Saturday, April 30, 2016

UDA sasa sarakasi, MKANGANYIKO mpya waibuka kuhusu umiliki wa hisa za Kampuni

MKANGANYIKO mpya umeibuka kuhusu umiliki wa hisa za Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) baada ya Msajili wa Hazina, Meya wa Jiji la Dar es Salaam na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kutoa kauli zinazokinzana.

Kukinzana huko kwa kauli kulithibitika jana katika mkutano baina ya Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo).

Mafuru ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu umiliki wa hisa za UDA, alisema ameamua kuzungumzia suala hilo baada ya kuwepo mkanganyiko wa muda mrefu wa nani anamiliki nini katika kampuni hiyo.

Alisema taarifa zilizo ofisini kwake zinaonyesha kuwa awali Serikali ilikuwa inaumiliki wa asilimia 100 katika kampuni hiyo lakini mwaka 1985 iligawa asilimia 51 ya hisa hizo Halmashauri ya Jiji ambalo baadaye liliziuza kwa Kampuni ya Simon Group Limited (SGL).

“Taarifa ambazo tumezipata kupitia kikao cha wanahisa ni kwamba, SGL wamemaliza kulipia hisa zao katikati ya mwezi huu. Hisa hizo ni zile zilizokuwa zinamilikiwa na jiji, kwa hiyo sasa SGL ndiyo wamiliki wa asilimia 51 ya hisa zilizokuwa za jiji.

“Kwa sababu hiyo, UDA sasa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 49 na SGL kwa asilimia 51. Serikali inaitambua SGL kama mmiliki wa hisa hizo kwa vile jiji wamepokea pesa na kutoa risiti inayothibitisha wamekubaliana na muamala huo ni halali,” alisema Mafuru.

Alisema malipo hayo yalitakiwa yafanyike kabla ya Aprili 30 mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mahakamani lilitolewa baada ya jiji kufungua shauri la kutaka malipo hayo yafanyike.

“Jiji wamepokea pesa zao na wametoa risiti kuthibitisha wameukubali muamala huo ni halali na kuna ‘decree’ ambayo ipo mahakamani ya jiji kuiomba mahakama itoe agizo kwa SGL ifikapo Aprili 30, mwaka huu wawe wamekamilisha malipo vinginevyo wanyang’anywe hisa hizo na kurudishwa jiji jambo ambalo lilitekelezwa,” alisema Mafuru.
Alisisitiza kuwa Serikali imezingatia ushauri wa CAG unaoitaka ifuatilie masilahi yake UDA na imejipanga kusimamia miradi yote ya UDA kwa umakini ukiwemo mradi wa DART shirika hilo ni mwanahisa.

Wakati Mafuru akieleza hayo jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita ambaye pia alizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kupitia simu yake ya kiganjani, alisema jiji ni mmiliki halali wa hisa za UDA kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa bungeni na CAG.

Mwita alisema akiwa msimamizi wa mali zote za jiji ataendelea kusimamia mali za UDA hadi mwafaka wa umiliki wa hisa hizo utakapopatikana.

“Mimi nasimamia taarifa iliyotolewa bungeni na CAG kwamba mchakato wa kuuza hiza za jiji ulikosewa na Serikali iendelee kuzisimamia. Nikiwa na dhamana ya kusimamia mali zote za jiji lazima nizisimamie na kuhakikisha mwafaka unapatikana,” alisema Mwita.

Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa SGL imekamilisha malipo ya hisa hizo kwa jiji, alisema hana taarifa na kwamba Rais John Magufuli anapaswa kuingilia kati suala hilo ili wananchi wa Dar es Salaam wapate haki yao.

“Mimi sijui kama fedha hizo zimeingizwa labda kama mhasibu alipokea na namwomba Rais Magufuli aingilie kati suala hili kwa sababu ni zito na kama tunauza hisa ijulikane tunauza vipi lakini si kwa mchakato ambao CAG amesema ulikosewa,” alisema Mwita.

Meya huyo alisema wameanza mchakato wa kupitia mikataba yote ya jiji ili kubaini makosa yalipo na kwamba mjadala utakuwa wa wazi ili kila Mtanzania ajue ukweli.

Kwa upande mwingine, Ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni mapema wiki hii ilieleza kuwa mauzo ya hisa hizo yalikuwa na makosa hivyo ilishauri Serikali kuziweka mali za UDA chini ya usimamizi wake hadi hapo mgogoro wa umiliki wake utakapopatiwa ufumbuzi.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger