MBUNGE wa Ulanga, Gudluck Mlinga (CCM), amesema Waziri Mkuu mstaafu,
Mizengo Pinda, alitaka kuchomokea dirishani baada ya kutoswa katika
uteuzi wa urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka jana.
Mlinga ambaye pia ni mtoto wa marehemu, Selina Kombani, alitoa kauli
hiyo juzi jioni, wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Alisema baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhamia
upinzani na wenzake, Pinda naye alitaka kuwafuata, lakini akashtuka na
kubaki CCM.
“Yule mwingine alituzingua tukampiga chini akaenda upinzani, Pinda
naye mwaka jana alitetereka, tukamtosa akataka kuchomokea dirishani…
akashtukia akabaki, kwahiyo CCM hatufanyi mambo kwa kuambiwa kama
wanavyofanya upinzani,” alisema.
Kauli ya Mlinga ilionekana kumkera Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali
Keissy (CCM) ambaye aliomba kutoa taarifa: “Mheshimiwa mwenyekiti nampa
taarifa mzungumzaji, amemvunjia heshima Pinda kwa kusema alitokea
dirishani, afute kauli yake mara moja au athibitishe ni lini Pinda
alitokea dirishani… mtoto huna adabu, huna nidhamu,” alisema Keissy huku
akishangiliwa na wabunge wa upinzani.
Baada ya taarifa ya Keissy, mwenyekiti akamtaka Mlinda kuendelea kuchangia na kujikita kwenye hoja.
“Pamoja na umbile langu ndogo, leo nipo hapa kuwapa semina wabunge wa
upinzani. Huyo mwenyekiti wenu namfahamu kwa sababu nimeoa huko,
kwahiyo aibu yake aibu yangu, na hata ile hotuba yake aliandikiwa hapo
mlangoni… mimi ningekuwepo asingetoa.
“Wabunge wa upinzani waelewe nimewaambia natoa somo kwao na naomba
nitoe mfano mwingine. Haya mambo ya mnakaa hapa eti mwenyekiti kasema,
kila kitu mwenyekiti… mimi namfahamu huyo mwenyekiti wenu kwa sababu
nimeoa huko, tangu nampata binti yao yeye ni mwenyekiti, nimeoa yeye ni
mwenyekiti hadi nimezaa mtoto wa pili bado yeye ni mwenyekiti.
“Juzi nilisikitika sana kuna mmoja alikuwa anahoji mshahara wa Rais,
yeye anachangia chama Sh milioni tatu kila mwezi… sasa hizo fedha
zinakwenda wapi?” alihoji ,” alisema Mlinga ambaye alitumia muda wake
wote kuvishambulia vyama vya upinzani, huku akizomewa na wabunge wa
upinzani wakimwambia “teja huyooo”.
0 comments:
Post a Comment