KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mara ya kwanza wametoa kanuni zao
ambazo zitatumika kama mwongozo kwa wabunge wanaotokana na vyama
hivyo.
Kanuni hizo ambazo zimeridhiwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai
inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika kwa
wapinzani kuwa na kanuni zao.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana Mkurugenzi wa Bunge wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema, alisema mchakato wa
kupata kanuni hizo ulipitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha
wabunge wa kambi ya upinzani ambao walizisoma na kusaini.
Kitabu cha Kanuni hizo chenye kurasa 24, kilitolewa jana na kusainiwa
na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kugawiwa kwa
kila mbunge wa upinzani hasa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
“Tumeamua kuwa na kanuni za kuelimisha Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni na awali tulifanya utafiti kwa nchi zote za Afrika hakuna kambi
ya upinzani yenye kanuni ila kwa Tanzania ni ya kwanza.
“Ni matumaini yetu nchi hizo zitakuja Tanzania kujifunza namna
tulivyotunga kanuni hizi, ambapo zimepitia hatua mbalimbali ikiwemo
kushirikisha vyama husika na unajua Kambi inaundwa na wabunge wa vyama
vinavyounda Ukawa.
“Imesomwa na kila mbunge na wote wameridhia na kuisaini kila mmoja na
baadae Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliridhia kuanza matumizi yake,
ninawapongeza wabunge wote wa upinzani kwa kuzikubali kanuni hizi ambazo
ndizo zitakuwa mwongozo wao,” alisema Mrema.
Mkurugenzi huyo wa Masuala ya Bunge wa Chadema, alisema anaamini
wabunge wote wa upinzani watazifuata kanuni hizo na kuwaongoza katika
majukumu yao ya kazi za kibunge.
0 comments:
Post a Comment