa na fursa ya kuona
jinsi Bunge lao linavyofanya kazi ya kuwawakilisha katika kazi hiyo, si
tu kuwakosesha haki, bali pia kunazua maswali mengi, pengine Serikali na
mpango wa siri wa kufuja fedha za umma katika matumizi yasiyo ya lazima
ndio maana haitaki wananchi wajue kinachoendelea bungeni,”alisema.
Alisema adhabu inayowafaa wabunge wa CCM ya kushabikia ufisadi, huku
wakipuuza maoni ya upinzani, ni kufutwa katika uwakilishi wa wananchi.
Alisema tamthilia inayofanyika hivi sasa ya waliokuwa watetezi
wakubwa wa ufisadi ya kutumbua majipu ni sawa na mchawi kutaka kurudisha
msukule wake ambao yeye mwenyewe ndiye aliyeuroga hadi jamii ikaamini
kuwa umekufa.
Japhary ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), alisema kambi
hiyo inaitaka Serikali kuleta muswada wa marekebisho ya sheria za
serikali za mitaa, ili sheria itamke kuwapa mameya na wenyeviti wa
halmashauri nguvu ya kiutendaji tofauti na sasa ambapo wanatambulika
kiitifaki.
“Pia tunapendekeza nafasi za kazi za wakurugenzi wa halmashauri za
wilaya, miji na majiji zitangazwe na waombaji wafanyiwe usaili kama
ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na si kwa uteuzi wa kisiasa kama
ilivyo sasa,”alisema.
0 comments:
Post a Comment