Friday, April 29, 2016

Rufaa Kupinga Kuachiwa Huru Abdallah Zombe na Wenzake kusikilizwa Leo

Abdallah Zombe (kushoto) akiwa na wakili wake, Richard Rweyongeza katika Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam

Mahakama ya Rufaa leo inatarajiwa kusikiliza rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na askari wenzake wanane waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.

Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Bernard Luanda, wengine ni Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles Kaijage. 
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alikata rufaa mwaka 2013, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyowaachia huru Zombe na wenzake, baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa inawakabili.

Katika rufaa hiyo, DPP anadai kuwa Jaji Salum Massati alikosea kuwaachia huru washitakiwa hao kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani wote. 
Mbali na Zombe, wajibu rufaa wengine ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam Zombe na wenzake waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, pamoja na dereva teksi Juma Ndugu.

Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Agosti 17, 2009, Jaji Massati aliwaachia huru washitakiwa kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao bila kuacha shaka na Mahakama ikiwaona hawana hatia kwa makosa yaliyokuwa yanawakabili.

Oktoba 6, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu hiyo kwa madai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, pia kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira unaotosha kuwatia hatiani washtakiwa wote.

Hata hivyo Mei 8, 2013 Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na dosari za kisheria zilizobainika kwenye rufaa, lakini DPP alipeleka maombi Mahakama Kuu ili aruhusiwe kukata tena rufaa nje ya muda. 
Mahamaka Kuu ilikubali maombi yake, akakata tena rufaa inayotarajiwa kusikilizwa leo.
Share:
Weka Maoni yako Hapa

0 comments:

Post a Comment

Become a Fan

Popular Posts

Copyright © GUMZO LA JIJI | Powered by Blogger