NI wazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), imempa hasira Rais Dk. John Magufuli, baada ya kumsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Ally
Simba.
Rais amemsimamisha kazi Dk. Simba kutokana na kile alichodai
kushindwa kusimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa
usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), kitendo kilichosababisha nchi
kukosa mapato ya Sh bilioni 400 kwa mwaka – zaidi ya Sh trilioni 1 kwa
kipindi cha miaka mitatu tangu walipoingia mkataba na Kampuni ya SGS
Machi 22, 2013.
Uamuzi wa Rais Magufuli umekuja siku moja baada ya CAG, Profesa Mussa
Assad kuwasilisha taarifa ya ukaguzi kwa mwaka 2014/15 kwa wabunge
mjini Dodoma juzi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ikulu, Dar es Salaam
jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, ilisema
Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kufanya kikao kazi, kati
yake na viongozi, wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi,
Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
“Machi 22, 2013, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliingia
mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa
mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano.
“Lakini mpaka sasa, Kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele
kidogo kinachohusiana na udhibiti wa mapato ya simu ya ndani (offnet),
hali ambayo imesababisha Serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa Sh
bilioni 400 kwa mwaka,” ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na hatua hiyo, Rais Magufuli ametangaza kuvunja Bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja.
Pia amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa
Makame Mbarawa kuteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo mara moja.
Licha ya kutoa agizo hilo, Rais Magufuli amewataka Waziri Mbarawa,
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Faustine Kamuzora na naibu wake,
Mary Sassabo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji mapato ya
simu za ndani uanze kufanya kazi na nchi ipate mapato yanayostahili.
“Waziri nakuagiza chukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato
yote ya Serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya
yeyote atakayekwamisha jambo hili,” alisema Rais Magufuli katika taarifa
hiyo.
MIEZI 9
Dk. Simba amedumu katika wadhifa huo kwa miezi tisa tangu
alipoteuliwa Julai 6, mwaka jana na aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kwa mamlaka aliyopewa
chini ya sheria Na. 12 ya mwaka 2003 ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Mawasiliano Tanzania Kifungu cha 13 (1).
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Simba alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia.
TAARIFA YA CAG
Juzi akiwasilisha taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali bungeni,
CAG Profesa Assad, alisema TCRA inaendesha mfumo wa udhibiti wa
mawasiliano ya simu (TTMS) ambao unafuatilia mwenendo wa mawasiliano ya
simu kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano waliopewa leseni, bila njia
sahihi.
Alisema mfumo wa mawasiliano kwa sasa unaweza kudhibiti mapato
yatokanayo na mawasiliano ya kimataifa, lakini haujaweza kudhibiti
mapato yatokanayo na mawasiliano ya ndani.
“Kukosekana kwa mawasiliano ya kutosha kati ya taasisi muhimu
zinazoweza kunufaika na mtambo huu, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kumesababisha Serikali kuendelea
kupoteza mapato yatokanayo na mawasiliano ya simu za ndani,” alisema
Profesa Assad.
0 comments:
Post a Comment